The Chant of Savant

Wednesday 26 February 2014

Kalenga watachagua ukoo au ukombozi?

 

PAMOJA na kuwa na ustaarabu wa miaka mingi, Bara Hindi linasifika kwa mifumo ya kibaguzi chini ya mfumo wa ‘caste’, unyanyasaji wa kina mama na ubaguzi wa watu wengine hasa wasio Wahindi.Pamoja na mfumo huu kuwabagua hata kuwanyanyasa kina mama, una udhaifu mmoja ambao ni kuabudia madaraka na wenye nacho. Hapa ndipo siri ya wanawake kama Indira Gandhi na Sonia Gandhi (India), Benazir Bhutto (Pakistan), Sirimavo na Chandrika Bandaranaike, (Sri Lanka) na Sheikha Hassina bint Mujibur Rahman (Bangladesh) walikuwa maarufu na kuvuka vikwazo wanavyopambana navyo wanawake wengine kwenye Bara Hindi, kwa sababu wazazi wao walikuwa watu maarufu, wenye ushawishi kisiasa na kiuchumi.

Hivyo, kwa kupitia majina makubwa ya baba, waume au wakwe, mabinti hawa walitokea kuwa maarufu.


Tanzania hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) taratibu kimeingiza nchi kwenye siasa za Kihindi, ukiachia mbali uwekezaji hata ujenzi na biashara za Kihindi.  CCM bila aibu wala kujali malengo ya waanzilishi wake waliolenga kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye unyonge, umaskini, ujinga, ubaguzi, magonjwa na maadui wengine, wameamua kuingiza nchini mfumo huu wa kilafi na baguzi ili waendelee kuhodhi madaraka ya taifa letu.
Ushahidi wa hivi karibuni ni kuteuliwa kwa mtoto wa kiume wa aliyekuwa Waziri wa Fedha na mbunge wa Kalenga marehemu William Mgimwa, aliyefia nchini Afrika Kusini mwanzoni mwa mwaka huu, kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mdogo.
Ukiuliza huyu bwana mdogo ana nini cha mno kisiasa zaidi ya jina la baba yake hakuna jibu linaloingia kichwani.
Walifanya hivyo Arumeru Mashariki alipofariki dunia, Naibu  Waziri wa Fedha, Jeremiah Sumari, kwa kumchagua mwanae Sioi kupeperusha bendera lakini akabwagwa na Joshua Nassari wa CHADEMA, baada ya watu wa Arumeru Mashariki kukataa siasa za kurithishana na majina makubwa badala ya sifa.
Je, tutegemee hili kujirudia Kalenga? Je, wapiga kura wa Kalenga watabariki au kukataa utawala wa kurithishana ambao umezalisha wanasiasa watokanao na majina ya baba zao kama vile Aman Abeid Karume, Ali Karume, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Vita Kawawa, Zainab, Adam Malima, Januari Makamba, Violet Mzindakaya,  Emanuel Nchimbi  na wengine wengi?
Kwa wanaojua majukumu na wajibu wa mbunge kwa wapiga kura, watakubaliana nasi kuwa sifa kubwa anayopaswa kuwa nayo ni kukubalika kwa wapiga kura na kuwa na sifa za kufanya akubarike zaidi ya jina kubwa la baba au mama yake.
Unapochagua mtu kwa kuzingatia ukubwa wa jina la wazazi wake, unakuwa unalirudisha taifa nyuma na kukiuka msingi mmojawapo wa mapambano ya uhuru wa taifa letu ambalo ni kuondoa ubaguzi wa aina yoyote.
Tunasema ubaguzi kutokana na wakubwa wenye majina makubwa walio au wanaotaka kuwarithisha madaraka watoto wao kuwaandaa kwa kuwadhulumu maskini. Kwa mfano, wakubwa hawa wamefanikiwa kuvuruga na kuharibu mfumo wa elimu yetu huku wakisomesha watoto wao nje kwenye elimu bora wanayotumia kama kigezo cha kuwarubuni wapiga kura.
Ni ajabu kwa wazazi au jamaa wa vijana wanaohenyeshwa kwenye mikopo na kusomea kwenye mazingira magumu kuchagua watoto wa wateule waliosoma ughaibuni.  Je, mtu aliyesoma nje tena kwa pesa na kodi za wapiga kura anafanana nao?
Je, wananchi wa kawaida hasa wa mashambani kama Kalenga wanapaswa kumchagua mtu huyu asiyefanana nao? Watakuwa wendawazimu kama watafanya kosa hili hata mgombea husika angetoka chama kinachopendwa vipi.
Mbunge lazima afanane na wale anawawakilisha na si kuwatumia kama mtaji wa kuendeleza jina la baba yake. Mgombea namna hii hatafuti ubunge kuwatumikia wananchi bali kutimiza malengo yake na ukoo wake hasa kuendeleza jina la baba au mama yake na kuendelea kuwatumia wananchi kuchuma utajiri.
Tunaposema mfumo wa kisiasa wa Kihindi tunamaanisha hali hii ya baadhi ya koo kama tulivyoona hapo juu kuwatumia watu maskini tena waliosababishiwa umaskini na koo hizi hizi kuendelea kuwatumia kwa kisingizio cha kuwatawala.
Huu ni ufalme fichi na wa kijanja wa Kihindi, sawa na ufalme na uemir wa Mashariki ya Kati. Tofauti ni kwamba inatumika demokrasia kama vile uchaguzi kuhalalisha ufalme huu wa kinafiki na fichi.
Koo, hizi licha ya kuwaona wapiga kura kama punda wazibebao, zinawachukulia kama watu wasio na akili sawa sawa, ambao wameshindwa kujitambua na kutumia nguvu yao ya kura kuziondosha kwenye ufalme fichi unaoanzia baba kuelekea mwana hadi wajukuu. 
Ukweli huu ulifichuliwa na Katibu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba, aliyesema kuwa hakuna awezaye kumzuia mwanae kuteuliwa waziri.  Kweli baada ya muda mfupi, aliteuliwa na kuwa waziri. Tumeyaona haya kwenye kashfa zilizowahusisha watoto wa wateule kama vile Hussein Mwinyi –  Waziri wa Ulinzi aliyevurunda wizara hii mara mbili na kurejeshwa hata baada ya milipuko ya mabomu kuuwa watu wasio na hatia mara mbili asiwajibishwe.
Tumeyaona kwenye kashfa ya Adam Malima na jinsi ambavyo amekuwa akirejeshwa kwenye baraza la mawaziri si kwa sifa yoyote bali jina lake la ukoo. Je, watu wa Kalenga watabariki jinai hii au kuikataa kama wenzao wa Arumeru Mashariki?
Je, watashabikia ukombozi au umwinyi na ufalme wa Kihindi ambao hautawapeleka popote zaidi ya kuwarejesha kwenye zama za mawe? Je, watajitambua na kutoa somo kama walivyofanya watu wa Arumeru Mashariki ambao wameingia kwenye vitabu vitukufu vya taifa letu kwa kujitambua na kuleta ukombozi kwa kukataa utawala wa koo na majina?
Tumalizie kwa kuwashauri wananchi wa Kalenga wachague ukombozi. Tunaamini historia fupi ya utawala wa kifalme fichi wa Kihindi utawasaidia kuona mwanga na kuuchagua wakikataa kuchagua giza na utawala fichi wa koo na majina makubwa ya makada wa vyama na wakubwa wa serikali ambayo kimsingi inawachukulia kama punda vihongwe wa kubeba koo husika.
Chanzo:Tanzania Daima Feb., 26, 2014.

No comments: