The Chant of Savant

Wednesday 21 May 2014

Kijiwe: CAG akague hata bwibwi


Baada ya kunyaka taarifa kuwa wezi wa ndani ya sirikali hasa ndata waliweza kuiba pembe za ndovu kwenye vituo vya polisi au kuzibadilisha na kuchukua kubwa na kuweka ndogo kama ilivyofichuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Fedheha za serikali (CAG), kijiwe kinataka afanye ukaguzi wa bwibwi lililokwisha kamatwa.
Kama kawa, bada ya kusoma gazeti la leo, Kijiwe kinajikita kwenye habari kilichoteua kujadili.
Hakuna cha mjdala wala nini. Anayewahi ndiye anakula mic. Msomi Mkatatamaa leo kaamua kuwa kinara. Anakatua mic, “Leo nimesoma habari ya ndata kuiba pembe za ndovu waliozokamata na au kuchukua kubwa na kuweka ndogo. Pia nimeona jinsi tiketi za ndege zilivyolanguliwa mara 160 kwa tiketi.Nashauri mkuu azuiwe kwenda kutanua ughaibuni. Heri angeenda kutanua tu kuliko kutulangua hata tiketi za pipa kama ilivyofichuliwa hivi karibuni.”
Mpemba anakunywa kahawa yake na kuchomekea, “Huu wizi wa kilafu na kitoto so to speak. Kuna mijitu imeumbika na tamaa kuliko hata panya na fisi.”
Mijjinga anakwanyua mic,”Hakika tumegeuka taifa la vibaka na mibaka kirahisi. Waziri anauza wanyama, ndata anaiba vizibo na mwanakaya wa kawaida anaingia porini kuua wanyama na kuharibu urathi wa kaya yetu. Kweli mbomoa kaya ni mwana kaya! Jaji anamwachia muuza bwibwi huku mkaguzi wa uwanja wa ndege akila naye na miteja inaongezeka na mkuu anapata wa kutumia kujionyesha kama mtu mwema wakati ni muhimili wa balaa hili!”
“Yakhe usinikumbushe majaji waliogeuka majunk. Wanikumbusha yule aliyetoa hukumu katikati ya usiku kuachia wauza unga umma usijue mshirika katika kuuza bwibwi wallahi. Wakumbuka jinsi Nyarandu alivomleta yule ntasha kumhonga akaishia kulipuliwa? Wakumbuka vita dhidi ya wauaji mazeruzeru? Imefia wapi baada ya kukuta wahusika wengi wazito?” Anakandia Mpemba.
Mgosi Machungi anakatua mic, “Tisiwache Naigeia wala Kenya. Kuna uwezekano tiishawapita miaka mingi iiiyopita. Inafikia hata tiketi ya mkuu ya kwenda ughaibuni inalanguliwa na hakuna anayewajibishwa? Je rahisi hajui au ni ile hali ya kuajiii watu wake? Kinachokea ni wachovu kuendelea kuwa mashahidi wa maangamizi yao.”
Kanji leo anaamua kuwahi mjadala kabla haujanoga ili asiachwe nyuma, “Hii si baya kama vatu nafanya biashara. Ila hii ya kuiba pembe dovu baya sana. Kama data iba exhibit basi kaya kwenda jehanam sikini.”
Mipawa anaingilia huku akimtazama Kanji kwa jicho kali, “Hapa nashindwa kuelewa mhalifu ni nani kati ya aliyekamatwa na pembe za ndovu au bwimbwi na anayeviiba tena toka kwenye vituo vya polisi au anayewatetea.”
Mgosi hangoji mwingine apoke mic, “Tikisema hii siikai ni ya wasanii na wezi mwasema twatukana. Sasa hii nini? Nijuavyo hakuna atakayejitokeza kukanusha wala kutoa maelezo. Ukisikia EpA ndogo ndogo ndiyo hizi wajameni.”
Sofia Lion aka Kanungaembe aliyekuwa akimwangalia Mipawa kwa chuki anakatua mic, “Jamani hakuna haja ya kupitisha hukumu bila ushahidi. Kama kuna mtu ana ushahidi wa yanayomkera aupeleke polisi.”
Mipawa anakwanyua mic kujibu mapigo, “Sofi usiwe kama walaji wa katiba wa chama chako ambao wanaongea kwa matumbo kukariri upupu na upuuzi wa viongozi wao badala ya kujenga hoja.”
Sofia akiwa anajiandaa kujibu mapigo Mpemba anamchomekea, “Sofia kweli untisha sana. Ndata hao hao watuhumiwa halafu wapelekewe ushahidi wa kuwafunga! Wacheza nini?”
“Umeinyaka kuwa balozi zetu ughaibuni zinaongoza kwa matanuzi?” Mbwa Mwitu anadakia
“Zitashindwa nini wakati zinasimamiwa na marafiki na watoto wa wa kubwa? Hii Bongolalaland alijisemea mzee Mpayukaji.”  Anajibu Mchunguliaji. Aniangalia huku mie nikitabasamu kwa kumwagiwa ujiko japo ni ukweli unaouma kuhusiana na ujambazi tunaofanyiwa mchana kweupe.
“Heri ingekuwa Bongolalaland na siyo Bungubungualand ambapo kila mtu anashindana kuhomola alipo kana kwamba kaya ni genge la wezi.” Anachomekea Kapende ambaye anakatua kashata na kuendelea, “Sisi tuna balozi nje au bazazi tu? Mijitu imekalia wizi roho mbaya na fitina. Niliwahi kukwama kwenye nchi moja ughaibuni ambayo sitaitaja. Nilipokwenda kwenye ubalozi wetu waliniuliza maswali ya ndata ndata utadhani nilikuwa central. Hovyo kabisa. Kumbe mijizi mitupu.”
“Itafikia mahali mtu akikuita Mdanganyika unarusha ngumi. Maana kwa maana nyingine anakuita bwege.” Anafoka Mijjinga.
Sofi anachomekea, “Kahamie huko unakoona kuzuri utuachia kaya  yetu. Kwanza nyie wapinzani mnatujazia mbu. “This is too much. Kwanini mnadhalilisha kaya yetu hivi nasi tukiona kana kwamba mna kwingine pa kuita nyumbani?”
Mijjinga anadakia, “Kaya inajidhalilisha yenyewe Sofi usitake mapenzi na ushabiki vya kibubusa. Sasa kama wakubwa wamegeuka mibaka na wadogo vibaka huku hakuna anayejaribu hata kulaani tuiteje?”
“Umesikia na JeiWii walivyofuja mabilioni? Nasikia walikufuru kwenye matumizi ya kijambazi.” Kapende anachomekea.
Mgosi Machungi anakula mic, “Watashindwa nini iwapo nao wamegeuka wanasiasa tena mafisadi? Huoni tinavyotishiwa kuwa watachukua kaya nao wanakaa kimya? Nadhani wamo kwenye ndoa moja ya haamu ya kulindana na kutisha wachovu ili waibiwe zaidi na zaidi. Who cares?”
Wanakijiwe wanakata jicho la haraka haraka kwa jinsi Mgosi anavyomwaga ung’eng’e.
          “You are dead right Mgosi. I fully concur with you kuwa kaya yetu sasa ni ya mibaka kuanzia juu hadi chini. Hata wachovu ni vibaka isipokuwa baadhi yetu tunaoshupalia upuuzi na ujambazi huu.”
Sofia anataka kuingilia kati Msomi anamkatiza, “Sofi tulia sijakufikisha. Nataka nikupe dozi hadi utosheke hata ukienda nyumbani unikumbuke.”
Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu anaingilia “Eti umpe nini akifika wapi akukumbuke?”
“Mbwa acha uswahili na tafsiri za kimipasho kama bunge la katiba. Naaminisha kumridhisha.”
“Eti kufanya nini?” Mbwa Mwitu anazidi kuzoza.
Msomi anajibu, “Kumtusholeza pamoja na wengine kama yeye. Tuache utani, kaya isipokuwa makini tutaangamia. Ndiyo maana napendekeza CAG akague mibwimbwi inayodaiwa kukamatwa ili tujue wakamataji wameishajiibia kiasi gani. Maana huu mchezo ni mauti ya kaya japo mkuu na wenzake wanakenua kwa vile wanaushiriki.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita mtumishi mmoja wa kukagua mizigo uwanja wa ndege. Acha tumwagie kahawa hadi akimbie akilia kama kichanga!
Chanzo: Tanzania Daima Mei 21, 2014.
 

No comments: