The Chant of Savant

Friday 11 July 2014

Mlevi kuanzisha kampuni za kitapeli

Baada ya kugundua kuwa ukwepaji kodi na wizi wa fedha za umma, mlevi amepanga kupiga njuluku kwa kugeuka mjasiriamali.
Napanga kuanzisha kampuni ya kupiga njuluku ya Mlevi Organized Network Enterprises Yo-yo (MONEY).
Maana, bwana Benny Tunituni Nkapa alituachia wosia kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake. Kwa wajanja kama mimi, mtaji wa Mlevi ni bongo lake.
Sina haja ya kutumia nguvu wakati nina akili inayochemka tena kwenye kaya ya vibaka na majangili na majambawazi ambapo kila mtu anapiga njuluku kulingana na mishemishe zake na hakuna anayehoji au kuuliza kapataje. Ukiwa na akili inayochemka kwenye kaya ya Bongolala, lazima uwe tajiri tu.
Wakubwa wanapiga njuluku kwenye uchukuaji na wadogo kwenye usanii.
Ngoma droo kama Nigeria na Ujerumani kule Brazil au vipi?
Nitaanzisha kampuni yangu itashughulikia yafuatayo:
Kutoa mizigo bandarini kwa bei kiduchu kulinganisha na ile ambayo ungetoa TRA.
Kupitisha bidhaa zilizozuilika kama vile kusafirisha pembe za ndovu kwenda Mashariki ya mbali.
Hapa tutashughulikia bidhaa kama pembe za faru, mbao za miti iliyo kwenye hatari ya kutoweka toka Madagascar na kwingineko, bangi, unga, dhahabu, shaba, urani na madude mengine ya bei mbaya.
Tunaandaa vibali feki kupitishia mizigo toka Uchina mfano khanga za wax kwa kudai zinasafirishwa kwenda DRC, Burundi, Malawi, Rwanda na Zambia wakati tunafaulisha na kuuza Kariakoo.
Lazima mlevi aitwe bilionea mwaka huu hasa kutokana na kaya kuruhusu wajanja kutajirika bila kutoa jasho. Kwanini kuwa maskini kwenye kaya ambako hakuna ulazima wa kutaja wala kueleza mlevi alivyopata njuluku zake? Ukiuza bwimbwi sawa. Ukifanya ujambazi sawa. Ukighushi vyeti vya kitaaluma na kupata kazi nono sawa tu mradi akili kichwani, au vipi? Ukianzisha TRA yako sawa.
Ni kama sera ya ruksa imerejea upya.
Naona kila kitu ni kama zama za mzee Ruksa ambapo misingi ya huu uhuru wa kupiga njuluku ilipowekwa na walevi wakaamua kuachana na kujibana kijamaa na kutengeneza njuluku na kutumia kibepari.
Abarikiwe aliyeanzisha mchezo huu ambao unatuwezesha wajanja kupiga njuluku kama hatuna akili nzuri.
Kuna kipindi nilipanga kuanzisha banda la ‘pilau’ yaani kuonyesha picha za ngono hata kwa watoto nikahofia bi mkubwa asingekubaliana na mradi huu hasa ikizingatiwa kuwa unaharibu watoto.
Badala yake napanga kuanzisha kampuni ya kurekodi kanda na CD ili niwaibie wasanii. Kwanini wengine, tena toka mbali waje hapa na kuanzisha biashara hii na kuwa mabilionea wakati nami naweza kujiunga kwenye mchezo huu na kupiga njuluku.
Nitaanzisha kampuni yangu nitakayoiita Mlevi Music Centre na ofisi zangu zitakuwa mitaa ya Msimbazi, Congo, Mahiwa hata Mponda.
Hapa lazima nitoe ushindani kwa waanzilishi wa biashara hii kuhakikisha hawavuni wasipopanda peke yao wakati nami nina bongo linalochemka.
Baada ya kuhakikisha kuwa biashara yangu ya kutoa mizigo bandarini na ya kuiba kazi za wasanii lazima nitafute nyumba maeneo ya ‘downtown’ Kariakoo au Posta kwenye nyumba za Msajili wa Majumba ili nilipe kodi kiduchu na maisha yaende kama maji mtoni.
Kwa vile nataka kuwa bilionea ndani ya muda mfupi, napanga kuanzisha kampuni nyingine yaani ya ujenzi wa barabara ya Mlevi Road Construction and Destruction (MRCD).
Kwa kutumia kampuni hii lazima nipate tenda za kujenga barabara za chini ya viwango ili kupiga njuluku.
Juzi nimegundua mbinu nyingine ya kupiga njuluku za umma ‘sorry’ za walevi wadanganyika.
Unasaini mkataba wa kujenga ‘road’ unaiminya kitu kama nusu mita au mita na njuluku inaingia.
Ukishapiga njuluku unaanzisha kampuni ya kutengeneza majeneza tayari kuwazika wahanga wa kazi ya mikono yako na unakuwa bilionea, au vipi.
Pia nitaanzisha kampuni ya kuagiza dawa nje ya kaya ili kuingiza dawa feki na kutengeneza njuluku haraka haraka.
Pia nina mpango wa kuanzisha dhehebu la dini au kikundi cha kutoa mihadhara ili kupiga njuluku zitokanazo na sadaka au michango.
Kwanini wachovu fulani waanzishe ulaji huu kwa jina la God nami niishie kuwa mtazamaji wakati najua siri zote za mchezo huu?
Hapa bado sijapanga kuanzisha kampuni ya kutafutia watu hasa akina mama huko Malaysia na Uarabuni ili wakachangamke kama si kuchangamshwa.
Najua watu wanavyopenda kwenda majuu wataingia laini na kuishia kuwa makahaba huko huku wakiteseka wasijue jinsi ya kurejea makwao.
Pia nina mpango wa kubadili jina langu na kujipachika jina la kigogo ili niweze kugombea urais baada ya kubadili cheti changu cha kuzaliwa ili nionekane kijana.
Bila kuwa na jina kubwa siku hizi urais hupati.
Kwa vile ninahitaji kuwa bilionea haraka, lazima niuze bwimbwi ili kutunisha fuko langu la kibilionea.
Kwa vile wauza bwimbwi kayani hawakamatwi, bila shaka nitaukata kabla umma kustuka na kuanza kushughulikia jinai hii.
Bila shaka nikipiga njuluku ya kutosha, lazima niwasiliane na profwesa Sospita Muongo nimkatie chake anipe uwekezaji, ‘sorry’ uchukuaji ‘sorry’ ulaji kwenye gesi inayogunduliwa kila uchao katika kaya ombaomba yenye kuwa na uchumi lakini ikaukalia. 
CHANZO: NIPASHE Julai 12, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Mwanachama kutoka kijiweni kwetu, nakukumbusha mwekazaji(mchukuaji) umesahau wapi ni sehemu nzuri kimkakati kufungua ofisi. Bila shaka pale ikulu itakuwa rahisi kufanya mawasiliano na waziri husika na baraka zingine kutoka mhe.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon, shukrani kwa nasaha zako na kunitia shime. Inshallah tutasonga mbele na kuukamata ule mjumba mweupe tayari kuzichanga njuluku.