The Chant of Savant

Wednesday 22 January 2014

Mzigo wote utuliwe, si sehemu tu

 You can add Mizigos.




BAADA ya kunyaka habari kuwa Chama Cha Majaribio (CCM) kiliwaita baadhi ya watu wake kuwahoji kuhusu kuongeza uzito kiasi cha kuwa zigo zito kwa ulaji wao, kijiwe nacho kimeamua kwenda hatua moja mbele.
Leo kitakaa kama kamati maalumu ya kuokoa kaya kuhoji sirikali nzima na kutaka ikitoe. Kijiwe hakina muda wa kutoa sanaa za kujipima na kufanya uamuzi wa hovyo wa kutowajibika.
Mpemba analianzisha. “Yakhe mmesikia sanaa za kuhojiana kuhusu ile mizigo iliyojaa njuluku ya umma?”
Msomi Mkatatamaa: “Yakhe umeamini hizo sanaa? Hujui jamaa wanataka kujikosha kwa waliwa kuwa wanawajali wakati wanawasanifu? Kwangu, kuhoji au kutoa fursa ya kujipima ni ufisadi wa aina yake. Kama mtu amebainika kuwa zigo bwaga chini. Hapa mzee Mizengwe Pinder sijui anangoja nini!”
“Msomi umenena. Hebu kwanza mmwagie kahawa mpaka azimie,” anasema Mbwamwitu.
“Niombe msamaha kwanza. Nimwagiwe hadi nizimie! No,” anasema Msomi kisha anamgeukia muuza na kusema: “Mmwagie huyo huyo anayetaka kuwamwagia wenzie kama anaona kumwagiwa kahawa ya moto ni jambo jema.”
Kijiwe hakina mbavu hasa ikizingatiwa kuwa Msomi huwa si mtu wa masihara.
Mgosi Machungi anakwanyua mic: “Wagoshi tiache utani. Hamijui kuwa tinaanza mwaka? Jamaa wamiona watiingize mjini kwa kujifanya wanatijali wakati wanatiibia kila uchao. Sasa niaminini. Ngojeni mione kama kuna mizigo itatimuiwa zaidi ya kuyamaiza kichama kama kawaida yao. Hawana lolote hawa. Wamefiisika kama alivyowahi kusema jamaa fuani.”
Mipawa anadandia: “Mgosi jana ulikulaga nini? Maana naona una mipwenti kama Juliyasi! Kwa ufupi, kama ni kuhoji, basi sirikali nzima ilipaswa kuhojiwaga na kutimuliwaga kabla ya kuzusha machafuko siku si nyingi. Sisi kwetu Ng’wanza tumeishasema kuwa kuna siku patachimbika bila jembe. Maana ubabaishaji umezidi.”
Anakunywa kahawa na kuendelea: “Kila mwaka wamekuwa wakiwakopa pamba wakulima halafu huyu Kinamna na Mapepe Ninaye wanakuja kutusanifu eti kwa kuwahoji mawaziri. Watoke wote kwani wameshindwa kusimamia shughuli za kaya. Wanachojua ni kuua wanyama wetu na kuiba fedha na kuficha ughaibuni.”
Kanji uzalendo umemshinda. Anakula mic: “Dugu yangu, this time chama iko very serious. Nyinyi taona. Mimi jua chama tafuta kazi ile yote zigo.”
Bi Sofi aka Kanungaembe anamuunga mkono Kanji. Anakatua mic: “Sioni haja ya kuwa na haraka. Nyie ngojeni mjionee. Mtukufu kama alivyowahi kusema atawaaibisha wakosoaji.”
Kapende anadandia: “Kwenda huko na ndoto zenu uchwara. Amuaibishe nani wakati yeye alishaaibika miaka mingi? Kanji na Sofi sijui mmeingiliwa na nini. Maana huko nyuma hamkuwa hivi. Nyie ngojeni kusikia mwandishi fulani wa habari amevamiwa na majambazi na kuuawa ili kuhamisha mjadala kama ilivyotokea kwa akina Ulimboooka na Kibaaanda.”
Msomi anarejea: “Hebu tuwe serious kama Kanji anavyoona. Je, kuna mtu nambari wani anayepaswa kuitwa mzigo na kuhojiwa kama Njaa Kaya ambaye kila uchao yuko kwenye matanuzi ughaibuni? Ana bahati yupo mzee Mizengwe anayetwishwa mzigo wake kila uchao. Hivi kuna bomu kama jamaa mwenyewe ambaye amewajaza jamaa zake kwenye ulaji halafu eti anajifanya kuendesha kigwena cha kuwajadili? Shame on you! Go tell it to the birds. Wa kuondoka ni wewe na genge lako lote.”
Anakunywa kahawa na kuendelea: “Najua wanywanywa wake watasikia vimondo vyangu na kumpelekea taarifa. Wakamwambie kuwa tumechoka na sanaa na rongorongo zake. Hakuna cha kuhoji wala kuhojiwa bali kukitoa maana wameshindwa kulhali. Na wakiendelea na sanaa hizi mie lazima mwaka ujao nimtokee mtu liwalo na liwe.”
“Msomi tuko nyuma yako,” anadakia Mbwamwitu.
“Nyuma yangu kufanya nini? Mmekuwa nyuma yao kila siku na hakuna mlichofanya zaidi ya kuendelea kuliwa huku mkijiona.”
Mgosi kaguswa pabaya. Anakatua mic: “Kwei wapo wengi wanaoiwa hasa Kanji na Sofi wanaotetea huu uoza. Sisi kue Ushoto tishaazimia kuhakikisha tinachagua upinzani.”
“Mara hii mmeishamchoka mtoto wa Makambale mliyebambikiwa?” anahoji Mchuguliaji aliyekuwa kimya muda mrefu.
“Timchoke maa ngapi. Sisi si wajinga kuendeea kuwa na mzigo wa Makambae. Titamtimua tu.”
Kapende anamnyang’anya Mgosi Machungi mic. “Naona tuazimie kama kaya nzima badala ya vipande vipande. Kwanini tusiamue kuitaka sirikali ikitoea baada ya kuchemsha. Hebu waulize. Ziko wapi njuluku zetu zilizofichwa ughaibuni?
Wako wapi wauza bwimbwi ambao mkuu amekalia majina yao? Yako wapi maisha fit kwa wachovu wote? Uko wapi uwajibikaji ambao sasa umegeuka uhojianaji?”
“Du! Inaonekana jamaa mmegeuka wanasiasa, tena wabukuzi kweli kweli. Yaani mnachambua mambo kuliko hata maprofesa wa chuo cha Manzese akina Baaana na wenzake wanaojikomba kwa genge la walaji!”
“Ulikuwa hujui kuwa kijiwe ni chuo kikuu na kile ni chuo cha Manzese siyo? Hapa ndipo kwenyewe mwanangu,” anachomekea Mbwamwitu.
“Tuache utani. Nadhani hiki kinachoitwa kuhojiwa na kujieleza ilikuwa janja ya kutaka kubadili baraza la ulaji hasa baada ya yule manzi aliyevurunda kwenye Uno kupewa ulaji ili akateuliwe. Mengine rongorongo. Nani alitegemea nyani amhukumu ngedere kwa kosa la kula mahindi wakati wote lao moja?” anazoza Msomi.
Mzee Maneno aliyekuwa kimya anaamua kuchomekea: “Da! Msomi umenifumbua macho. Kumbe ndiyo maana Kinamna na Mapepe waliamua kulianzisha wakiwa vijijini na yule manzi! Sasa nimeelewa.”
Mpemba anakwanyua mic: “Yakhe hii yaweza kuwa kweli. Maana ukiona huyo manzi alivyoteuliwa haraka haraka na kuwekwa mbele lazima kuna jambo wallahi.”
Sofia anaonekana kuudhika. Anakula mic: “Wewe ulitaka awekwe nyuma wakati ana sifa zote? Huyu ni mkombozi wa akina mama.”
“Mkombozi wake anabebwa na kushindwa kujikomboa hadi abebwe. Si akagombee tumuone,” Mzee Kidevu anazoza.
“Mie naona tusizungushe. Kwanini tusijipange tukawatokea huko Dom na kuwatimulia mbali kwa kuangusha kaya yetu?”
“Twende sasa, twende saaa…” Kijiwe kilihanikiza isipokuwa Kanji na Sofi walioamua kuondoka haraka.

Tulipokuwa tukijiandaa kwenda si umeme ukakatika! You know what. Tusingeenda bila kuonana.
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 22, 2014.

No comments: