The Chant of Savant

Monday 25 February 2013

Kiashiria cha mauaji ya padri Zanzibar hiki hapa.



Hakuna ubishi kuwa mauaji ya padri Evarist Mushi yalijulikana kabla ya kutekelezwa kama alivyosema kardinali Polycarp Pengo. Pengo alikaririwa hivi karibuni akisema, “Tumekuwa tukipokea vipeperushi toka kwa watu wanaojiita Uamsho, wakisema mapambano yanaendelea,”
Pengo alitoa hata ushahidi kwa kuonyesha kipeperushi walichotumiwa. Kwa maneno mengine ni kwamba serikali ilikuwa ikijua kilichokuwa kinaendelea ingawa haikutaka kuchukua hatua? Uko wapi mkono mrefu wa sheria? Uko wapi umakini wa vyombo vya usalama? Je nchi yetu ni salama? Sababu? Nadhani ni wakati muafaka kuitaka serikali ijibu madai ya Pengo. Si serikali tu. Hata Uamsho wanapaswa kujibu madai haya bila kuchelewa. Kwani kutofanya hivyo kutaonyesha moja kwa moja walivyo nyuma ya mauaji ya kinyama na kishenzi ya padri Mushi.
Ukiachia mbali na kitisho cha Uamsho, kuna mtu anayeweza kukamatwa na kueleza vizuri maagizo yake juu ya kuua viongozi wa kidini hasa wa kikatoliki. Katika pita pita zangu kwenye mtandao wa Jamii Forum, niliwahi kukutana na link hii http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/403448-majibu-kwa-hoja-ya-uchochezi-ya-ustaadh-ilunga-serikali-inamuogopa.html
Na link nyingine ni http://www.youtube.com/watch?v=NL9AkL0goTU
Sina wasi wasi. Vyombo vya usalama vinajua mambo haya. Haiwezekani mtu akurupuke na kuweka maagizo haya kwenye mitandao bila wao kuwa na habari. Kwa yeyote aliyebahatika kusikiliza mahubiri ya huyu anayejiita ustaadh Hassan Ilunga, atakubaliana nasi kuwa mtu huyu ni hatari kwa usalama wa taifa.
Kwanza, mtu huyu anaonekana kama aliyekata tamaa kiasi cha kutaka umaarufu kwa kuchochea umwagaji damu chini ya chuki za kidini baina ya waislam na wakristo. Ingawa wengi wanaweza kumpuuza na kumuona kama hamnazao, tukubaliane kuwa kuna hamnazo wenzake wanaoweza kuona mahubiri na maagizo yake kuwa ya kidini wakati siyo.
Pili, mhusika anaonekana kutokuwa na elimu ya kutosha kiasi cha kuhatarisha usalama wake na wa taifa kwa kutaka sifa zisizokuwa na msaada si kwake tu bali hata wale wanaomsikiliza na kuyazingatia maagizo yake.
Tatu, huyu Ilunga kama ni mzima kiakili, alipaswa kubanwa aeleze lengo la maagizo na mahubiri yake. Kwa mfano, katika moja ya mahubiri yake anasema kuwa akiuawa shehe basi auawe na padri. Ni bahati nzuri kuwa hakuna shehe aliyekwisha kuuawa Tanzania ukiachia mbali yule shehe anayeonekana kuabudiwa na Ilunga aitwaye Abdul Rogo aliyeuawa huko Kenya mwaka jana.
Je mauaji ya Mushi ni kulipiza kisasi cha mauaji ya Rogo? Maana, kwa mantiki ya hoja za Ilunga ni kwamba waislamu wote ni ndugu na atakapouawa mmoja mahali popote basi ni halali kuua mkristo sehemu yoyote duniani. Je huyu ana tofauti na makundi ya kigaidi kama Al Qaida au Al-Shabaab ambayo Rogo alikuwa akiitetea kwa udi na uvumba huku akimsifia Osama bin Laden kwa kumuita shehe?
Je mauaji ya Zanzibar ni mwendelezo wa kampeni za Al Qaida katika Afrika Mashariki? Maana ukisiliza mahubiri ya Rogo ukayaunganisha na ya Ilunga unapata jibu moja kuwa Al-Qaida imeishafungua cell Tanzania na Kenya.
Je vyombo vyetu vya usalama hata vya Marekani havijui njama hii ambayo imevishwa udini?
Nne, ni ajabu kuwa ustaadh Ilunga haelezi chanzo cha chuki baina ya waislam na wakristo. Wala hatoi suluhu ya chuki hii ya kupandikizwa na kuundwa na wachumia tumbo wanaotaka kuishi kwa kutumia mgongo wa dini hasa uislam.
Tano, kwanini serikali haikuchukui tahadhali hasa pale padri mwingine Ambrose Mkenda alipojeruhiwa kwa risasi hapo Desemba 25, 2011? Je ni sababu zipi zilizoifanya serikali kuendelea kutochukua hatua kama vile kuwakamata kuwahoji hata kuwafungulia mashitaka watu wanaoeneza chuki za kidini kama Ilunga?
Sita, yalipochomwa makanisa huko Zanzibar jambo ambalo limerudiwa siku tatu baada ya kuuawa kwa padri Mushi, kwanini serikali inaendelea kuzungusha bila kuchukua hatua mujarabu?
Kama msomaji atajipa muda wa kusikiliza mahubiri ya Ilunga, atakubaliana nami kuwa, kama vyombo vya dola vingekuwa na nia ya kutafuta waliotekeleza mauaji ya Padri Mushi, basi ina pa kuanzia ambako si pengine bali kumuweka nguvuni Ilunga ili awataje wenzake na kwanini wanafanya hivi.
Tunaweza kuendelea kujidanganya kuwa mauaji ya Zanzibar yanasukumwa na udini bila kujua kuwa kumbe yanaweza kubeba hata msukumo wa kisiasa hasa ikizingatiwa kuwa kuna wenzetu wengi upande wa pili wasioridhika na Muungano kiasi cha kutaka uvunjike kwa gharama na namna yoyote ili wapate madaraka ambayo wameyakosa kutokana na Zanzibar kuwa kwenye Muungano.
Tusidanganywe na vurugu za kidini tukasahau kuwa maadui wa taifa hasa mshikamano wanaweza kutumia upenyo na sababu yoyote kutudhoofisha ili wafanikiwe. Hata haya mauaji ya Buseresere ni ushahidi kuwa vyombo vya dola havifanyi kazi zake vilivyo. Maana hii si mara ya kwanza kwa chokochoko zenye harufu ya udini kutokea Tanzania. Nani mara hii kasahau kadhia ya uvunjaji mabucha ya nguruwe uliotokea chini ya utawala wa Ali Hassan Mwinyi baada ya baadhi ya waislam kudhani kuwa kwa vile rais alikuwa muislam basi wangepitisha ajenda zao za siri? Ni bahati nzuri kuwa wakati ule baba wa taifa Mwalimu Nyerere alikuwa hai na alimtaka Mwinyi wazi wazi kutoa msimamo wake ambao ulikuwa ni kuanzisha falsafa ya RUKSA.
Leo Nyerere hayupo. Watanzania tupo na urathi wake upo. Historia siku zote ni mwalimu mzuri. Kwa vile tatizo hili si mara yake ya kwanza kujitokeza, tungeshauri serikali na viongozi wake waache woga na uzembe. Kazi ya serikali yoyote ni kulinda uhai na mali za wananchi wake. Anapouawa mmoja kwa uzembe wa serikali, ingekuwa ni kwenye nchi za wenzetu, serikali ingetimuliwa madarakani. Kwa vile Tanzania hatujakomaa kwa kiwango hiki, kuna haja ya kuikumbusha serikali kuwa kulinda uhai na uhuru wa raia zake ni wajibu namba moja. Hivyo, tunatoa taarifa kama hizi kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake wa kulinda uhai, uhuru na mali za raia.
Kwa kuanzia tumetoa taarifa kuhusiana na Ilunga ambaye akishughulikiwa vilivyo licha ya kuacha kueneza sumu yake, anaweza kutusaidia kuwajua wenzake. Pia tunaweza kujua lengo lao la kufanya wanayofanya.
Kwa ukumbusho ni kwamba uislam hauruhusu matumizi ya vurugu na nguvu kuueneza. Ndiyo maana mtume Muhammad (SAW) alisifika kwa uvumilivu wake. Hawa wanaohubiri vurugu wasipewe nafasi. Hata waislam wa kweli wanapaswa kuwalaani na kuwafichua wao na hila zao. Kwa ufupi ni kwamba mahubiri ya Ilunga yanaelezea maandalizi ya kifo cha padri Mushi. Je watafuata wangapi? Je serikali inataka wafe wangapi ndipo ichukue hatua? Je serikali ina lipi la kutueleza ni kwanini isiwakamate akina Ilunga? Je inangoja wahubiri mapinduzi ya serikali ndipo istuke?
Tukubaliane. Na wakristo ni watu. Je wakiamua kulipiza kisasi au akatokea Ilunga wa kikristo serikali itamlaumu nani? na katika vita ya namna hii inapoanza haina macho. Watakaoumia ni pande zote hasa maskini, wanawake, wazee na watoto. Tuchukue hatua haraka. na hakuna haja ya kuogopa machafuko wakikamatwa wachochezi hawa kama wanavyoota. Waulize akina Ponda walipokamatwa si wamejikuta peke yao huku walichotegemea kisitokee.
Chanzo: Dira Februari 24, 2013.

3 comments:

Jaribu said...

Kumbuka "makafiri" ndio wanaotengeneza bunduki! Osama alitamba mpaka walipomuondolea uvivu.

Jaribu said...

Ndugu Mhango mbona unaniacha ninaning'inia hapo juu peke yangu? Wallahi watu wanaweza kunifikiria kuwa nimeanza kutafuna mirungi:-)

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Sijakuacha ukining'inia. Kuna kipindi watu wanatoa comments zenye kuharisha na kuchafua hewa hivyo hulazimika kuzifyeka bila kujali watasemaje. Pole sana ndugu yangu. Kuna kipindi natamani nitoe mawazo yangu lakini huchelea kuona kama najipigia debe.
Kila la heri ndugu yangu.