The Chant of Savant

Wednesday 24 April 2013

Kibanda ni nani? Wassira ni nani?


HAKUNA kauli imekera na kuhuzunisha wengi kama ile iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Steven Wassira aliyeuliza kwa kebehi kuwa ‘Kibanda ni nani?’
Kauli hii itokanayo na upogo na ulevi wa madaraka iliwakilisha mawazo ya serikali.
Maana tangu Wassira aliporopoka, serikali haikumkana wala kumkaripia. Hii maana yake ni kwamba kauli yake ni kauli ya serikali.
Wassira alikaririwa akiwa bungeni hivi karibuni akisema kuwa haamini wala haiingii akilini kuwa Usalama wa Taifa (TISS) wanaotuhumiwa wanaweza kumteka na kumtesa Mhariri Mtendaji wa Habari Corporation (2006) na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda Machi 5 kwa vile ni mtu mdogo.
Yaani si saizi ya TISS. Kumbe Watanzania tunatathimiana na kuthaminiana kwa matabaka!
Kukoleza kejeli na matusi yake ya nguoni kwa Watanzania, Wassira alisema kama wangekuwa wameteswa Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe au Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa ingeingia akilini! Je, kauli ya Wassira ilimaanisha nini? Je, kuna mpango wa kuwateka na kuwatesa Mbowe na Slaa? Je, kama TISS ‘wanashughulika’ na wazito ina maana Wassira anaweza kuwajua waliowaua watu maarufu kama vile Edward Sokoine (Aprili 12, 1984), Horace Kolimba (Machi 13, 1997), Lt Gen. Imran Kombe (Juni 30, 1996) na Zakayo Wangwe (Julai 20, 2008)?
Maana kauli ya Wassira kwa wachambuzi na wajuzi wa mambo inatoa hitimisho moja kuwa TISS ina jukumu la kuwateka na kuwatesa hata kuwaua wazito kama tuliowataja hapo.
Ni ajabu TISS hawakujitokeza kupinga wala kumkaripia. Je, walimtuma aseme aliyosema? Muhimu Mbowe na Slaa wawe makini wakijua fika wanatafutwa. Maana lisemwalo lipo kama halipo laja. Wassira hata kama ni mropokaji si mwendawazimu.
Laiti Jeshi la Polisi lisingekuwa linatumika kisiasa, lilipaswa kumbana aeleze anachojua kuhusiana na Kibanda.
Inasikitisha na kutisha kuona waziri mwenye hadhi ya Wassira kutojua hata haki za binadamu wala ukweli kuwa hakuna taasisi yoyote hata iwe kubwa namna gani yenye mamlaka ya kumtesa au kumdhuru raia hata kama ni msukuma mkokoteni.
Inasikitisha na kuudhi kuona waziri mzima hajui kuwa Watanzania wote ni sawa na wanapaswa kulindwa na serikali yao. Ni uzembe na mawazo mgando kiasi gani? Nitashangaa sana kama Rais Jakaya Kikwete hatamwajibisha kwa kumuaibisha na kumwangusha ukiachia mbali kumtukana na kumuonyesha kama kiongozi wa wenye mamlaka.
Hata hivyo, tumshukuru sana Wassira kwa kutoa mwanga kuhusiana na matukio yaliyotokea huko nyuma maana yalikuwa kitendawili kabla ya kutujuza haya.
Sasa tuangalie swali la Wassira ni nani? Kwa wanaomjua, Wassira ni mmojawapo wa wanasiasa wenye utata na wapenda madaraka.
Ni Wassira huyu huyu aliyekihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na NCCR-Mageuzi pale alipokosa nafasi ya kugombea ubunge mwaka 1995.
Ni ajabu kuwa Wassira huyu huyu anausakama upinzani uliomhifadhi kipindi kile alipokuwa amepigwa teke na CCM anayoitetea.
Kilichofanyika alipohama Wassira si kufaidi haki ya kikatiba ya kuhama toka chama kimoja kwenda kingine bali uchu wa kutaka kuwa mbunge alioupata kabla ya kuvuliwa mwaka 1996 na baadaye kuadhirika na kujirejesha CCM akijikomba na kupewa ulaji alionao sasa ukimlewesha na kujiongelea hata bila kufikiri.
Wassira ni kati ya wanasiasa ambao vinywa vyao vilishakata mawasiliano na vichwa. Hana tofauti na Peter Serukamba aliyetukana matusi mazito bungeni asichukuliwe hatua.
Wassira ni mbunge anayesifika kwa kusema hovyo na kulala bungeni akisingizia madawa bila kutoa uthibitisho.
Pia Wassira ni mwanasiasa mbabe na kichwa ngumu ambaye amethibitisha sifa hizi kwa kujiita ‘Tyson’ ambaye kila mtu anamjua alivyokuwa akijidhalilisha ulingoni hadi kufikia kumng’ata mwenzie sikio kama ishara ya kushindwa kuzuia hasira zake.
Wassira pia husifika kwa kuwatupia wenzake madongo hata juu ya madhambi anayotenda kama alivyowahi kusema kuwa wapinzani wanawaita wake za watu vyumbani wakati ndani ya CCM wapo wanaotuhumiwa kwa hili na wasijibu.
Je, Kibanda ni nani? Kibanda ni mwanataaluma ya uandishi wa habari na mwandishi wa habari mwandamizi na Mtanzania anayeishi kwa jasho lake na si posho za makalio ambazo upinzani umekuwa ukipigana ziondolewe.
Kibanda ni Mtanzania kama mwingine asiye na makuu wala asiyejisahau kama Wassira.
Ingawa Wassira anamuona Kibanda kama mtu mdogo asiyepaswa kuwa na thamani, kitendo hiki ni tusi kwa bosi wake yaani Rais Jakaya Kikwete ambaye alikwenda Afrika Kusini anakotibiwa Kibanda kumjulia hali.
Je, Wassira ana maana Kikwete alikwenda kule kumsanifu Kibanda au alikwenda kule kwa dhati? Kibanda anaweza kuonekana mdogo mbele ya Wassira lakini si mbele ya katiba ya nchi yenye jukumu la kuwalinda Watanzania bila kujali vyeo, kipato, rangi, dini, itikadi na mengine kama hayo.
Kwa ufupi ni kwamba Kibanda ni mtu mwadilifu asiye na hatia ambaye ni sauti ya wasio na sauti kutokana na taaluma yake ambayo anaitumikia kwa ufanisi mkubwa kiasi cha kuwatia hofu akina Wassira.
Kibanda si mwanasiasa nyemelezi na aliyefilisika kimawazo kama wale wanaouliza kuwa Kibanda ni nani?
Nadhani tofauti ya Kibanda na Wassira ni kwamba Kibanda si mropokaji, mjivuni wala mlevi wa madaraka.
Bila kusema mengi, tumalizie kwa kuwataka Watanzania wachukue tahadhari na watu kama Wassira na Taasisi ya Usalama wa Taifa ambayo imekuwa ikituhumiwa kuhusika na jinai mbalimbali kama vile kuteka na kutesa watu na kuwalinda mafisadi.
Ila ni vizuri Wassira na TISS wakajua kuwa wapo hapo walipo wakifaidi vinono hadi kulewa na kupayuka hovyo kutokana na madaraka na pesa ya Watanzania.
Hakika Mungu hamfichi mnafiki. Wassira amejifunua, kazi kwetu kumsoma na kufanyia kazi kauli zake.
Aliyosema Wassira yangesemwa na mbunge wa upinzani angekuwa ndani akisota. Kila kitu kina mwisho. Tumalizie na nukuu hii. “Sina ubongo… bali mrija.”
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 24, 2013.

No comments: