The Chant of Savant

Saturday 10 August 2013

Tendwa alikuwa msajili au mnajisi wa vyama?


“KUTOKANA na utendaji dhaifu wa John Tendwa unaoegemea upande mmoja na uliojaa ‘propaganda’, Kamati Kuu ya CHADEMA imetangaza kuwa Tendwa ni adui wa demokrasia na hafai kuwa katika nafasi aliyonayo.”
Hayo ni matamshi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alipokuwa akijibu tishio la Msajili wa zamani wa Vyama vya Siasa, John Tendwa la Septemba 4, 2012.
Ugomvi wa Tendwa na CHADEMA japo ulikuwapo kwa muda mrefu kutokana na Tendwa kufanya kazi kwa kuigemea CCM, ulikolezwa na Tendwa kutishia kuifuta CHADEMA baada ya kumpelekea malalamiko dhidi ya serikali na Jeshi la Polisi kuhusika na kuihujumu na kuwaua wapenzi wake kama ilivyokuwa imetokea kwenye mkutano huko Arusha. Badala ya Tendwa kuwafuta machozi CHADEMA, aliamua kuwamwagia upupu ili kuwafurahisha waliokuwa wamempa tenda yake ya ulaji ya kuwa msajili wa vyama vya siasa.
Kwa wanaofahamu neno msajili na mlezi, watakubaliana nami kuwa lazima awe mtu mwenye hekima, ustahimilivu na matokeo ya kazi yake lazima yajulikana kupitia kuwaangalia wale aliowazaa hata kuwalea. CHADEMA wanaweza kukupa picha nzuri ya Tendwa kwa maneno mafupi hapo juu.
Leo tutamuangalia Tendwa aliyekuwa msajili na mlezi wa vyama vya siasa nchini. Kwanza, wanaokumbuka, alipoteuliwa na rafiki yake, rais mstaafu Benjamin Mkapa, alionekana kama mtu ambaye alikuwa hajulikani. Na kwa waliomjua walimjua kama mtu ambaye hakuwa na sifa wala udhu wa kufaa kwenye nafasi hiyo.
Na kweli punde si punde, baada ya kuingia kwenye Ofisi ya msajili wa vyama, badala ya Tendwa kujijengea sifa kama Msajili, alianza kujijengea sifa ya mnajisi kutokana na kutoa matamko yenye kupendelea Chama Cha Mapinduzi. Kwa wale waliodai kuteuliwa kwa Tendwa kulitokana na urafiki wake na Mkapa, walianza kupata la kusema: Si tuliwaambia.
Ni bahati mbaya kuwa pamoja na kuanza kuonyeshwa tathmini ya kazi yake muda mfupi alipokuwa ameingia ofisini kupitia maoni ya wananchi na vyama vya siasa, Tendwa hakutaka kusikia wala kuelewa. Aliendelea kufanya madudu kiasi cha vyama vya siasa kuzidi kuteketea huku msajili akizidi kuonekana kama mnajisi zaidi ya msajili. Je, kwanini Tendwa alijenga taswira mbaya hivi?
Kwanza, kama tulivyoeleza hapo juu, alipatikana kutokana na mazingira yenye kutia utata. Pili, inawezekana Tendwa ni kada wa CCM kutokana na kufanya kazi kama mwanasiasa zaidi ya mwanasheria. Kwa wale wenye wasi wasi na hili la kuwa kada kwa vile Tendwa ni mwanasheria, warejee jinsi wanasheria wawili tena majaji, Joseph Warioba na Mark Bomani walivyoweza kufikia hata kutaka kugombea urais kupitia CCM.
Je, waliwezaje kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kutaka kugombea urais kwa tiketi ya CCM kama hawakuwa na kadi za CCM? Je, waliaminije kuwa CCM ingewapitisha kama hawakuwa makada wa CCM? Maswali ni mengi ila la msingi hapa ni kwamba hawa majaji walikuwa na kadi za CCM kinyume cha sheria.
Kitu kingine kinachoweza kutajwa kama sababu ya kutobadilika kwa Tendwa ni ile dhana nzima ya kulipana fadhila au kuneemeshana kama inavyoendelezwa na CCM. Kama Mkapa alimteua ili apate mahali pa kulia na bado walikuwa na uhusiano mzuri nani alitegemea kuwa Tendwa angewajibika kwa vyama au watanzania?
Katika hili Tendwa hakuwa peke yake. Hebu kwa mfano rejea mawaziri waliotuhumiwa wazi kwa kughushi na bado wakaendelea kufumbiwa macho na kuendelea kuwa kwenye ofisi za serikali. Tuwakumbushe majina yao ambao ni Mary Nagu, Makongoro Mahanga, Emanuel Nchimbi, na William Lukuvi bila kusahau Dodorous Kamala balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji.
Pia unaweza kurejea watu kama Mnadhimu Mkuu wa Majeshi mstaafu, Abdulrahaman Shimbo, aliyeteuliwa balozi China. Hivi kama hana kadi au upenzi na CCM mwanajeshi na ubalozi wapi na wapi jamani? Watajwa hapo juu wasingekuwa makada unadhani wangeendelea kukingiwa kifua?
Kitu kingine kinachoweza kuonyesha ni vipi Tendwa alikuwa mnajisi wa vyama ni msimamo wake kuelekea na baada ya uchaguzi uliopita wa mwaka 2010 ambapo uchakachuaji wa wazi ulifanyika na rafu katika kampeni lakini bado Tendwa akakaa kimya au kutoa maonyo kwa vyama ambavyo havikuridhishwa na utendaji wake.
Tukio la hivi karibuni lililomvua nguo Tendwa akaonekana wazi kama kikaragosi cha watawala ni pale ilipozuka sintofahamu kuhusiana na haki ya chama kuwa na kundi la kujihami na kujilinda. Baada ya CHADEMA kutangaza kuwa itaunda kikundi cha namna hii ambayo kingeitwa Red Brigade, Tendwa kwanza alikubaliana nao lakini baada ya mabosi wake kuja juu, bila  chembe ya aibu, Tendwa aliwageuka CHADEMA na kuanza kutoa ushauri wa ajabu ajabu na hatimaye matishio kuwa chama hakina haki ya kuunda makundi ya kujihami ilhali CCM na washirika wake wa Zanzibar CUF wamekuwa na makundi haya kwa muda mrefu tu.
Wengi walihoji uwezo wa Tendwa hata kufikiri achia mbali kutenda. Kwa waliofuatilia utendaji wa Tendwa, watakubaliana nasi kuwa hakuwa anafaa kwenye nafasi hii nyeti.
Kwa vile Tendwa ni historia hata kama ya machukizo, wachambuzi na wapenzi wa demokrasia tuelekeze macho na mawazo yetu kwa Msajili mpya Jaji Francis Mutungi. Nikiri kuwa huyu bwana simfahamu. Ninachoweza kusema kuwa anapaswa kujifunza mambo makubwa mawili toka kwa mtangulizi wake.
Mosi, ni uteuzi utokanao na kujuana. Kama ana namna yoyote anayofahamiana na aliyemteua, kabla ya kumtumikia auulize moyo wake angetaka nini kama ‘legacy’ yake. Kama atakuwa mtu wa kufaidi ulaji basi Tendwa ni role model kwake. Kama atakuwa mtu wa kutumikia nchi yake, basi urafiki na kazi shurti vitenganishwe.
Jambo la pili, aepuke kuwa romote controlled na chama tawala kama ambayo Tendwa alikuwa. Ajue kuwa kuna maisha baada ya kustaafu ambayo ni muhimu kuliko hata wakati mtu akiwa kwenye utumishi. Hivyo, hatuna la kumkosoa jaji Mutungi bali kumshauri awe na jicho pana la kujifunza toka kwa mtangulizi wake ili naye asiishie kuwa mnajisi wa vyama badala ya mlezi.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 11, 2013.

No comments: