The Chant of Savant

Tuesday 11 June 2013

Makinda na Ndugai wanaonyesha udhaifu wao


KWA wafuatiliaji wa mitafaruku, ombwe na uongozi mbovu wa Bunge letu, watakubaliana nami kuwa kile kinachosemwa kuhusu kupwaya kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda   na Naibu wake Job Ndugai kunazidi kujidhihiri haraka sana na mara nyingi.
Matukio ya hivi karibuni ya baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuligeuza Bunge kuwa uwanja wa matusi yamewavua nguo wawili hawa ambao uongozi wao umeonyesha wazi ulivyo hatari kwa taifa letu.
Wawili hawa wamethibitisha wasivyojua demokrasia wala mipaka ya uongozi wao, ukiachilia mbali utawala wa sheria na uwajibikaji.
Haiingii akilini mbunge anaamka na kuwatukana wenzake matusi mazito kama ‘f**k you’ na spika hamchukulii hatua. Ajabu, Spika huyu huyu amekuwa hodari wa kuwanyamazisha, kuwaburuza hata kuwasimamisha vikao wabunge wa upinzani kama ilivyotokea hivi karibuni ambapo wabunge watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walifukuzwa bungeni bila sababu za msingi kisheria na kibunge.
Spika wa Bunge na Naibu wake licha ya kuonyesha udhaifu mwingi, wameonyesha upendeleo wa wazi. Wameonyesha wanavyotumikia serikali ya CCM zaidi ya wananchi waliowachagua. Unapofumkuza mbunge au kumsimamisha kuhudhuria vikao, unakuwa umewafukuza na kuwanyima haki wale waliomchagua awawakilishe.
Ukiachia mbali upendeleo, spika na naibu wake wameonyesha wazi walivyo kwenye madaraka kutumikia makundi fulani tofauti na dhana nzima ya kuutumikia umma wa Watanzania bila upendeleo wala uonevu.
Nilishangaa niliposikia Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) alipopinga kutengwa shilingi bilioni 29 kwa idara mpya ambayo rais anataka kuianzisha eti kufuatilia utekelezaji wa miradi wakati wizara na idara husika zipo.
Mdee aliposema kuwa hili ni chaka la ulaji, spika alikuja juu na kutaka afute kauli yake hata bila kumpa nafasi ya kumaliza hoja yake wala kutoa maelezo.
Lakini Mbunge wa Kigoma Mjini Peter Serukamba alipomwambia mwenzake ‘come on f**k you’ spika alinyamaza kana kwamba hili ni tusi dogo!
Kimsingi, Serukamba alitukana Watanzania wote akiwamo spika, ingawa spika hakuliona hili. Unaposimama bungeni na kurusha matusi unawalenga wenye Bunge ambao ni Watanzania wote.
Kama kulikuwa na fursa ya spika na naibu wake kuonyesha uongozi uliotukuka na siyo uliochafuka kama sasa, ilikuwa ni kwenye kipindi hiki cha kugeuzwa Bunge kuwa uwanja wa matusi bila sababu.
Bahati mbaya wawili hawa waliacha nafasi hii ikapita bila kuitumia kuonyesha ukomavu na uwajibikaji wao kwa wananchi.
Kadhia nyingine kati ya nyingi iliyoonyesha wazi upendeleo wa wawili hawa, ni pale mbunge wa viti maalumu, Christina Mughwai alipougua na ukatolewa ushauri na madaktari apelekwe India kwa matibabu zaidi. Hadi tunaandika Mughwai hajapelekwa India. Badala yake, kwa mujibu wa mdogo wake Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), familia ndiyo inahangaika kumpeleka Mughway baada ya Bunge kuwa linawapiga danadana kana kwamba kumpeleka mbunge huyu India ni hisani na si haki yake.
Lissu amekaririwa hivi karibuni akitoa kauli ya kukata tamaa. Alisema; “Walimshauri akasubirie nyumbani, ingawa hali yake sio nzuri.” Kwanini asuburi nyumbani kana kwamba huko ndiko kuna matibabu. Ni unyama kiasi gani kushindwa kutambua kuwa ugonjwa hausubiri ukiachia mbali mateso anayopata?
Je, Mughway angekuwa mbunge wa CCM wangengoja hivyo na kumshauri bila kufikiri kuwa akasubiri nyumbani? Mbona kwenye kulipana posho za vikao hawasubiri bali kukatiana papo kwa papo? Inakuwaje serikali inapata pesa haraka ya kushughulikia mambo mengine yasiyo muhimu kuliko pesa ya kuokoa uhai wa mbunge?
Si uzushi. Makinda na Ndugai wameshusha uwajibikaji na hadhi ya Bunge kwa kiwango kikubwa. Wamekuwa waanzilishi wa fujo kwa wakati tofauti bila hata kujifunza wala kujirekebisha. Mchezo wa kufukuza wabunge toka kwenye vikao umekuwa ndiyo alama ya Makinda.
Makinda ni spika atakayeingia kwenye historia ya nchi yetu kama spika muonevu na mbabe kuliko waliomtangulia. Imefikia mahali watu wanajiuliza: Makinda anawajibika kwa nani? Je, anafanya yote haya kumridhisha nani? Je, matendo ya Makinda na naibu yake yanaendena na masharti ya nafasi zao ambayo mojawapo ni kutokuwa na ushabiki wa kisiasa? Je, wabunge wataendelea kunyanyaswa na kushikwa mateka na watu hawa wawili hadi lini?
Kwa vile Bunge halina utaratibu wa maana na wa haki wa kumuondoa spika pale anapoonyesha kukosa sifa kama ilivyo kwa Makinda kutokana na chama chake kuwa na wabunge wengi, wabunge wanaoathirika wanapaswa kwenda majimboni mwao na kumshitakia kwa wananchi ili uchaguzi ujao wakiadhibu chama chake kutokana na kazi mbaya ya kada wake.
Ingawa CCM wanaweza kuona anachofanya Makinda ni kuwasaidia, kimsingi, kama wataangalia mbali, anaizika CCM taratibu. Kama wabunge watasimama na kutafsiri na kuelezea aina ya mateso na manyanyaso wanayopata kutoka kwa Makinda na naibu wake, uwezekano wa CCM kuathirika kwenye uchaguzi ujao ni mkubwa.
Maana unapomfukuza mbunge unamnyima fursa ya kuwatetea watu wake. Ni bahati nzuri kuwa si wabunge wote wa CCM wanakubaliana na madudu anayotenda spika na naibu wake. Hawa wakipewa motisha wanaweza kuleta mageuzi ya kweli ndani ya taasisi hii adhimu.
Ni vizuri wabunge wa CCM wakaelewa kuwa anachofanya Makinda kitawaathiri mbele ya safari. Ni vigumu kwao kuona madhara ya uongozi mbovu wa Makinda. Ila wafahamu kuwa kutokana na kuenea kwa mawasiliano na upashanaji wa habari, madudu ya Makinda yanajulikana kwa wananchi. Haiwezekani wananchi hata wapenzi wa CCM washuhudie hoja zinazolenga kuokoa pesa yao zinazimwa eti kwa vile zimeletwa na wabunge wa upinzani.
Watanzania wanajua machungu ya umaskini unaosababishwa na mfumo mbovu wa utawala ulioshindwa kusimamia kodi na rasilimali zao. Wanasikia madudu yote yanayoibuliwa na wakaguzi wa hesabu za seirikali kila mwaka ambayo ni chanzo cha umaskini wao. Watafikia mahali watachoka na hapa ndipo uhovyo wa Makinda utaitafuna CCM.
Tuombe Mungu Makinda na Ndugai waendelee kuonyesha udhaifu wao ili wananchi wautumie kuwaadhibu wao na chama chao.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 11, 2013.

No comments: