The Chant of Savant

Friday 9 May 2014

Civil disobedience njia pekee ya ukombozi Tanzania

          Hali ilivyo ni kwamba demokrasia nchini imeshindikana. Pamoja na kulazimika kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuridhia mfumo wa vyama vingi na kufanyika uchaguzi kwa zaidi ya miaka 20, Tanzania imeonyesha kuwa nyuma linapokuja suala la demokrasia ya kweli. Vyama vya upinzani vimekuwa vikihujumiwa karibu kila uchaguzi.  Mchezo huu mchafu ulianza mwaka 1995 pale Chama cha NCCR-Mageuzi kilipokuwa kwenye kilele cha umaarufu wake kabla ya kuhujumiwa na kusambaratishwa. Kinachoendelea ni sawa na kile alichowahi kusema Joseph Stalin imla wa zamani wa uliokuwa muungano wa Kisoviet aliyesema, "It's not the people who vote that count. It's the people who count the votes." yaani, wanaopiga kura hawaamui lolote ila wanaohesabu kura uamua kila kitu.
Hakuna ubishi. Uchaguzi wa mwaka 1995 ulichakachuliwa kiasi cha kuwaacha watanzania walio wengi wakishangaa matokeo ya uchaguzi husika yaliyompa ushindi wa “kishindo” mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa ambaye alikuwa hakubariki.
Mwaka 2005 hali ilijirudia ambapo zamu hii hujuma ilielekezwa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya NCCR-Mageuzi kuhujumiwa na kutoweka kwenye kilele cha uongozi. Kadhalika mwaka 2010 CCM kama kawaida yao walichakachua uchaguzi na kumpa ushindi Jakaya Kikwete kwa mara ya pili pamoja na kuboronga kwenye kipindi cha kwanza.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga uliofanyika hivi karibuni ni kielelezo halisi cha mchezo huu mchafu ambao ni kifo cha demokrasia. Katika uchaguzi huu mdogo madudu mengi yalifanyika ikiwemo kutumia daftari lililochakachuliwa na wapiga kura lililopingwa vikali na vyama vya upinzani hasa baada ya kugundua ongezeko la wapiga kura kwenye ngome za CCM huku kukiwapo upungufu wa wapiga kura kwenye ngome za upinzani.
Kimsingi, kinachoendelea ni kupoteza fedha ya umma kwenye zoezi ambalo limeonyesha kuwa kiini macho na hujuma ya hali ya juu kwa demokrasia. Uchaguzi hauna heshima tena. Umegeuka zoezi la kuchezea akili za watu na pesa yao. Inasikitisha kwa nchi maskini na ombaomba kutumia pesa kwenye zoezi la uongo kama hili.
Licha ya kuchakachuliwa kwa daftari la uchaguzi, matukio ya hivi karibuni ya kuwateka, kuwadhalilisha na kuwapiga viongozi wa upinzani ni ushahidi tosha. Yote hii ni hitimisho la amri iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM rais Kikwete kuwa chama chake kijibu mapigo na kuachana na uvumilivu. Na kweli, baada ya Kikwete kutoa amri hii ya kufanya fujo, tumeshuhudia amri yake ikitekelezwa huko Kalenga ambapo mwana wa mteule wa CCM alishinda uchaguzi katika mazingira ya kutia shaka.
Maana ya haya yote ni kwamba ustaarabu wa wapinzani unaonyesha wazi kushindwa. People power imefeli licha ya kusahaulika. Hivyo, wapinzani badala ya kushikiria kushiriki uchaguzi, waususie na kuhakikisha nchi haitawaliki. Watumie njia na haki ya kidemokrasia ambayo ni kuanzisha maandamano na migomo nchi nzima ili nchi isitawalike. Hili litailazimisha CCM kufuata kanuni za demokrasia.  Laiti kama upinzani ungezingatia ushauri wa mwenyekiti wa chama cha DP, Christopher Mtikila aliyeshauri usishiriki uchaguzi hadi tume huru ya uchaguzi inayohusisha vyama vyote iundwe. Unaweza kwenda mbali zaidi na kusema kuwa bila kuwa na Katiba mpya, Tume mpya ya Uchaguzi na Daftari mpya la wapiga kura lililoandaliwa chini ya usimamizi wa tume huru tutaendelea kushuhudia matusi kwa demokrasia.
People Power imefeli kutokana na tabia ya watanzania kusahau mambo kirahisi. Nani anaulizia mabilioni ya fedha yaliyofichwa Uswisi ambayo balozi wa Uswisi nchini Olivier Chave alisema hivi karibuni kuwa yanahamishiwa kwingine baada ya vyombo vya habari kuyashupalia? Nani anakumbushia uwajibishwaji wa wale walioshiriki ufisadi wa Richmond ambapo vinara wa wizi huu sasa wanapigana vikumbo eti kutaka wagombee urais. Ili wachaguliwe na nani na wafanye nini zaidi ya kuzidi kuiingiza nchi kwenye matatizo zaidi? Nani anapiga kelele kutaka kujua sababu za kupanda kwa deni la taifa ambalo hivi karibuni limeumka bila maelezo ya kina na yenye kuingia akilini?
Nani anapigia kelele uteuzi wa upendeleo wa makada wa CCM kusimamia uchaguzi ambapo tume ya sasa imefeli kama alivyosema jaji mstaafu Amir Manento Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora aliyekaririwa akisema, “Tume ya Uchaguzi haifanyi kazi kwa usawa, inavibagua baadhi ya vyama vya siasa, haiko huru, hii ni hatari katika ujenzi wa demokrasia hapa nchini.” Ajabu hata hiyo tume iliyoshutumiwa hakijihangaisha kujibu tuhuma hizi. Hii maana yake ni kwamba madai haya ni ukweli mtupu.
 
Imefikia mahali watu wanasema kuwa hata CCM wakisimamisha bata au mbuzi, kwa mfumo mbovu wa uchakachuaji na wizi wa kura wa sasa, atashinda tena kwa kishindo.
Hii maana yake ni kwamba ustaarabu umeshindwa. Hivyo, wapinzani wanapaswa kufanya kile ambacho kwa kiingereza huitwa Civil Disobedience yaani kuhakikisha nchi haitawaliki ili kutenda haki. Hii ni haki ya kikatiba ambayo imetumika sehemu mbali mbali na kuleta matunda tarajiwa.
Pia wapinzania licha ya kugomea chaguzi zitakazofuata, waende kuelimisha watu wa vijijini ambako CCM imekuwa ikijigamba kuwa kwa kiwango kikubwa cha ujinga kilichopo si rahisi kushindwa kwa vile wananchi hawajui haki zao. Wanaishi kwa kutishwa na watendaji wa CCM waliojazwa serikalini. Wapinzani wasidanganywe na umati wa watu wanaokwenda kwenye mikutano yao kushangaa helikopta ambayo wengi wa wakazi wa mashambani hawajawahi kuona wala hawawezi kuitofautisha na ndege ulaya.
Tumalizie kwa kuwashauri wapinzani kuacha ubinafsi na upogo wa kudhani kuwa wanaweza kushinda chini ya mfumo mbovu wa sasa.hata chama kipendwe vipi na kupigiwa kura, zitaitibwa na kitashindwa chini ya mfumo huu mchafu wa uchakachuaji na unyanyasaji wa wapinzani.  Pia wahakikishe jeshi la polisi linabanwa na kuacha kutumiwa kisiasa kama hali ilivyo kwa sasa.
Bila kufanya hivyo basi wategemee CCM kutawala milele na nchi kuendelea kuwa chini ya utawala wa chama kimoja kama ilivyofichua hivi karibuni gazeti la Uingereza la The Mail on Sunday wakati likimtuhumu Kikwete na CCM kushiriki ujangili ili kupata mtaji wa uchaguzi. Kwa ufupi ni kwamba demokrasia nchini imeshindwa hivyo, Civil Disobedience ndilo jibu mujarabu.
Chanzo: Dira

3 comments:

Unknown said...

Safi! Kwanza Tanzania hamna demokrasia bwana Mhango. Bora Kondoo na punda waende wakafanye maonyesho ya silaha pale uwanja wa uhuru. Sijui itakuwaje kondoo watano wanashuka kutoka mbinguni na miamvuli. hahahahah

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Karibu sana bwana Samwel,
Umeiacha hoi na analogue yako ya kondoo na walinda ufisadi wetu uchwara.Karibu tena na naamini ujumbe wako umefika.

Unknown said...

Bila shaka bwana mhango. Tuko pamoja sana, fear nothing but fear itself.