The Chant of Savant

Friday 8 August 2014

Mlevi ajitolea kubomoa ghorofa 'uaji' la Uhindini


Hakuna  jambo lililoharibu uhusiano na dada yangu mshirika wangu porofwesa Anna Kajuamlo Tiba-ijuka kama mghorofa wa uhindini. Nilimbana aubomoe akasema eti sheria zinabana. 
 Acheni mambo ya kitoto kwani hamjui jinsi ya kubadili hata kupinda hizo sheria? Mbona mnapokuwa mnatafuta uchache wenu mnazipinda kirahisi na kupata mnachokitaka bila kuogopa wala kulalama? 
 Nilishauri my sister Nshomile porofwesa waziri apeleke mswaada bungeni kuzifutilia mbali au kuzirekebisha zile sheria chafu ili kuokoa uhai wa walevi. Nilifikia hata hatua ya kumshuku kuwa … 
Sasa baada ya mstahiki asiyestahiki meya wa Ailala muishi Jerryfish Slaa kuja na kituko kuwa mghorofa ule hauwezi kubomolewa kwa vile zinahitaji njuluku zipatazo madafu milioni mia sita yaani milioni 600/-   nimeamua kujitolea lau kuonyesha si njia bali hata uongozi hata kama ninalewa na kuvuta mibangi kama sina akili nzuri. Sijui kama hata huo mghorofa fweki umefikia thamani hii.  
Nina sababu za kutoa usaidizi huu tena bure.
Mosi,  nitatengeneza njuluku kibao kwa kuuza nondo mawe na matofali hasa usawa huu ambapo vyuma chakavu ni big deal mitaani. Nani asiyetaka ulaji kama huu?  
Hapa bila shaka nitakuwa nimeokoa njuluku ambazo wezi fulani wanataka kuiba kwa kisingizio cha kuangusha mjengo huu ambao ulishaanguka bali kilichobaki ni kumalizia tu. Ni kama kusukuma mlevi au aliyechuchumaa. 
  Pili, kwa kuangusha huu mjengo uaji nitaokoa maisha ya walevi wengi kiasi cha kuepusha maafa ambayo kaya ingeyapata baadaye. Nani amesahau kuwa mjengo dada ulianguka na kuua walevi zaidi ya 30 huku ukijeruhi mamia?  
Ni yupi huyu anapenda kuona walevi wakirejesha namba kabla ya wakati tena kwa kuuza roho zao kwa mafisadi wa kigeni ambao wengi wao wanaishi kayani hata kinyume cha sheria? 
Tatu, sitaki njuluku bali kuokoa maisha ya walevi wangu na kuonyesha mfano kuwa kumbe mambo mengine ni rahisi ili wakwasi na mafisadi wetu wanaotumia utumbo badala ya ubongo wanayafanya kuwa magumu ili wapige njuluku za dezo na chafu haraka. 
 Nne, kuonyesha kuwa kuna ngurumbili wanataka kupokea rushwa bila kujali kuwa uhai wa walevi nao ni muhimu sawa na wao. Haiwezekani watu wenye kujaliwa kuwa na utu wakubali kushindwa kuangusha mjengo huu hatarishi. Lazima wawe wamepokea chochote kit utu. 
Tano, kuonyesha njia kuwa hata nasi tunaweza kujitegemea maana si kila kitu hata kuchimba vyoo au kuangusha mjumba kama huu tuhitaji wafadhili. Mbona tunapononihino kwenye vyoo hatuhitaji wafadhili? Kwanini kazi yetu iwe sawa na y a bata yaani kuchafua wengine waje wasafishe? Je sisi ni hamnaza kiasi hiki? Kwanini baadhi yetu wanaendekeza ubata? 
Sita, kuonyesha kuwa kuendekeza utegemezi rushwa na njaa ndicho chanzo cha viungo vya miili ya ndugu zetu kutupwa kama mbwa au kondom kwenye jalala huku waliotenda jinai hii wakiendelea kudekezwa. Ingekuwa waswazi wametupa mabaki ya magabacholi huku Gujarat si ungewaka moto?  Hata katika kaya jirani ya nyayo huwezi kutenda jinai kama hii ukapona. 
  Saba, kuonyesha kuwa kubomoa ni rahisi kuliko kujenga. Hawa wanaosema eti mjengo unahitaji milioni 600/- ni waongo na wezi wa kawaida wanaotaka kuwageuza walevi majuha wasijue zinachaji kuliko wao hasa wakishaweka mibangi yao. 
 Nane, nataka kuonyesha moyo wa kujenga kaya kwa vitendo wakati wao wakilibomoa kwa uroho na roho mbaya zao. Pia ningeomba wahusika waniletee wale wote waliojenga au kuidhinisha jengo hili kujengwa niwanyonge hadharani ili liwe somo kwa tumbili wengine wanaodhani kaya yetu ni No Man’s Land au shamba la chizi. 
 Hatuwezi wote kuwa majuha na waroho na wasaka tonge hata kama tu walevi bwana. Haiwezekani nakataa. Lazima tutokee watu kama sisi wenye mawazo mapana na vichwa vinavyochaji tuonyeshe njia wengine wafuate. 
Laiti ingekuwa amri yangu, huyu aliyedanganya kuwa kudondosha ule mjengo kunahitaju milioni 600/- ningempiga kalamu aende akamwambie sheteni huo  uongo kwa vile ndiye aliyemhadaa na kumlea vibaya. 
Tisa, huyu meya amenikumbusha kituko cha hivi karibuni ambapo imegundulika kuwa makondrati wa barabara zetu uchwara wamefikia hata kupunguza upana kuanzia nusu mita hadi mita nzima ili kupiga njuluku na wahusika wasisituke wala kutoa maelezo.  
Ama kweli hii kaya si walevi tena bali ya vichaa na majuha! Inawezekanaje vyombo vya umbea kufichua ujambazi huu na lisirikali likakaa kimya kama halihusiki? Ajabu ya maajabu wakati uchafu huu wote ukiendelea, kuna matapeli wa Kinigeria wanaotoa tuzo kwa mugu yaani majuha wanayotapeli kwa uongozi bora. Uongozi au uongo bora?  
Kumi licha ya kutoa somo, nataka kutoa onyo kuwa sasa walevi wameamka na hawatalala tena. Yeyote anayepokea rushwa na kuidhinisha kujengwa mijengo miuaji lazima tumnyotoe roho kabla hajanyotoa zetu. Sitashangaa kusikia kuwa hata lile daraja la Kigambwoni nalo limejengwa chini ya kiwango. Hivyo, lazima mlevi niombe kibali kulichunguza kuona kama liko gado lisijeua walevi wangu bure kama ajali za barabara zilizofinywa zinayonyonga walevi wasio na hatia.  
Hatuwezi kuwa wapuuzi na walafi na wasaka tonge sote. Lazima sisi wenye udhu na taadhima tuongoze njia bila kujali kama wahusika wanapenda au kuchukia. Mnaigeuza kaya yetu kaya ya majuha kana kwamba sote tu majuha na mafisi na mafisadi kama nyinyi!  
Mshindwe na kunyong’onyea.  Kila siku mnataka mtajirike nyinyi tu. Ajira mnapaeana kuanzia BoT had Uhamiaji. Urais na Ubunge nyinyi na watoto wenu.  Scholarship pia na makando kando mengine. Nanyi mnapaswa kuporomosha bure kama ghorofa angamizi la Uhindini.
CHANZO: NIPASHE Agosti 9, 2014. 

No comments: