The Chant of Savant

Saturday 10 May 2014

Hii NHC au Nation Housing Corruption?

Hivi karibuni shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilitoa tangazo la kuuza nyumba 118 kwenye eneo la Hananasif, mtaa wa Wakulima, Kinondoni jijini Dar es salaam, kwa lengo la kutaka eti kutekeleza ujenzi wa nyumba 15,000 nchini.
Kwa juu mipango kama hii ni mizuri sana. Ni habari tamu kusikia. Ila kwa ndani licha ya kuwa balaa ni uoza mtupu. Kwa mfano, bei ya nyumba ni kubwa na masharti ya kuzinunua yanatia shaka na kuonyesha kutokuwepo umakini juu ya mazingira mazima ya upatikanaji wa pesa. Kama kuna umakini basi ni mojawapo ya namna ya kubariki jinai inayoendelea nchini ambako mtu anaweza kuiba au kufanya biashara haramu na kupata pesa na kuihalalisha kwa njia ya kuwekeza kwenye miradi michafu kama hii.
Kinachogomba pamoja na ukweli kuwa miradi ya namna hii inasaidia kusafisha pesa chafu ni je NHC inauza nyumba na kujenga nyumba kama sehemu ya huduma au biashara? Je nini malengo ya kuanzishwa shirika la Nyumba ambalo lilianzishwa na serikali kwa ajili ya kuwawezesha watanzania kupata pa kuishi ingawa kwa sasa linamilkiwa kibiashara huku nyumba zake zikiwanufaisha wenye nazo? Inakuwaje NHC wapate nyumba za kuuza wakati wafanyakazi wa taifa hilo hilo linaloimilki hawana nyumba zaidi ya kunyonywa na kuteswa kwenye nyumba za watu binafsi? Je kwanini wasikopeshwe wafanyakazi wa serikali wakalipa taratibu ili lau ziwe kiinua mgongo kwao?
Hata hivyo, serikali inayowalipa mshahara kiduchu hao wafanyakazi haitakubali kuwauzia hizo nyumba wakalipa kidogokidogo.  Tunaweza kusema ni roho mbaya na ubinafsi wa kawaida vinavyowasumbua wakubwa wetu. Mbona mawaziri waligawana nyumba za serikali zilizoko kwenye maeneo mazuri kibiashara na hawakuona hasara yoyote?
          Kama tutaangalia hali halisi ya taifa letu tukizingatia tulikotoka, bei ya nyumba husika si kwa ajili ya watanzania wa kawaida. Maana nyumba husika zinauzwa kuanzia shilingi 199,000,000 hadi 253,000,000 bila kodi ya ongezeko la thamani (Value Added Tax). Je ni watanzania wangapi wenye uwezo wa kuwa na pesa taslimu kama hizi zitokanazo na kazi halali kama ajira zao? Je huku si kuwabagua watanzania wenye kipato cha chini na kuruhusu wageni wajizolee nyumba za umma? Kariakoo tumeruhusu wahindi na wageni wengine wanunue nyumba zote na nje ya mji kadhalika. Je baadaye tutakapojikuta wakimbizi kwenye nchi yetu kwa tamaa ya watu wachache tuanze kupiga kelele? Maana haiingii akilini eti wanauza nyumba za umma kujenga nyumba za umma. Kwanini msikusanye kodi na mapato vizuri mkaongeza nyumba nyingine badala ya kulangua hizi? Ni hakikisho lipi linatolewa kuwa nyumba zitajengwa?
          Tokana na bei ya kuruka ya nyumba husika, ni rahisi kubashiri nani watakuwa wanunuzi. Bila shaka nyumba hizi zitanunuliwa kama njugu na wauza unga, maharamia, wageni wenye kutia shaka, mafisadi wakubwa serikalini na familia zao. Wahalifu mbali mbali kama vile majambazi, matapeli na wote walioweza kuchuma utajiri kwa njia za kijinai wanaomba Mungu iwepo miradi mingi ya kijambazi kama hii ili waweze kusafisha pesa yao chafu itokanayo na jinai mbali mbali kama zilivyotajwa hapo juu.
          Kuna haja ya kuwaambia wahusika kuwa wanachofanya ni kutaka kuwatumia wananchi kama mihuri ya kuhalalisha uchafu na haramu hii. Si mseme tu kuwa mmeamua kuiba nyumba za umma kutumia kuuza baada ya kustukiwa mlipogawana zile za mwanzo?
          Hizi haziwezi kuwa nyumba za shirika la nyumba la taifa maskini kama letu
Kwa mfumo huu wa kijambazi ni kwamba tunatoa motisha kwa jinai ziwezeshazo watu kupata utajiri na pesa ya haraka kwa hasara ya taifa letu. Hii ni baada ya wenye nafasi kuitumia kuliibia taifa huku wakitoa mwanya kwa wenye kuweza kutenda jinai na kupata pesa kushiriki maisha haya. Watu hawalipi kodi wala hawelezi walivyopata pesa lakini wanaruhusiwa kununua vitega uchumi.
Viongozi hawataji mali zao wanaendelea kuiba na kujilimbikiza.
          Haitashangaza kusikia au kushuhudia kuwa nyumba husika zimenunuliwa na wale wale tunaowajua kuwa ni wezi wakubwa wa mali za umma, wauza unga, na kila aina ya wahalifu wanaosifika kwa kuitumia Tanzania  kutokana na kuonekana kuwa kama shamba la bibi.
          Kuonyesha huu mchezo ulivyo mchafu na hasara kwa taifa, wahusika baada ya kununua nyumba hizi kwa pesa chafu, watatumia nyumba hizi kujipatia mikopo toka kwenye taasisi mbali mbali za kifedha hata za serikali na hata ikibidi wengine kuishia na mikopo hiyo huku wakiicha serikali ikishikilia nyumba zao ambazo zitageuka tena kuwa zake. Upuuzi huu utaendelea kwenye kile ambacho unaweza kuita revolving door miaka nenda rudi huku uchumi wa nchi yetu ukiendelea kudidimia tokana na mfumo jambazi kama huu.
          Nchi zilizoendelea zimeweka mfumo wa mortgage wa kulipa kidogo kidogo kulingana na kipato cha mtu ili kuwawezesha wananchi kuchapa kazi na kuwekeza kwenye mali. Pili wamefanya hivvyo ili kuzuia wizi wa mali za umma. Tatu wamefanya hivyo kuzuia usafishaji wa fedha chafu zinazoweza kuingizwa kwenye nchi husika japo si nyingi ikilinganishwa na nchi fisadi za kiafrika.
          Tumalizie kwa kuiasa serikali iache mchezo mchafu wa kutumia mali za umma kuuibia ukiachia mbali kuhalalisha pesa chafu na kudumaza uchumi. Pia biashara ya namna hii isiyofuata haki wala mazingira halisi, inazidi kuwaondoa wananchi wa kawaida kwenye maisha na kuwatupa nje ya miji kiasi cha makazi yasiyo rasmi kuongezeka huku wahalifu na wageni wakizidi kuongezeka kwenye miji yetu. Sijui ni maharamia wangapi toka Somalia au wauza unga wangapi toka Pakistani, India na kwingineko wamejazana kwenye miji yetu simply because wana uwezo wa kutumia pesa yao chafu kununua au kujenga majumba Tanzania? Je hii ni National Housing Corporation au National Housing Corruption?
Chanzo: Dira Mei 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Ndiyo sababu jira kuu ya vijana ni kubeba unga(Sembe) ili waamishe tatizo kama hizo akili ndogo zinaongoza akili kubwa, wanapoamisha matatizo kwa watu wengine wanapokuwa madarakani wanapokaribia kutoka mashaka yanakuwa makubwa kujaribu kutafuta wezi wenzao waingie madarakani

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon nakubaliana nawe kuwa akili kubwa inapotawala ndogo lazima kuwe na tatizo tena si tatizo tu kwa upande mmoja bali pande zote. Kwanini akili kubwa ikubali kutawaliwa na akili ndogo na kwanini akili ndogo ifanikiwe kuitawala akili kubwa? Naona wameanza kurithishana karibu kila kitu kuanzia ubunge. Si ajabu hata urais tukaletewa watoto wa wakubwa kama vile Hussein Mwinyi hata Ali Karume kama si Amani.
Mungu atuzindue tuondoe mazandiki na vibaka hawa.