The Chant of Savant

Thursday 10 October 2013

Mwakyembe na sura nyingi za kutia shaka

DK. Harrison Mwakyembe mbunge wa Kyela na waziri wa Uchukuzi ni mtu mwenye sura na sifa nyingi. Kwa wasiomfahamu ni kwamba ni miongoni mwa vijana waliokuwa waandishi wa habari wakasomea sheria. 
Baada ya kusoma sheria na kufikia shahada ya Udaktari, Mwakyembe licha ya kufundisha kwenye kitivo cha sheria cha chuo kikuu cha Dar es salaam, alikuwa wakili maarufu wa kujitegemea kwa muda mrefu.
Kazi ya uwakili ilimjengea umaarufu kiasi cha kugombea ubunge na kushinda. Baada ya kuwa bungeni kwa kipindi cha kwanza, Mwakyembe alijizolea sifa baada ya kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond al maarufu kama Tume ya Mwakyembe. 
Kitu kilichomleta karibu na watanzania, kama mwenyekiti wa timu, ni kuweza kumshinikiza rafiki na mshirika mkuu wa rais Jakaya Kikwete, Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani kuachia ngazi kutokana na kubainika kuwa nyuma ya kashfa ya Richmond. Je Lowassa alikuwa peke yake kwenye kashfa hii? Jibu sahihi analo Mwakyembe, ambaye alikaririwa akimjibu Lowassa, alipodai kuwa alionewa kuwa anyamaze. 
Maana, kwa mujibu wa Mwakyembe, kama tume yake ingeweka mambo yote hadharani basi nchi isingetawalika. Wengi walidhani na kuamini baadaye kuwa alichofanya Mwakyembe na tume yake ni kuficha uhusika wa bwana mkubwa yaani rais. Hili halina utata wala ubishi. 
Kwani baada ya ‘kuficha mambo nyeti’ rais aliwapa uwaziri Mwakyembe na Sitta, aliyekuwa spika aliyeamuru kufanyika uchunguzi na ukuu wa mkoa Stella Manyanya, aliyekuwa mwiba kwenye tume husika.
Kwa waliotafakari maneno ya Mwakyembe kuwa kumbe kuna mambo yalificha, walianza kukosa imani na ithibati yake. Kwa mara ya kwanza kwa mujibu wa ushahidi wa mazingira na kukiri kwake, Mwakyembe alijionyesha kama mtu fisadi anayeweza kuhongwa cheo kwa gharama ya kuliangusha bunge na taifa.
Mara ya pili ambapo Mwakyembe alizoa umaarufu ni pale aliteuliwa kuwa naibu waziri na kudaiwa amelishwa sumu na wabaya wake kiasi cha kwenda nje kutibiwa. Wengi walimuonea huruma wakidhani kuwa alipewa sumu kutokana na uchapa kazi wake ingawa hili nalo ni tata. Maana tangu apone na kupewa uwaziri kamili, hakuweza kusikika akilalamikia hao ‘wabaya wake’.
Nyota ya Mwakyembe iliendelea kung’ara kwa kasi ya ajabu. Haijulikani kama ni kutokana na uchapakazi wake au kuwa karibu na wakubwa. Kwani alijionyesha kama mchapakazi na mtetezi wa maslahi ya taifa jambo ambalo lilizusha utata kwa wachambuzi wanaoendelea kuhoji mambo nyeti aliyoficha wakati wa uchunguzi wa kashfa ya Richmond.
Muonja asali haonji mara moja. Baada ya kunogewa na sifa, Mwakyembe alikuja na mpya ambayo ilifanya aonekane kama kiongozi wa aina yake ambaye ni nadra kumpata duniani hasa Tanzania. Alitangaza kuwa angewataja vigogo wa biashara ya mihadarati. 
Kwa kiasi fulani aliweka taifa kwenye hati hati huku viroho vya wengi vikidunda kutaka kuwajua hawa vigogo waliomshinda bosi wake kwa miaka nane tangu atangaze kuwa ana orodha yao. Siku ya siku ilipofika, watanzania walishangaa kugundua kuwa Mwakyembe alikuwa akitumia biashara ya mihadarati kutafuta umaarufu. 
Kwani licha ya kutowataja vigogo wa madawa ya kulevya, alijibainisha wazi alivyo mbabaishaji kama alivyosema katibu mkuu wa CHADEMA Dk. Wilbrod Slaa, hivi karibuni huko jimboni kwa Mwakyembe alipomtuhumu kuwa fisadi na mbabaishaji kutokana na kushindwa kuwataja wauza unga kama alivyokuwa ameahidi huko nyuma. 
Ni bahati mbaya sana kuwa Mwakyembe hakujitokeza kujitetea wala kujibu tuhuma. Hii maana yake ni kwamba tuhuma za ubabaishaji na ufisadi ni za kweli. Je ni kwanini Mwakyembe hakujitokeza kujitetea wakati ni haki yake kikatiba? Je aliogopa kumwaga mtama kwenye kuku wengi na kukubali yaishe akithibitisha ithibati na ukweli wa tuhuma? Kwa mwanasheria mahiri hili ni jambo la kuhuzunisha sana.
Ingawa tuhuma za Slaa zinaweza kuchukuliwa kama tuhuma za kisiasa, zina mashiko hasa tukiangalia tabia za Mwakyembe ambaye tumejaribu kudurusu historia yake.
 Wengi wanaojua uoza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanamshangaa Mwakyembe kwa mambo anayosema anataka kutenda ukiachia mbali kumshuku kuwa fisadi kutokana na chama chenyewe kuendeshwa kisanii na kifisadi. 
Mwakyembe amethibitisha hili katika kitisho chake cha kuwataja vigogo wa madawa ya kulevya. Alitufanyia usanii. Kwani hakutaja hata mmoja ukiachia mbali kutaja maafisa wadogo wa uwanja wa ndege ambao wanaweza kuwa ima walikuwa wakiruhusu unga kupita kutii maagizo ya wakubwa zao au njaa ndiyo ilikuwa ikiwasumbua. 
Hata hivyo, hili la pili linatia shaka ikizingatiwa kuwa mtandao wa vigogo wa mihadarati ni mkubwa na unaohusisha wakubwa kama alivyosema waziri Lukuvi hivi karibuni kuwa wakiamua kutaja wabunge hawatanusurika.
Kama kweli wahusika walihusika kwenye jinai tajwa, ni kwanini hawakupelekwa mahakamani ili haki itendeke? 
Mwakyembe kama mwanasheria anajua kanuni ya kumpata au kutompata na hatia mtuhumiwa? Je ni kwanini aliamua kuwafukuza wahusika kinyume cha sheria kama hakuna namna? 
Je huu si ushahidi wa wazi wa Mwakyembe kukiuka kanuni za haki za binadamu na utawala bora kwa makusudi? Je ikitokea waathirika wakaamua kwenda mahakamani kupinga hatua waliyochukuliwa kinyume cha sheria Mwakyembe atatwambia nini? 
Yapo mengi ya kuthibitisha madai ya Dk. Slaa dhidi ya Dk. Mwakyembe. Kwa mfano, nani mara hii kasahau jinsi Mwakyembe alivyoua kashfa ya Richmond . Wapo wanaodai kuwa Mwakyembe alikula dili na kuishia kupewa uwaziri ambapo yeye Samuel Sitta, na Stella Manyanya, walipewa vyeo vya uwaziri na ukuu wa mkoa. 
Ni bahati mbaya tena kuwa Mwakyembe hajawai kukanusha hili kama wakosoaji wanavyodai kuwa hili lilikuwa dili la kuua kashfa ya Richmond baada ya kumtoa kafala Lowassa.
Kitu kingine ni kwa Mwakyembe kushindwa kuwataja waliompa sumu. Hii inamwonyesha kama mtu muongo au mwenye kuweza kuzua mambo bila kujali athari zake kwa jamii.
Pia kushindwa kuwataja wauza unga aliokuwa ameahidi kuwataja kunamweka Mwakyembe kwenye kona mbaya ya ima muongo au mbabaishaji kama alivyosema Slaa. 
Kitu kingine kinachomharibia sifa na hata kuvuruga nia yake nzuri ni ile hali ya Mwakyembe kufanya mambo kwa nguvu ya soda na kukurupuka. Muulize. Yote aliyotangaza kufanya yamefikia au ameyafikisha wapi? Hatumsikii tena akishupalia wauza unga. Je amehongwa, kunyamazishwa au ilikuwa ni nguvu ya soda?
Doa la mwisho la Mwakyembe kati ya mengi ni ile hali ya kubaki ndani ya CCM akijua fika kuwa inaendeshwa kifisadi kiasi cha kutapatapa ili kuweza kunusurika na mabadiliko yanayoendelea nchini. Rejea CCM kuchakachua mswada wa katiba ili kujinusuru. Kwa mtu safi hili lingetosha kumuondoa CCM. Hakika hizo ndizo sura nyingi za utata za Dk Mwakyembe.

No comments: