The Chant of Savant

Saturday 17 August 2013

Sitta mnufaika wa Viti Maalumu aviita mzigo!


KWA miongo mingi walipa kodi wa Tanzania wamekuwa wakibebeshwa mzigo bila sababu wala ulazima wowote. Hakuna kitu kimekuwa kero kwa wengi hasa wenye kuzingatia uchumi zaidi ya siasa kama uwepo wa Viti Maalumu bungeni.
Licha ya kuwa mzigo kwa mlipa kodi, upatikanaji wa viti hivi umekuwa kitendawili kilichozungukwa na tuhuma nyingi za rushwa hasa ya ngono, kujuana, udugu, kulipana fadhila ukiachia mbali udhalilishaji wa kina mama.
Hivi karibuni, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, aliamua kuvitolea uvivu Viti Maalumu akisema wazi wazi vilivyo mzigo kwa taifa.
Sitta alikaririwa akisema: “Wanakwenda bungeni hawachangii, hawana hata hoja za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo, hawawezi kuwajibishwa na yeyote kwa mfumo uliopo na pia hawawajibiki popote, sasa huu si mzigo?”
Madai ya Sitta licha ya kuwa na muelekeo wa kuhami chama chake dhidi ya upinzani, hata hivyo, yana ukweli. Swali kubwa ni: Je, hawa wabunge wa Viti Maalumu licha ya kuwakilisha matumbo yao wanamwakilisha nani?
Kwanini kulipwa kodi za wananchi kwa kuwakilisha matumbo yao na wale waliowapa fadhila kama vile vyama vyao? Je, tunawahitaji wabunge wanaoonesha wazi wazi udhalilishaji wa kijinsia katika karne hii?
Je, ni kwanini wanawake nao wamekubali kudhalilishwa kwa kuhongwa vyeo vidogo na vichache ambavyo vimekuwa chanzo cha uhasama na mgawanyiko miongoni mwa wanawake? Sasa wakati wa kuwakomboa wanawake kutoka kwenye udhalilishaji huu ni sasa.
Hakuna kitu kinatia kichefuchefu kama kugundua kuwa viti maalumu kwa kina mama na vijana vilianzishwa ili kuwadhoofisha tayari kwa kutumiwa na wanasiasa katika uchaguzi.
Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya mwaka 2012, idadi ya wanawake ilikuwa kubwa kuliko wanaume katika mikoa yote ya Tanzania isipokuwa Mkoa wa Manyara wenye uwiano wa 101 kwa100 kati ya wanawake na wanaume huku Mkoa wa Njombe ukiongoza kwa wastani wa wanawake 100 kwa wanaume 88.
Hivyo, kwa wingi wao, kama wanawake na vijana wangeungana katika uchaguzi wowote, hakuna shaka washindi wangekuwa ima ni wanawake au vijana. Kwa kujua ukweli huu mchungu, tangu wakati wa chama kimoja, vilianzishwa viti maalumu kwa ajili ya kina mama na vijana ili kuweza kuwahujumu au tuseme kuwazuia wasiangushe mibuyu.
Walioanzisha mzigo huu kwa mlipa kodi, waliona mbali hasa ikizingatiwa kuwa wanawake wangegombea viti hivi vichache kiasi cha kusahau kuwashughulikia wagombea wanaume.
Ni bahati mbaya kuwa pamoja na idadi ya wanawake wasomi kuongezeka, wanawake hawakuliona hili na kama waliliona hawakulifanyia kazi.
Ni bahati mbaya kuwa mtego huu haukuwanasa wanawake peke yao bali hata vyama vya upinzani ambavyo navyo vina wabunge wa Viti Maalumu ambao watani wao huwaita wabunge wa misukule huku wanaowadhalilisha zaidi wakiviita viti vya chupi.
Wanaviita hivyo kutokana na kukumbwa na tuhuma za baadhi ya wanufaika wa viti hivi kuhonga ngono ili kupigiwa upatu na wakubwa vyamani.
Hata hivyo, mwandishi wa makala hii haungi mkono dhana ya kuitwa viti vya chupi hata kama kuna baadhi ya watu walivipata kwa njia ya kuhonga miili yao. Kwa vile sasa mazingira ya ushindani kisiasa hayana vikwazo vya kijinsia isipokuwa vya kiitikadi, umefika wakati wa kina mama kuachana na viti vya udhalilishaji na kujisimamia.
Tuna mifano hai ya wanawake walioachana na udhalili huu na kusimama na kushinda ubunge bila kutegemea kupewa kama vile Halima Mdee CHADEMA (Kawe). Beatrice Shellukindo na wengine wengi tu. Hivyo hofu ya kushindwa kwa sababu ya jinsia haina msingi tena katika mazingira ya sasa ya ushindani.
Nani anahijtaji wabunge wa Viti Maalumu wakati huko watokako kuna wabunge wa kuchaguliwa wanaowakilisha jinsia na rika zote? Nani anahitaji wabunge wanaokwenda bungeni kuligeuza kijiwe kwa kutokuwa na wanayemwakilisha wala hoja ya kuchangia bungeni?
Hata wakichangia michango yao mara nyingi ni dhaifu na wakati mwingine haipo kabisa.
Kimsingi, viti maalumu na vile vitokanavyo na kuteuliwa na rais ni mzigo na wizi wa pesa ya mlipa kodi maskini. Ni upanuzi wa hovyo wa serikali bila sababu ya msingi zaidi ya wanasiasa kuyafarakanisha makundi yenye idadi kubwa ya watu na kulipana fadhila kama si kutafutiana ulaji.
Hata hivyo, pamoja na Sitta kuuona ukweli, ‘sincerity’ yake inatia shaka ikizingatiwa kuwa mnufaika mkubwa wa kadhia hii ni mke wake, Margaret Simwanza Sitta, ambaye kupitia kadhia hii aliwahi hata kuteuliwa kuwa Waziri wa Elimu.
Je, Sitta amekumbuka shuka asubuhi au ni unafiki wa kawaida wa wanasiasa wa ‘fanya nikwambiacho lakini si nitendavyo?’ Je, Sitta ameliona hili ili aonekane ana uchungu na mlipa kodi hivyo kujipatia umaarufu kisiasa au kweli vinamuudhi?
Tukiachana na utata wa Sitta kuona ubaya wa viti vilivyomnufaisha, kuna ukweli usiopingika kuwa viti hivi ni mzigo unaopaswa kutuliwa hasa kupitia Katiba mpya inayosisitiza usawa wa kila hali.
Wakati wa kuachana na unyonyaji huu mkongwe umefika ambapo wanawake waelimishwe na kuachana na kupitia viti maalumu ambavyo kimsingi vipo pale kuwadhalilisha na kuwadhoofisha kama tulivyoonesha hapo juu.
Hatuna haja ya kuendelea kuwa na ubunge nyemelezi na dhalilishaji katika karne ya 21 ya maendeleo makubwa kidemokrasia.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili Agosti 18, 2013.

2 comments:

Anonymous said...

Huyu Sam Six si mtu wa kuchukuliwa "sirias" hata chembe! Heshima alijijengea alipokuwa "spika" wa bunge lile lililopita kabla ya chama chake kumpiga chini. Angekuwa "sincere" bora angeng'ang'ania kule kule CCJ ili kuonesha kutofautiana na "genge" lake. Lakini kwa kuwa, kama walivyo wengi wa aina yake, naye ni mchumia tumbo, ameamua kujifanya ni "mtetezi" wa kodi za mafukara wa Tanzania. Wizi mtupu!

Ninachokiona sasa ni kuwa hawa jamaa bado wanadhani dunia imelala. Wanadhani bado hizi ni zama za wananchi kuwapima "pafomansi" yao kwa kusoma Uhuru, Mzalendo na kusikiliza/tazama TBC tu. Hizo zama zimekwishwa, watu wanafahamu mbivu na mbichi sasa. Tena kwa kasi ya ajabu.

Ushauri wangu kwao: Wajipange!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon hapo juu
Mie siwashauri wajipange. Muda wa kujipanga ushapita. Kama ni kujipanga basi wajipange kukitoa kwenda kuzimu. Watu gani wasiojifunza na wanaoweza kufanya makosa kila hatua? Hivi bado kuna magazeti yanaitwa Uhuru na Mzalendo? Laiti ningepata wavuti wao!