The Chant of Savant

Saturday 16 March 2013

Napanga kuanza kuuza mitumba na si maneno


Ingawa mimi si mtumba, napanga kuuza mitumba. Nimechoshwa na jamii ya mitumba. Kila kitu mitumba. Mitumba, mitumba mitupu.
Siasa za mitumba, maisha ya mitumba hata mawazo ya mitumba.
Kama wasomi mitumba, wanaghushi shahada na kuendelea kutoa hujuma badala ya huduma, ni ‘ki-mitumba-mitumba’, mimi nifanyeje?
Silalamiki wala kunung’unika. Nitauza mitumba amini usiamini. Heri niuze mitumba, ijulikane nauza mitumba badala ya kulazimishwa kuishi kama mtumba.
Mie sina mawazo ya mitumba wala elimu mtumba. Hata sera zangu kama nitauza mitumba, si za kimitumba. Ubongo wangu hata kama umejaa ulevi na bangi, si mtumba.
Najua wengi watajiuliza, ni kwanini ninabwabwaja kama vile nimewekewa mashine. Nina jibu. Baada ya Absalom Kibanda kutekwa, kushambuliwa na kung’olewa kucha na meno, napanga kuachana na uandishi wa habari.
Napanga kuanza kuuza nyanya au mitumba. Maana siko tayari kufanyiwa unyama kwa sababu ya taaluma.
Si juzi ‘majambishaji’ mitumba yaliyotumwa na `mafwisadi’ mitumba wenye ulaji, kwenda kumnyotoa roho jamaa.
Ninapoongea, nimetoka kupokea simu kutoka kwa mkewe ambaye amenitonya kuwa nifanye haraka, ima nitoweke au nifanye nijuavyo.
Amenisisitizia sana nihakikishe napotea kabla hawajanipoteza. Hivyo lazima nipotee, lakini niendelee kusikika nakushusha `mandogo’ na nondo ili kulijenga taifa.
Najiuliza, `ndata’ wanafanya kazi gani kama nao si mitumba? Mbona hawalindi uhai wangu jamani? Wanalipwa ‘njuluku’ zetu kwa kazi gani? Je, hao wanaonitawala kama nao si mitumba, wanafanya nini kuhakikisha nalindwa?
Si kuongeza chumvi wala kukufuru, nilitonywa na jamaa yangu wa ‘uhasama wa taifa’, kuwa nitafuatia kutokana na nyodo zangu za kilevi. Alinipa ‘laivu’ kuwa nondo zangu zinawanyima `wakubwa mitumba’ usingizi kutokana na kuwasuta na kuwaacha uchi.
Je, wanadhani nitaacha na kugeuka mtumba kama wao? Nikiacha kuchonga nitakufa. Maana, majaliwa yangu ni kulewa na kuchonga. Wao wanachonga ‘dili’ mimi nachonga maneno.
Ubaya uko wapi hapa hadi kustahili kunyotolewa roho bure? Kwa vile wenye `mamlaka mitumba’ wameamua kutugeuka na kuacha `manyang’au mitumba’ wachache watuue au kutuziba midomo, sibabaiki ng’o wala siach ikuchonga na kuchongoa.
Kwa vile mimi ni mjanja, nimegundua njia ya ‘kuepa’ mikono michafu ya mafisi hawa wanaokula waandishi wa habari. Napanga kuanza kuuza mitumba, huku nikibwabwaja ili niendelee kuwa na uhai na heshima vyangu. Siko tayari kuwa kanjanja au `nepi mtumba’ ya kutumiwa na `wakubwa mitumba’ kuwasafisha na kuisaliti taaluma.
Hivyo, natangaza rasmi kuwa nitaachana na uandishi active. Ila ulevi siachi. Hata nikiandika nitaandika kama muuza mitumba na si mwandishi wa habari.
Kwa vile nimesomea taaluma nyingi, naona nianza kuuza mitumba wakati nikitafakari nitatumia taaluma gani kati ya nyingi nilizo nazo, kuendesha maisha yangu.
Kabla ya kupanga kuanza kuuza mitumba badala ya maneno, nilitaka nibadili jina langu na kuitwa Nkwazi Kikwete, ili wauaji wa waandishi waniogope.
Japo nisingekuwa wa kwanza wala wa mwisho kufanya hivyo, ili kujiokoa na kutesa nilifikiria hivyo. Soma taratibu. Ninapanga kubadili jina langu na kuitwa Nkwazi Kikwete.
Najua nikibadili jina `waovu mitumba’ wataniogopa. Badala ya kutuma watu waninyofoe kucha na kuning’oa meno, wataanza kujipendekeza kwangu, ili nitumia jina la dingi wangu kuwafanikisha `madili’ yao mitumba.
Hapa bila shaka watanikatia kitu kidogo na kikubwa, hadi nami niwe milionea kama si bilionea kama wale wenye majina makubwa.
Nilimtonya Bi Mkubwa juu ya mpango huu. Binti wa watu alichachawa na kuogopa, utadhani nilikuwa napanga kuua mtu! Nilimtoa wasi wasi kuwa jina ni jina tu na hakuna anayeweza kulimilki peke yake.
Jina ni kama barabara. Yeyote anaweza kupita. Mbona kuna watu wanaitwa majina, tena mkubwa na ya maana kama vile Mohamedi, Paulo, Yohana na wengine wengi wanakunywa gongo na kuvuta bangi nami?
Mbona kuna watu wenye majina kamaa Maria, Haddijja na mengine wanafanya uchangu na haiwi `noma’?
Kwa vile mimi ni genius, naamini hata wajina wangu watafurahi kuwa na mtu mwenye ‘bongo’ linalochemka kama mimi.
Watafurahi kuwa na jamaa aliyepiga mabuku lakini akaishia kulewa na kuchonga kwa sababu ya kutawaliwa na sera za mitumba.
Hivyo, siku moja msishangae kukuta jina langu limebadilika hata kwetu. Lazima nibadili historia na kuiandika upya. Kwa mfano, usishangae naongelea home kwetu Bwagamoyo au Msogali kama siyo Lindi kwa mama yangu mzazi.
Nadhani kuna haja ya kubadili hata jina la Bi Mkubwa. Naona nitamwita Mwanaasha kama si Salama hata Salma ili kuendana na ukoo wangu mpya.
Pamoja na hii kuwa matokeo ya kugopa kunyotolewa roho, sababu nyingine ni kutaka kufaidi ujiko mtumba. Nataka nifaidi `ujiko’ wa baba yangu mpya kama wafaidivyo wale wa uzao wake.
Najua. Nikiitwa Nkwazi Kikwete nitakuwa na nafasi yakuwania ulaji na uongozi kwenye chama `twawala’.
Kwanini nisipate cheo kitokanacho na ubora wa ukoo wangu mtumba, ili niwale kama wale wanavyowala wale?
Hakika nikiwa na jina hili nitapata upendeleo mtumba. Nitaweza kupatiwa viwanja vya bure na hata tenda za biashara. Hata washirika wangu wanaonisumbua kwa `kunibomu’ wataanzisha biashara na kuukata simply because wanafahamiana nami.
Mpango wangu umenikumbusha jamaa aliyebadili jina na kujiita Kanjibhai. Alitajirika hivi hivi kwa kukopa kwenye mabenki simply because alikuwa akiitwa Kanji.
Bila `maujanja’ kwenye kaya ya walaji utaliwa. Lazima niwale kabla hawajafikiria kunila. Kwa vile nina ‘bongo’ linalochemka, nitafanikiwa bila kutoa jasho.
Kuna kipindi nilitaka nibadili jina niitwe Riz au Mira, ila niligundua kuwa kuna mwenzangu ambaye alishafanya hivyo. Hivyo, kwa vile umebaki ubin, nitatumia mwanya huu.
Wazungu husema: Kila unachofanya lazima uwe na plan B. kubadili jina naifanya plan B wakati nikijiuzia mitumba.
Nifanye nini iwapo `ndata’ wanasifika kuunda tume baada ya mtu kuumia, badala ya kuchukua hatua za makusudi kuzuia uovu huu tunaotendewa kwa sababu ya taaluma zetu?
Leo sitawananga. Kipo kigongo chao chaja kutaka wabinafsishwe kwa FBY, lau tupate usalama.
Najua wengi wanataona kama bangi na ulabu, vinanisumbua kiasi cha kuacha kazi ya heshima na kujiingiza kwenye kazi ya aibu. Heri nionekane mwoga. Maana kwa mwoga huenda kicheko huku kwa shujaa kikienda kilio.
Japo wengi watashabikia kuona nanyamazishwa na kugeuzwa muuza mitumba, wajue kama wote wanaochonga maneno kama mimi, watafanya maamuzi ya maana kama mimi biashara ya siasa itadoda kama si kufa.
Japo wanasiasa hawapendi kukiri hili, bila waandishi hakuna wanasiasa, hawatapata wa kutangaza biashara zao.
Nawahi mtaa wa Kongo kwenda kuuza mitumba!

Chanzo: Nipashe Jumamosi Machi 16, 2013.

No comments: