The Chant of Savant

Saturday 26 April 2014

Luku plus vi usitutishie nyau


Japo  wasomaji na wapenzi wa safu hii huwa wanauliza kama kweli navuta mibangi na kunywa migongo, huwa sijibu.
Hata hivyo, kazi zangu zinaweza kunitetea. Kama vipande vyangu huisaidia jamii kuondokana na watu hasa wala watu waitwao ‘human eaters aka watwawala’ kwa lugha ya kitaalamu, basi mibangi yangu ni mali au siyo?
Hivi karibuni kuna kihiyo mmoja anayetuhumiwa kughushi vyeti na sifa za kisomi hadi kujinadi kuwa ana ‘Masters’ wakati ni mwalimu wa zamani wa UPE aliyeibuliwa na siasa uchwara za kulindana na kufadhiliana.
Kihiyo huyu sitamtaja jina. Ila jina lake linafanana na Bill  mita ya LUKU ongeza VI alijifanya ni mpenzi na mzalendo wa kaya wakati si chochote si lolote bali mhalifu anayepaswa kupelekwa The Hague kwa kuchochea fujo.
 Bwana Luku plus vi si alikwenda kwenye ‘house of God’ na kufanya vitu ambavyo siyo saizi ya pale. ‘We can’t allow the house of God to go to dogs’. Eti alidai kuwa kama wachovu wataridhia kuwa na siri kali tatu basi wageshi watachukua kaya. Hivyo, walevi watatawaliwa kwa mtutu wa bunduki. ‘Shame on you Luku plus vi! How dare you to say that?’
 Hata hivyo, mshukuru Mungu kwa vile Njaa Kaya amekuwa akikukingia kifua kwa sababu ajuazo pamoja na kuambiwa kuwa ulighushi na ni kihiyo. Sijui kama kipindi hiki ataendelea kukudekeza wakati ukisema wazi kuwa anaweza kupinduliwa vinginevyo kuwe kuna tatizo ‘upstairs’.
Kwanza, licha ya kuwa aibu na kuvunja sheria, ni ukosefu wa heshima na hekima kwenda kwenye ‘house of God’ na kufanya siasa tena siasa zenyewe uchwara zenye kujaa mawazo mgando na utapiamlo vya hali ya juu. Pili, ni kukataa kukua na kukomaa kwa mtu kuwa na fikra za ki-Interahamwe, wale wahalifu waliotekeleza ‘genocide’ kule Ruanda.
Tatu, Luku plus vi alionyesha alivyo kihiyo kweli pale alipovuta mibangi yake ya kimadaraka na kulinganisha hali ya kisiasa kayani na ile ya Korea Kaskazini na Kusini. ‘How dare you compare a sheep to a hyena?’
Maskini kihiyo huyu hajui kuwa Korea iligawanywa tokana na siasa za kihasama za wakati wa vita baridi. Kwanini usijiandikishe Chuo Kikuu Huria lau ukapata msasa na kujua ‘basic things like these man?’
Najitolea kukufundisha bure lau uondokane na ukihiyo na aibu unavyozidi kuvionea sifa.
Kama wewe ni mwoga tokana na mazabe na madhambi mliyotutenda na wenzako kwenye genge lako, basi usitake kutujaza woga.
Yakupaswa uelewe. Mtu mzima hatishiwi nyau. Isitoshe, vijana wa sasa wa ‘ki-dot com’ si wa kutishia nyau wakati mmewanyonya hadi wakapigika. Wanajihangaisha kupata elimu ili wasiwe vihiyo kama wewe.
Lakini bado mnawanyima au kuwalangua mikopo ya elimu ya juu wakati wengi wenu mmesoma ubwete chini ya sera kombozi za mzee Mchonga. Ukome na kukomaa japo unaonyesha kukataa kukoma.
Nashangaa bangi wanazovuta madingi wetu ambao wanalindana hata kwenye upuuzi.
Laiti wengi wao wangekuwa wamesoma falsafa kama mimi, wangejua hatari ya kile wanachotengeneza huku wakiwatishia watu kwa mauaji ya kimbari yaliyoasisiwa na kutekelezwa na vihiyo kama wao.
Leo nitawapa faida kwa kuwapa nukuu moja kavu kavu ya gwiji Martin Luther Jr aliyesema, “We must learn to live together as brothers or we perish together like fools.” Tafsiri rahisi ni kwamba tujifunze kuishi pamoja kama ndugu au tukubali kufa pamoja kama wapumbavu. Hii nukuu noma siyo? Inachoma hadi ndani au vipi?
Hivyo bwana Luvu plus vi na wenzako mnaootea kuvuta mibangi na kuitumia kutudanganya, kutuibia, kututisha na kutuburuza mjue hili kuwa tuko kwenye mtumbwi mmoja. Mtu mmoja akitia tobo tutazama wote. Umenoa sana yakhe.
Luvu plus vi anadai eti kama Bunge la Ulaji la Katiba litapitisha uwepo wa siri kali tatu kaya haitatawalika. Uongo mtupu.
Kama imetawalika chini ya siri kali mbili tena zenye kila utata na ujambazi kila aina itashindwaje kutawalika kwa kuwa na siri kali tatu?
Basi mie nasema tena kwa herufi kubwa, TUWE NA SIRIKALI MOJA NA KAYA MOJA SIMPLE AND FINITO. 

Wanaoogopa siri kali tatu ni woga wa kawaida. Hata hivyo, siwezi kumlaumu kihiyo huyu kwa vile hana elimu ya kutosha kujua mambo mepesi.
Wapo mavuvuzela wenzake wengine wanaosema eti siri kali tatu zitatushinda kuzihudumia.
Urongo. Kama tumeweza kuhudumia wezi na majambazi na vihiyo kila aina tutashindwa nini kuhudumia siri kali tatu?
Isitoshe, hata kama sikubaliki na utitiri wa siri tena kali, kama walevi wataamua kuwa wanataka siri kali hata mia, tawile au vipi?
Kama tumeweza kuliwa na kutawaliwa na mabingwa wa kughushi na wengine wengi tutashindwa nini? Kama tumeweza kuwahudumia wauza bwimbwi, majambazi na mafisadi wengi tutashindwa nini? Kama tumeweza kuwahudumia wababaishaji na wazururaji aka Vasco da Gama na misafara yake ughaibuni kila mwaka bila kusahau wachukuaji muwaitao wawekezaji tutashindwa siri kali tatu?
Leo nina usongo na Luku plus vi na wenzake. Natamani nivute mibangi inibangue niende nimbangue mtu kwa manundu na ngeu kama si kumnyotoa roho.Mkome na mkomae huku mkishika adabu na adabu ikiwashika vinginevyo hakitaeleweka.
Salam maalum ni kwa wababaishaji wote wanaolala kitanda kimoja na wachunaji wajiitao wachungaji wakitumia roho mtakakitu wamuitaye roho mtakatifu kuacha kutuchezea kwa kuchanganya politiki na dini. ‘Shame on you!’

Chanzo: Nipashe 26, 2014.

No comments: