The Chant of Savant

Thursday 12 December 2013

Natamani Kikwete atuumbue wakosoaji

  
Akiwa mkoani Geita, rais Jakaya Kikwete alikaririwa wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) kwenye Kijiji cha Katunguru/Nyamtelela wilayani Sengerema, mkoani Mwanza akisema kuwa wanaombeza wataumbuka ifikapo 2015. Heri ingekuwa hivyo. Hata hivyo, sijui kama Kikwete anayaona mambo kama yalivyo au anachukuliwa na wimbi la kujiridhisha na kujiisha pepo kwa kuona mawenge. Kama Kikwete anataka tunaombeza tuumbuke basi afanye yafuatayo:
Mosi, apambane na ufisadi uliomzunguka ambao hata hivyo, harufu yake ni kali kiasi cha hata kunguru kuihisi. Awawajibishe marafiki zake waliotuhumiwa moja kwa moja kujihusisha na ufisadi na uhujumu wa taifa. Nitaumbuka kama Kikwete atawashughulikia, kwa mfano, wezi wa Kagoda, EPA, Richmond, Sukita, Meremeta, Mwananchi Gold, Buzwagi na ujambazi mwingine. Nitaumbuka kama Kikwete atawashughulikia watuhumiwa wanaojulikana mfano Edward Lowassa, Nazir Karamagi, Rostam Aziz, Andrew Chenge, Peter Noni, Japhet Mangula, Idris Rashid na wengine wengi. 
Pili, ataje mali zake ili umma ujue ana mali kiasi gani na amezichuma vipi. Asisahau mali za mkewe ambaye kupitia NGO yake ya WAMA atakuwa bila shaka ana pesa ya kutosha tofauti na anayostahili kuwa nayo kihalali. Kama atavunja NGO hii ya shaka na kuwataarifu watanzania jinsi alivyogundua kuwa inamtia doa basi huenda tukaumbuka. Akiendelea na whitewash na window dressing asitegemee kuumbuka zaidi ya kuimarika zaidi na kupata la kusema.
 
Tatu, aandike katiba mpya isiyo na uchafu wala athari za chama chake. Nilishaliongelea hili kuwa Kikwete amshinde shetani anayemrubuni achakachue katiba ili kulinda maslahi ya chama chake. 
Nne, Kikwete atimize ahadi yake ya maisha bora kwa wote. Hili litasaidia kufuta kauli yake ya kushindwa isemayo'raha jipe mwenyewe' akimaanisha kila mmoja ajiletee maisha bora hata kama kufanya hivyo kunahujumiwa na ufisadi uliotamalaki nchini huku Kikwete akiangalia.
 Nne, ataje vigogo wa mihadarati ambao alisema ana orodha yao mnamo mwaka 2006. 
Tano, atoe maelezo kuhusiana na tuhuma kuwa yeye ni miongoni mwa mafisadi wakubwa waliotajwa na katibu mkuu wa CHADEMA,Dk Wilbrod Slaa  kule Mwembe Yanga, 2007 kwenye kile alichoita list of shame.Kwa kujua ukweli wa mambo Kikwete aliogopa hata kumtaka Dk Slaa alete ushahidi. Anadhani haya yamesahaulika ndipo atuumbue? Je hawa mafisadi wamelitia taifa hasara kiasi gani na pesa waliyofisidi ingejenga miradi mingapi? 
Sita, atoe utetezi wake kuhusiana na kuhusishwa na kashfa za EPA, List of Shame iliyotajwa hapo juu na Richmond ambazo amekuwa akikwepa kuziongelea.
Saba, asambaratishe utawala wa kujuana ambao umeshindwa kuwawajibisha watuhumiwa  wa kashfa mbali mfano, mawaziri waliotuhumiwa kughushi ambao ni Makongoro Mahanga, Mary Nagu, Emanuel Nchimbi, William Lukuvi na balozi wake nchini Ubelgiji Deodorus Kamala, katibu mkuu wa chama chake Abdulrahaman Kinana aliyetuhumiwa kujihusisha na biashara ya pembe za ndovu na wengine waliotamalaki kwenye chama chake na serikali yake. Asipowawajibisha na kuwajibika hata ajisifu na kujiridhisha vipi hatamuumbua mtu bali yeye mwenyewe.
Nane, ahakikishe anakusanya kodi na kuitumia kwa uangalifu na busara huku akiziba mianya ya ukwepaji na misamaha ya kodi vilivyotamalaki. Aachane na matanuzi ya kusafiri hovyo nje ya nchi akiandamana na misafara mikubwa kwa kisingizio cha kuomba. Huwezi kutegemea kuomba omba halafu ukajisifu kuwa umeleta maendeleo kiasi cha kuwazodoa wanaokupinga kwa haya.Mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe na si wafadhili ambao hutoa misaada na mikopo kwa maslahi yao na si yako. Laiti kama Kikwete ataacha nchi angalau imepunguza utegemezi kwa wafadhili ambapo bajeti ya taifa kwa sasa inawategemea kwa asilimia 40, huenda tukaumbuka.
Tisa, asimamie vizuri raslimali na pesa ya umma iibiwayo kila mwaka kama inavyofichuliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za umma.Imefikia mahali wezi wa fedha za umma wanajiona kama serikali ndani ya serikali. Rejea kiwango cha pesa zinazoibiwa kinavyoongezeka mwaka hadi mwaka huku kukiwa hakuna waliowajibishwa achia mbali namba ya wawajibishwa kuongezeka. 
Kumi, thamani ya miradi anayojisifia kujenga na kuzindua ifanane na miradi husika.Huwezi kusifia miradi ambayo imejengwa chini ya kiwango baada ya wahusika kukatiwa ten percent yao na kusunda nje kama ilivyotokea kwenye ununuzi wa rada mbovu na ndege ya rais. Maana ukiangalia kwa mfano shule za kata anazojivunia, licha ya kutokuwa na walimu wa kutosha, hazina vifaa muhimu na hata matokeo yake kila mwaka ni kilio kwa wazazi wenye watoto kwenye shule hizo. Hata pesa inayosemekana kutumika kuzijenga ikilinganishwa na shule zenyewe utakuta madudu matupu. 
 
Kumi na moja, awajibishe viongozi wengi waliotamalaki kwenye chama chake ambao anajua udhaifu wao ambao ni kikwazo kwa maendeleo ya nchi. Kwa mfano katika hafla hii alikaririwa akisema, "Mmekuwa hodari wa kushupalia dosari zinazosemwa na wapinzani na kuacha mazuri haya?”  Hapa anakemea tabia ya nyani haoni kundule ashakum si matusi. Ameona fika ubovu wa CCM kiasi cha kuamua kuwapasha wazi bila kujali watasuka au kunyoa.Hata hivyo, hawatabadilika kwa vile wanamjua mtu wao alivyo mwepesi wa kusema na mgumu wa kutenda.
 Kama wahusika mfano spika wa bunge na naibu wake wangewajibishwa, kungekuwa na sababu ya Kikwete kutuumbua. 
Kumi na mbili, Kikwete ahakikishe anafanya yaliyopendekezwa hapo juu ndani ya muda mfupi badala ya kuyafanya kwa mdomo na hotuba tamu majukwaani. Watanzania wamepigika sana chini ya utawala wa Kikwete. Hivyo, wangetaka kuona na si kusikia ambavyo Kikwete atabadili welekea wa mambo kutoka kwenye hali tete ya ufisadi na kutowajibika kwenda kwenye maadili na uwajibikaji. 

Mwisho, haitoshi kwa Kikwete kusema atawaumbua wakosoaji ambao siku zote amepuuzia ushauri wao wa maana na dhati. Sana sana, kama ataacha kutumia bunge kuwahujumu wapinzani, huenda anaweza kufanya hayo yanayopaswa kufanywa ili kuweza kuwasuta wakosoaji wake. Tunangoja kwa hamu sana Kikwete atusute vinginevyo siku ya siku tutamsuta yeye bila kujali kuwa ataacha serikali dhaifu na nchi iliyofilisiwa. Tutamuandama kama tunavyowaandama Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi walioweka mizizi ya ufisadi na uhovyo nchini.
Chanzo:Dira Desemba, 2013.

No comments: