The Chant of Savant

Thursday 11 July 2013

Uhovyo wa Kikwete wazidi kufichuka



Rais Jakaya Mrisho Kikwete anaingia kwenye vitabu vya historia ya Tanzania kama rais wa hovyo sana anayeweza kudhalilishwa hata kutapeliwa kirahisi kwa sababu ya kutokuwa makini na kupenda sifa.
Tangu aingie madarakani, Kikwete amekumbwa na kashfa nyingi sana zikiwemo zile za wizi wa pesa ya umma toka kwenye Benki Kuu chini ya jinai ya EPA, kuteua watendaji wabovu, kuuza nchi kwa wawekezaji, kupokea rushwa ya suti, kusaini sheria feki, kutumia vibaya madaraka na pesa ya umma, Richmond, kuruhusu mkewe kuunda NGO ya mashaka, kuruhusu watoto wake kutumia madaraka yake kujitajirisha na kutumia vyombo vya habari kuwahujumu wapinzani wake.
Kashfa nyingine zinazomkabili Kikwete ni kutumia vibaya jeshi la polisi na wananchi kwa manufaa yake kisiasa, kupewa orodha ya wauza unga na majambazi asiwachukulie hatua, kuunda mitandao hatari kwa taifa, kutumia udini na ukanda kujinufaisha kisiasa, kutoa ahadi za uongo, kuzurura, kuunda serikali kubwa, kuunda mikoa na wilaya mpya kuwanufaisha marafiki zake, kushindwa kuulinda muungano na katiba, kuendekeza kujuana na kulipana fadhila ambavyo vimekuwa vigezo na msingi mkubwa wa uteuzi wake, kutotangaza mali zake, kuwakingia kifua wahalifu kama vile walioghushi shahada na sifa za kitaaluma, kumkingia kifua rais mstaafu Benjamin Mkapa,mkewe, wakweze na watoto na marafiki na washirika zake, kuwakingia kifua marafiki zake wanaotuhumiwa kwa ufisadi na kuwapigia kampeni, kushindwa kusimamia uchumi wa nchi, kuendelea kuingia mikataba ya kijambazi kwenye sekta za uwekezaji na nishati, kutojua anachopaswa kufanya kama rais, kulea udini, kutawala bila sera wala dira, kutumia watu wenye kutia shaka kama vile Salva Rweyemamu, 'profesa' Julius Nyang'oro aliyeandika kitabu cha maisha yake, kuamuru polisi kuua wananchi, kuhujumu demokrasia nchini, kutelekeza na kulihujumu taifa kwa ujumla na nyingine nyingi.
Hivi karibu kuliibuka kashfa ya kutumia kihiyo na profesa feki kuandika kitabu cha maisha yake. Bahati nzuri blogu hii mnamo tarehe 6 May 2012 ilichapisha kashfa ya Julius Nyang'oro mwandishi wa kitabu cha maisha ya Kikwete. Ni baada ya kupata dokezo toka kwa mdogo wa Nyang'oro kuwa angetoa kitabu cha maisha ya rais Kikwete. Mdogo huyu wa Nyang'oro alikuwa rafiki yetu ingawa baada ya kukandia kitabu husika urafiki huu ulikufa.
Kashfa hii ya hivi karibuni imelipotiwa na vyombo vya habari nje na ndani ya nchi. Kwa habari zaidi kuhusiana na kashfa ya profesa huyu tapeli na kihiyo BONYEZA HAPA.Pia BONYEZA HAPA.

No comments: