The Chant of Savant

Saturday 2 August 2014

Mlevi aanzisha gazeti la mauza uza ‘The Fiction’

Kikwete, jamaa apendaye umaarufu  (cheap popularity) kiasi cha kutapeliwa mara mbili na matapeli wa Kinigeria
Iruh (tapeli aliyempa  kikwete tuzo feki)  aktioa tuzo hiyo kwa mtu ambaye hakutambuliwa wao humuita mugu yaani jinga au zuzu

Membe akipokea tuzo feki ya kwanza kutolewa na matapeli wa kinigeria kwa niaba ya Kikwete
Japo huu unaweza kuonekana kama utani au bangi na gongo vya mlevi, kuna ukweli na faida kubwa sana kwenye haya nitakayoandika. Walengwa wangu wakuu ni wamilki wa vyombo vya umbea ambao ima kutokana na misimamo yao au kushikilia maadili hadi kupambana na madili na ufisadi wanajikuta wakinyimwa kazi hasa matangazo.
Ujumbe huu ni kwa wale wanoonewa kiasi cha kutaka kufutwa kwenye ramani ya dunia ya habari kwa kuhujumiwa vombo vyao. Ni ujumbe mahususi kwa wale waliokataa uumbwa na upaka kwa wenye maulaji.
Baada ya kugundua kuwa kutumiana kunalipa japo wengine wanakosea kudhani huku ni kutapeliana, napanga kuanzisha gazeti la The Mauzauza akaThe Fiction ambalo wasomaji wake wengi ni wanakijiwe.
Lengo kuu la kuanzisha gazeti hili si kuuza wala kutoa habari kama vilivyo vyombo vingine vya habari. Nia yangu ni kuchanga njuluku haraka hasa baada ya kupata matangazo toka kwa wenye kaya. Nitakachofanya, kwanza ni kumwalika mkuu na kumpa tuzo ya kuwa kiongozi bora duniani kama yalivyofanya majarida ya The Blagh Blagh of the World and The East Miscast Gunk hivi karibuni.
Najua dili hii itajibu na kunipa njuluku hasa kuelekea kwenye uchakachuaji ambapo wasaka tonge la urahisi watanijaza mifweza ili niwaandike vizuri hata  kama nitakachokuwa naandika ni urongo mtupu. Mara hii nani kasahau mazabe ya 2005 ambapo fisi waliitwa kondoo na shetani malaika?
Wakati wasiojua kinachoendelea nyuma ya pazia wanaona dili kuwa kama kutumiana, tunaonufaika tunaliona kama ukombozi na uwezo wetu wa kutumia bongo zetu kuchanga njuluku.
Wahenga walinena: Baniani mbaya kiatu chake dawa ati.Nani anajali maadili wakati wakubwa walishayageuza madili? Nani anajali taaluma wakati wanataaluma waliishazitelekeza wakavamia siasa za ulaji kwa miguu na mikono tena bila kunawa?
Kwa vile uongozi ni kuwa na sifa hata kama ni za kipuuzi, we koma, najua idea hii itakubalika haraka haraka.  No small fame when it comes to fame. Fame is fame even in infamous hall. Ikishakubalika lazima kuzipiga njuluku kama sina akili nzuri.
Kama yule Porofwesa wa kughushi na kuiba maandiko ya wenzie aliweza kutunga kitabu cha kipwagu na kipwaguzi kumvika kilemba cha ukoko mkubwa akaondoka na uchache kwanini nasi tusipige njuluku? Mie lazima nichange njuluku angalau baadaye nitumie usanii wangu kuingia mjengoni kama mheshimiwa aliyekuwa muishiwa lakini achanganya na za kwake akaibuka na uheshimiwa hata kama sitachangia mjengoni zaidi ya kuuchapa usingizi na kungoja posho ya mipasho.
Lazima kuwahi kabla jamaa hajaachia ngazi au mchezo huu kuzoeleka kiasi cha kila tapeli kuutumia. Ili kumnasa viliyo kama anavyowanasa walevi, lazima kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa huku niking’ata na kupuliza ili asistuke buzi likakata kamba.
Shurti kumpongeza kwa kupambana na ufisadi kiasi cha Kaya kuwa mfano wa kuingwa kwenye vita dhidi ya ufisadi ambapo mafisadi hawauawi wala kushitakiwa zaidi ya kuonywa wakapunguza kuiba. Jamaa lazima tumpongeze kama yule msanii maarufu aliyechukua fagio la chuma kufagia ufisadi ambao alihakikisha anaufagia na kuuweka chini busati ili aukanyage uumie. Nani mara hii kasahau mavituz kama Liloyondo?
Pia namkumba Tunituni wa Uwazi na Ukweli ambaye alihakikisha uwazi hauwi wazi wala ukweli kuwa kweli mpaka aamue.
Kama umemsahau huyu jamaa mjivuni aliyewahi kuwaambia wamilki wa vyombo vya habari kuwa kama wao si mafisadi waeleze walivyopata mitaji ya kuviashisha akimaanisha kwake kila mtu ni fisadi na bila ufisadi hakuna anayeweza kutoboa.
Kweli jamaa aliujua ufisadi kiasi cha kuigeuza familia yake yote kuwa ya vitimbakwiri na mafisadi wa kunuka kuanzia mama hadi watoto. Ukiuliza yuko wapi? Unaambiwa, kwa ufisadi wake yuko nyuma ya pazia akivuta kamba kuhakikisha katiba mpya haitoki akanyea debe.
Ukisikia kutumiwa na kutumiana ndiyo huku.
Jamaa kapanga aondoke na sifa za kuleta katiba halafu jamaa kwa madhambi yao yanamchimba mkwara anaishia kuondoka kwa aibu ya kujipiga mtama akionekana kigeugeu.
Dingi lazima apongezwe kukuza uchumi kiasi cha kaya kuwa na uwezo wa kupoteza dolari bilioni mbili kwa mwaka bila uchumi wala siasa kuyumba huku tukiondoka na sifa moja ya kuwa na mafisadi wengi walioficha njuluku Uswizi ya Uswazi.Uchumi usingekuwa umekuwa kiasi cha kujitosheleza pengo la dolari bilioni mbili lingesababisha kaya isitawalike.
Hakika, nitampa nishani ya kupambana na mihadarati ambapo waliojifanya wajanja alipiga simu wakanaswa na tani kibao kule Sauzi baada ya kuwaacha wapite kwenye viwanja vyetu ili waingie mkenge wajue wameshinda wasijue watanyakwa kule Sauzi.
Pia nitampa nishani ya kupambana na ujangili. Nani mara hii hatambui mchango wa operesheni Tokomeza iliyotokomezwa baada ya kugusa pabaya? Hata wale wanyama waliotoroshewa Umangani watakujarejeshwa. Ngojeni.
Siku hizi kupongeza wakubwa imekuwa fasheni ya kuchanga njuluku.
Ndiyo njia rahisi na mujarabu ya kula nao na kupata tenda, matangazo, trip nje wakuu wanapokwenda kutanua na maulaji mengine. Kwa hali ilivyo, kama gazeti lako litawakandia wakubwa ujue litasuasua.
Watakunyima matangazo na kuwashawishi wenzao kukufungulia kesi zisizo na kichwa wala miguu ilmradi ujirudi uwapongeze na kurejea kundini.
Bahati yetu, mkuu huwa hafanyi mambo kama haya. Hivyo tunapanga kumpongeza si kwa kujikomba bali kumpa haki yake.  Mfano, amefanikiwa kulinda muungano kwa kukataa sirikali tatu katika kaya moja.
By the way, hawa magabacholi waliodhalilisha miili ya ndugu zetu na kuitupa ndani ya mto  Mpigi  walitaka  igeuke maji watu wanywe, umeinyaka vipi na kufanya nini?
CHANZO: NIPASHE Augost 2, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Natapika rais wetu kugeuzwa toy lakuchezea
Usalama wa taifa mko wapi
Aibu aibu aibu
Wasaidizi wa rais Nani anawapitisha
Ikulu iluku imegeuka kwa fundi

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon usemayo ni kweli tupu. Inakera ajuaye ni Mungu pekee. Rais anageuzwa mumu na bado wapambe na waramba viatu wake wanamsifia wakati wanamsifia upuuzi!