The Chant of Savant

Saturday 20 September 2014

Mlevi alipochonga na mzee Mchonga

Baada ya dunia kugeuka gunia nilijikuta nikifufua kipaji changu cha kuota na kuona maono huku nikitoa maonyo kwa umma ili usiangamie ima kwa kujua, kutaka, kulazimika au kutojua kabisa. Naona yule anacheka asijue huu ni unabii na si bangi na gongo kama wengi wanavyonichukulia. Hivyo, msishangae siku moja moja nikitongoa na kuwamegea yale niliyoona ambayo walevi wa kawaida hawawezi kuona. Kwa vile walevi wananiaminia, huwa nikiona mambo na kuwambia huwa hawanipuuzii ili wasije jilaumu au kuumia. Nikishaweka kanywaji na bangi vitu hushuka utadhani mie nabii. Hata hivyo ni nabii kwa walevi wa Danganyika.  Hivyo, wewe unayesoma haya uyazingatie kwa usalama wako. Mie natabiri ukweli wala si kama wale wachunaji wanaojiita wachungaji waliojipa na kujivisha vyeo vikubwa vya kiroho wakati lao ni uroho. Wanawahadaa watu kuwa wanatenda miujiza na wana roho mtakatifu wakati wamejaa roho mtakakitu na tamaa ya utajiri wa kuwaibia makapuku.Hayo tuyaache kwanza.
Najua wengi watadhani hizi ni kamba au bangi vinavyonisumbua kuwataarifu kuwa usiku wa jana niliopata maono yenye faida kwa walevi na kaya yao. Nazidi kuwaonya. Atakayepuuzia haya asinilaumu siku ya siku yatakapomkuta ya kumkuta.
Amini nawaambieni. Jana nilikutana na mtu mmoja maarufu na muhimu. Je wajua ni nani? Huna haja ya kuumiza kichwa kujibu. Habari njema ni kwamba nilikutana na mzee Mchonga tukachonga ile mbaya.  Habari mbaya ni kwamba mzee Mchonga aliondoka akiwa amesononeka na kuudhika ile mbaya baada ya kumaliza kumpa taarifa ya mambo ambayo si mambo yaliyoendelea tangu alipoondoka duniani.  Baada ya kumeza kanywaji aina ya Justice alinipa kama saa na ushei hivi kumchapia yote yaliyojiri kwenye kaya yake.Wenye kuamini aminini kwa faida yenu na wasioamini msiamini kwa maangamizi yenu. Kazi yangu ni kumwaga unabii hata kama ni wa kilevi.
Basi, baada ya kumkaribisha kiti na kumpa chupa ya kanywaji kaitwako Justice, nilimchapia yote yaliyojiri baada ya yeye kuondoka. Nilimpasha kuanzia mtu wake aliyembeba hadi watu wakasema amebeba kinyago cha mpapure na jisi jamaa alivyoboa hasa baada ya kugeuza ikuuu mahali pa wanyang’anyi kupangia misheni zao. Nilimchapia kuwa baada ya paka kuondoka, panya walijitawala na kujitwalia kila kitu kuanzia Benki ya NbC hadi machimbo ya makaa yam awe kule Kiwila.
Habari hii ilimchanganya na kumuudhi mzee Mchonga kiasi cha kusema, “I didn’t know my hunk’d go to the dogs. Had I known, I’d not have wasted my time and my people.” Alisema kwa kimombo chake safi.
Baada ya kumpa nafasi amalize hasira na kutoa nasaha zake, nilimpa mchapo wa katiba mpya isiyo mpya bali viraka, uchakachuaji sanaa na kujilisha pepo. Yote tisa. Kumi ni pale aliposikia funga kazi kuwa mkuu ameridhia Bunge Maalum la Kushiba lisitishwe huku likiendelea kutafuna madafu bilioni 200. Kwanza hakuamini hadi nilipomhakikishia kuwa ninachosema si hadithi za kilevi wala bangi.
Mchonga alisema, “ Wana akili hawa au vichaa? Where do people living on shoestring get such money to offer to thugs in the first place? I don’t get it really.” Nilishindwa kumjibu ikabidi nicheke kwa uchungu kabla ya kububujikwa machozi. Baada ya kunionea huruma kwa nilivyokuwa nikilia na kuugulia, mzee Mchonga alisema, “Mwanangu nimekuelewa. Huna haja ya kuendelea kulia. Kwani siku yao ikifika watalia wao nawe utacheka. Sikujua kuwa kumbe niliopoondoka na akili na hekima vilitoweka. How come you don’t have sane people who can zero in?”
Alishika kifimbo chake na kukichezesha kama anapanga kuwaramba watu bakora na kusema, “Kumbe mema yote niliyoacha yameharibiwa hivi!”
Alichukua kifimbo chake akaamuka kwenye kiti ili aende kuwatia adabu. Nilimfuata na kumsihi asifikirie hivyo kwa vile wale wezi wanalindwa kwa mitutu ya hatari na hawatamsikiliza. Alikubaliana nami tukaendelea kuchonga.
Alinyamaza huku akinikazia macho kusikia utetezi wangu. Ndipo nilipomjibu kuwa si kwamba watu wenye akili na mapenzi na kaya hawapo. Nilimwambia kuwa tupo lakini hatusikilizwi. Nani angetusikiliza wakati ulaji unapozidi hugeuka ulevi na wendawazimu wakati walaji wakiamini kuwa kutenda jinai ya kula na kuuza wenzao ni haki waliyopewa na Mungu?
Hakuna kitu kilimwacha hoi mzee Mchonga kama kummegea kuwa baada ya mtu wake ku-mess na kukitoa waliingia wale aliowakataa wakafanya kila unyani kwa kuuza na kuhujumu kila kitu. Kama ada, ilimchukua muda kuamini kuwa hata makapi yanaweza kuwa na thamani kiasi cha kupwakiwa na watu wenye akili. Alihoji akili zetu huku akitikisa kichwa kwa masikitiko. Aliponiuliza ilikuwaje makapi yakapeta, nilimchorea kuwa yalikwapua njuluku benki na kuwahonga waandishi nyemelezi aliowakataa Yesu wakawapamba na kupambika kiasi cha walevi kuingia mkenge wakajuta baadaye.
Baada ya kukuna kichwa chake alisema, “Ushauri wako mzuri mwanangu. Ni kweli. Baada ya nyani kuteka shamba mwenye shamba anapoteza nguvu. Nimekuelewa.”
Kabla sijasema lolote mzee Mchonga aliuliza, “Una maana yale maadili tuliyoweka yameondolewa?” nilijibu ndiyo na kumwambia kuwa maadili yaliondolewa na nafasi yake ilichukuliwa na madili. Nilimwambia kuwa hata lile azimio la Arusha aliloacha likibanjuliwa mapanga lilishazikwa na la Zenj la Uhujumaa na Kujimegea. Hakukubali kirahisi. Aliuliza tena, “Una maana Ben aliwasaliti walevi wangu? Nilijibu ndiyo akatikisa kichwa kwa hasira.
Tokana na muda kutuacha. Mzee Mchonga aliulizia habari za Mary wake na watoto. Nilimpa kuwa Mary alikuwa mzima na msafi kama alivyomuacha. Kwani hakuwahi kuanzisha NGO yoyote ya wizi wala kuusaka ulaji kwenye chama kama wengine. Habari hii ilimfurahisha kiasi cha kuniaga na kutokomea akitikisa kichwa asiamini aliyosikia. Leo nawapa hi washikaji zangu wa Msimbazi Roundabout na Shule ya Uhuru Mchanganyiko hasa wa kwenye kijiwe cha kahawa.
CHANZO: NIPASHE 

No comments: