The Chant of Savant

Tuesday 23 July 2013

Tunatawaliwa na watu wa aina gani?


Hebu fikiri. Yaani tangu mwaka 1940 hadi 1994 mtu anachimba madini ya thamani tena kwa tani na anakwambia kuwa hapati faida nawe unakubali? Hii ni akili au kichaa? Je, anayekufanyia ushenzi kama huu anakuchukuliaje zaidi ya kukuona kama kinyama mwitu tena kisicho na akili hata ya kujitambua?
TAARIFA za hivi karibuni zilizochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima kuwa mgodi maarufu wa almasi wa Mwadui wa Williamson Diamond Mine haujawahi kupata faida tangu kugunduliwa kwa almasi nchini ni ushahidi tosha kuwa nchi yetu inaendeshwa kiajabu.
Na hata hiki kinachopigwa upatu kuwa ni uwekezaji, si chochote si lolote bali wizi, uporaji na ujambazi wa mchana.
Haiwezekani mgodi wenye miaka zaidi ya 70 usipate faida na hivyo kutolipa kodi na mrabaha. Mgodi huu ulianzishwa na Mkanada Dk. John Thoburn Williamson (1907 –1958) mwaka 1940.
Hebu fikiri. Yaani tangu mwaka 1940 hadi 1994 mtu anachimba madini ya thamani tena kwa tani na anakwambia kuwa hapati faida nawe unakubali? Hii ni akili au kichaa?
Je, anayekufanyia ushenzi kama huu anakuchukuliaje zaidi ya kukuona kama kinyama mwitu tena kisicho na akili hata ya kujitambua? Akili ya kawaida inasema kuwa hakuna biashara inayoweza kuendelea kufanyika kama hakuna faida.
Kanuni ya asili ya biashara ni kwamba biashara isiyoingiza faida hujifunga yenyewe. Je imekuwaje mgodi wa Mwadui haujawahi kupata faida? Je, ni kweli kuwa mgodi huu maarufu haujawahi kuingiza faida?
Je, umekuwa ukiingiza faida na baadhi ya wajanja kulipana nyuma ya pazia? Je, kuna biashara kichaa kama hii?
Maswali ni mengi kuliko majibu. Kama kweli Mwadui Mine ilikuwa haipati faida ilikuwaje ikapata mteja wa kuinunua, yaani Petra ambayo nayo, kwa mujibu wa gazeti husika ni kwamba hailipi kodi kwa kisingizio kile kile cha mwaka 1947. kutopata faida.
Je, hawa watawala wetu wanahusika na uporaji huu ama ni kule kufumbwa macho na kuwaamini mno weupe? Ni ajabu kuwa hata ripoti hii ilipochapishwa hakuna aliyehangaika kukanusha au kutoa maelezo!
Huu ni ushahidi kuwa wahusika wa pande zote, yaani watawala na wawekezaji wanavyowachukulia Watanzania kama mataahira wasiojitambua wala kutambua mambo yanayoendelea kwenye nchi yao.
Hata hivyo, si kwamba wananchi hawajui. Wanajua sana. Tatizo lao ni woga na kujifanya hayawahusu. Ila ifahamike kadiri muda unavyokwenda wataamka na kudai haki yao tena kwa hasira za ajabu.
Tunaomba tuweke wazi kuwa hakuna jinsi ambavyo watawala hawanufaiki na jinai hii. Ushahidi wa wazi ni ile hali ya Bunge kuunda kamati ya kuchunguza kadhia hii na ripoti yake kuatamiwa na wahusika ili kukwepa kugusa maslahi yao.
Je, hawa ni akina nani? Umma unapaswa uwajue na kuwachukulia hatua.
Gazeti husika lilisema kuwa mgodi unaochimba almasi umewahi kununua mitambo ya kusafishia dhahabu badala ya mitambo ya kusafishia almasi. Hii maana yake ni kwamba wahusika hawachimbi almasi tu bali wanachimba na dhahabu.
Je, inakuwaje wawe na jeuri ya kufanya hujuma kama hii kwa taifa bila kuwa na wakubwa wanaowakingia kifua? Kwa wanaojua sheria kali za biashara za Kanada wanashangaa Wakanada wanavyoweza kutenda jinai kama hii bila kuwapo ‘mkono tena mkubwa wa mtu’. Je, watawala wa namna hii wanafaa kuendelea kutenda jinai yao huku wakitutoza kodi makapuku ilhali wanawakingia vifua wezi wakubwa wa kimataifa?
Laiti Watanzania wasingekuwa wavivu wa kufikiri na wendawazimu kiasi cha kuruhusu walevi wajifunzie kwenye vichwa vyao kunyoa, wangeamka na kuchukua hatua.
Kuendelea kuwavumilia majambazi hawa ni kujitia kitanzi hasa kizazi kijacho.
Je, Mwadui Mine wako peke yao? Wako wapi Wahindi wa Kampuni ya RITES walioingia nchini mikono mitupu na kuondoka na magunia ya fedha? Wako wapi akina Richmond waliojibadili majina kwenda Dowans na sasa Symbion Tanzania ambayo ilimchafua Rais wa Marekani Barack Obama kwa kuifungua ikimaanisha kuibariki na kuihalalisha?
Wako wapi kina Meremeta, Mwananchi Gold, Sukita, IPTL na wengine wengi? Je, tutaendelea na utaahira huu hadi lini? Kwa ujambazi huu wenye baraka zote za serikali, sichelei kusema kuwa watawala wetu ni majambazi wa kawaida walioaminiwa mali ya umma jambo ambalo ni kosa watakalojutia Watanzania maisha yao yote.
Yuko wapi Rais Jakaya Kikwete aliyeahidi kufuta au kurekebisha mikataba hii ya kijambazi? Mbona naye anatuhumiwa (kama ni kweli) kwamba alishirikiana na Edward Lowassa kuianzisha na kuiingiza nchini Richmond?
Nani mara hii amesahau maneno ya Lowassa kuwa kila alichofanya kuhusiana na ujio wa Richmond alimtaarifu na kumshauri bosi wake Kikwete? Je, hii ndiyo sababu ya Lowassa kuenguliwa na kulipwa mafao yake nyuma ya pazia na kuendelea kupigiwa debe na Kikwete?
Rejea maneno ya hivi karibuni ya Kikwete aliyekaririwa akisema kuwa Lowassa ni jembe.
Tulisikia kuwa Rais Obama alikutana na ‘mabilionea’ wa Tanzania mmojawapo akiwa Rostam Aziz aliyetuhumiwa kutumia Kampuni ya Kagoda kuchota fedha za EPA. Nani anahanikiza Lowassa na Rostam kwa mfano wafikishwe mahakamani?
Naleta hoja nikitaka Watanzania tufungue macho na kupambana na watu wanaotuibia waziwazi tukishuhudia. Na kama hii itaendelea, tusimlaumu Mungu wala mtu bali sisi wenyewe. 
Chanzo: Tanzania Daima Julai 24, 2013.

1 comment:

Jaribu said...

Kikwete mwenyewe ni tapeli. Wanawatumia wawekezaji kutuibia kwa sababu wanajua waswahili walivyokuwa wepesi kudanganyika, ukiwaambia tunapunjwa na wazungu wenyewe wanakubali. I bet you ukiwauliza wawekezaji kwa siri watakwambia kuwa faida yote wanagawana na Dr Dumbo.