The Chant of Savant

Saturday 8 June 2013

Sasa mlevi atangaza kugombea urais

Hii si fununu si umbea na udaku. Kwa vile katiba mpya imetangaza rasmi kutambua mgombea binafsi, mlevi sasa natimiza azma ya kugombea urais kuwakomboa walevi. Japo niliwahi kugusia kuwa nina mpango wa kugombea urais, sasa natangaza rasmi; kwenye uchaguzi ujao nitakuwamo kwenye sanduku la kura.
Juzi nililewa na kuvuta kama sina akili nzuri. Nilikesha nikisherehekea hatua hii adhimu ya kuwakomboa walevi toka kwenye mikono michafu ya mafwisadi na majambaziii.  Naona yule anasonya.  Mwingine anacheka utadhani utani. Kwa taarifa yenu, nitagombea urais tena wa muunganiko na si wa Danganyika. Nataka niwe top boss wa kaya hii ya walevi ili niwaonyesha wavivu wa kufikiri jinsi ya kuongoza na si kutawala.
Huna haja ya kucheka wala kushangaa mlevi kugombea. Kama inawezekana kwa mafisi na mafwisadi kugombea, nini tatizo mlevi kugombea huu ulaji wa dezo? Kwa taarifa yenu, nina sifa zote za kuwa rais. Kwanza, nina elimu ya kutosha. Nina shahada gunia za PhD tena si za heshima wala za kughushi kama akina Emmy Nchimvi, Bill Lukuvi, Marry Nagu, Makorongo Mahanga,Didass Makalio na wengine wengi walioogopa umande ima wakaishia kughushi.
Pia nina sura nzuri ya kuvutia wapika kura ya kula. Afya yangu ni fiti. Hata nikinywa, kubwia na kuvuta sianguki kwa vile niko gado kishenzi. Hivyo, kwa sifa za haraka haraka mie ndiye kidume pekee anayefaa kuwa rais wa kaya hii inayohitaji mkombozi ambaye imemngojea kwa miaka mingi. Mie ni yule aliyetabiriwa na manabii kama Mchonga huku nikapigwa vita na mashetani kama yule habithi Shehe Yaya.
Pia nina mitandao ya kutosha ambayo lazima iingie viwanjani na kunisakia kura kwa udi na uvumba. Sina haja kuiibia Banki Kubwa wala kujiingiza kwenye biashara ya Kikagoda wala kuwatoa kafara walevi kwa wachukuaji waitwao wawekezaji. Mie ni mzalendo wa kupigiwa mfano.
Ili kuwashawishi walevi wanipe kula, nina mpango wa kufanya yafuatayo.
Mosi, nitatangaza mali zangu za bi mkubwa na vitegemezi na marafiki zetu.
Pili, nitaarifu walevi kuwa nikiingia madarakani, nitapunguza baraza la mawaziri. Nina mpango wa kuwa na mawaziri 20 tu ambapo watapatikana kwa njia ya kuomba kuajiriwa na si kuteuana wala kulipana fadhila.
Tatu, nikiishaingia madarakani, nitafuta cheo cha First Lady. Hili nalo juzi lilitaka kuvunja ndoa yangu na bi Mkubwa. Nilimwambia fika kuwa nikiwa rais sitaki nisikie habari za NGO za uongo na ukweli wala yeye kwenda kushindania vyeo vya kichovu kwenye chama changu na Pilau Mahanjumati Ulabu na Pilau (MUP).
Juzi kulikuwa hakukariki nyumbani kwangu. Maana baada ya kumwambia bi mkubwa kuwa sina mpango wa kumruhusu aitumie ikulu kufanya biashara alitangaza mgomo wa kila kitu kuanzia jikoni hadi kwenye bedroom. Nilipomtaarifu yaliyowapata marais kama Lora Gbagbo ambaye ananyea debe na mkewe, alinielewa. Bila kumuelimisha nadhani angeanza kuhujumu harakati zangu ya kuwania ukuu. Maana, baada ya kusema wazi kuwa utawala wangu hautakuwa biashara ya familia kama wale, bi mkubwa na vitegemezi vyetu walianzisha kigwena kuhakikisha sipati ukuu. Baadaye niliwahakikishia kuwa serikali yangu haitakuwa family business wala ya ubia kwa vile ni hatari ikitokea ukaondoka madarakani.
Baada ya waambia vitegemezi vyangu yanayomkuta yule jamaa wa Masri Mubaraak Kibaraak na wanae walinielewa wakakubali kuwa lazima kila mtu ale jasho lake. Ili kumridhisha bi mkubwa, nilimwambia kuwa kama katiba mpya isingefuta ubunge msukule bin underwear aka viti maalumu,ningempachika pale.
Nne, ili kuhakikisha nashinda, nitaanza kutangaza sifa zangu kaya nzima. Nina mpango wa kupeleka picha zangu wa wataalamu wa picha ili wafanya photoshopping niweze kuonekana kijana kuliko nilivyo. Kuanzia juzi napaka  piko kuficha mvi. Pia naitwa mzee kijana. 
Tano, nitahamasisha walevi wote kaya nzima wanipigie kampeni ya baa kwa baa. Sitaruhusu upuuzi wa kitanda kwa kitanda ili wasiambukizane miwaya kama wale wachovu waliokuwa wakitumia kampeni hii ya kimalaya. Wala sitaruhusu mambo ya mafiga matatu maana asili yake nayo ni uchangu.
Kwa waliofuatilia mikakati yangu siku zilizopita wanakumbuka nilivyotangaza neema kwa waandishi wa habari. Nawashauri kuanzia sasa wanipigie kampeni nishinde kitsunami na kuondosha kadhia ya kutekwa na kunyofolewa kucha na kutobolewa macho. Nawashauri wanoe kalamu ila wasitegemee kuteuliwa ukuu wa wilaya na mkoa. Wanipigie kampeni wakijua kuwa nia yangu si kulipana fadhila bali kukomboa kaya toka kwenye mikono michafu. This time around the kaya won’t go to the dogs anymore. Believe ye me everybody.
Kwa wasiojua chama changu kitukufu ni kwamba sera yangu kuu ni kuhakikisha kila mtu anapata uwezo wa kuweka mahanjumati na pilau mezani huku akishushia na ulabu. Nani asiyependa ulabu iwapo tunaambiwa hata peponi utakuwapo? Kwanini tusianza kuuramba ulabu kabla ya hata ya kufariki na kuingia huko peponi? Kwa maana nyingine ni kwamba sera yangu ni kuwaingiza walevi peponi kabla ya kurejesha namba. Mnaonaje sera hii walengwa?
Tano, ili kupata kura ya kula, nina mkakati wa kufanya kile wazungu huita miracles. Nitawambia baadaye hiyo miujiza.
Sita, nitafutilia mbali mikoa na wilaya vilivyoanzishwa kisiasa na kutengenezeana ulaji kichovu na kifisadi.
Saba, nitahakikisha naweka sera ya kuzuia watumishi wa serikali kuwa na nyumba ndogo; zinamaliza pesa ya kaya bila sababu. Pia ni mwiko kwa mtu kuiba wala kuficha pesa nje ya kaya.
 Saba, ili kuepusha mzigo kwa walevi, sitakuwa nikifanya ziara ughaibuni mara kwa mara.
Nane, nitasafiri ughaibuni mara nne kwa mwaka.
Tisa, nitakuwa nikiandamana na watu wachache ambao majina yao hayatafanywa siri kama ilivyo.
Kumi, tumekubaliana na bi mkubwa kuwa hataruhusiwa kudandia safari zangu unless otherwise.
Kumi na moja nimemshauri bi mkubwa atumie muda wake mwingi kujitafutia elimu badala ya kufikiri juu ya NGO za kufanyia biashara ikulu. Maana elimu yake ni ya UPE na alikuwa mwalimu wa chekechea.
Kumi na mbili nawataarifu wapiga kura na mashabiki wangu kuwa sitajiingiza kwenye biashara yoyote. Sitanyakuwa kiwanda wala mgodi wala sihitaji kuwekewa kinga kwenye katiba.
Kumi na tatu, nitabadili katiba na kutamka wazi kuwa rais akiiba,kufanya biashara ikulu au kushiriki ufisadi anyongwe.
Kumi na nne, natangaza kuwa hata nitakapokuwa nikisafiri kwenda uwanja wa ndege au matembezini sitahitaji misiruru ya magari na wala body guards. Vya nini iwapo sina mpango wa kumuibia mtu wala kuridhi tabia za kikoloni kama wengine?
Kumi na tano, nina mipango gunia. Mengine nitawaeleza siku za baadaye.
Kumi na sita, nawashauri wote mniamini na kunipa kula ili mpate kula. Hata nikiwaingiza mkenge mvumilie na wala msilalamike.

Kumi na saba, kula la heri.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Juni 8, 2013.

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

kila la kheri..ila hizo ahadi naona kama zimezidi zipo 19 si kumi na saba....

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Da Yacinta shukrani sana. Unajua tena. Ukiandika umetoka kuuweka lazima mambo mengine yajiweke. Ahadi zisikutie hofu. Mbona Njaa Kaya alitoa ahadi milioni bila kutekeleza hata moja na bado anapeta. We nitafutie kura ya kula nami nile dezo kama Njaa Kaya na jamaa zake au vipi?