The Chant of Savant

Thursday 23 October 2014

Katiba feki imepita au imepitishwa?


          Vyombo vya habari viliripoti tukio la kupitishwa rasimu iliyochakachuliwa ya katiba mpya. Vilionyesha Chama Cha Mapinduzi, na vyama nyemelezi washirika wakie wakishangilia kufanikiwa kupora na hatimaye kupitisha katiba yao wanayoiita ya wananchi. Walishangilia hujuma na si huduma. Si jambo la kushangila kwa vile ni maafa kwa taifa na wao wakiwamo tokana na upogo na ulafi wao. Kwa upande mmoja ilikuwa furaha. Kwa upande wa pili wa Umoja wa Katiba ya Wananchi, (UKAWA) na wananchi wapenda mabadiliko, haki na uwajibikaji ilikuwa ni kilio.
          Pamoja na CCM kufanikisha hujuma hii kwa umma na vizazi vijavyo, kuna masomo mawili matatu tuliyopata kama jamii ya kitanzania.
          Kwanza, CCM imethibitisha wazi kuwa iko madarakani si kwa ridhaa na maslahi ya wananchi bali ya kikundi kidogo cha walaji kilichopania kuendelea kula hata kama ni kwa kuvunja sheria. Hili linapaswa kuwa onyo na kumbusho kwa umma wa watanzania kutafuta jibu ya jinsi ya kupata serikali na katiba vinavyowafaa. Maana hii rasimu iliyopita na serikali iliyopo haviwafai tena. Vingewafaa visingedharau mawazo na maoni yao. Visingewapuuzia na kuchakachua katiba yao waliyodhamiria kuandika.
          Pili, tumejifunza kuwa CCM na washirika zake hawana nia nzuri na taifa hili. Maana kwa walivyopoteza muda na fedha za umma ni ushahidi mwingine kuwa mambo si sawa. Hivyo, watanzania, kwa mara nyingine, wanapaswa kufikiri sawa sawa namna ya kujikomboa na kuondokana na ufisadi na uhujumu vilivyotamalaki kiasi cha kujipatia uhalali japo kwa njia haramu ya uchakachuaji wa rasimu na matumizi mabaya ya fedha za umma.
          Tatu, CCM wameonyesha wazi kuwa hawana huruma na wala hawaujali wala kuuheshimu umma uliowaweka madarakani. Wangeujali na kuuheshimu umma, wasingefanya madudu waliyofanya.
          Nne, tumejifunza kuwa watanzania bado wana safari ndefu ya kufikia ukombozi kamili hasa kutokana na tabia yao ya kuacha suala la katiba ambayo ni mkataba baina ya watawala na watawaliwa kupokwa na watu wachache wanaolinda madhambi na maslahi yao. Haiwezekani rasimu ichakachuliwe kwa kuondoa mambo ya msingi kama vile kupunguza mamlaka yanayotumiwa vibaya ya rais nao wakawa mashahidi kusiwe na tatizo tena kubwa. Haiwezekani mambo mazuri kama vile kupambana na ufisadi yaondolewa na watanzania wasifanye kitu kusiwe na tatizo kitaifa na kijamii. Je tatizo ni woga, ujinga au kutojua haki na wajibu wao kama jamii. Maana inashangaza kuona kikundi kidogo cha watu tena wenye kutia kila shaka kikajifanyia mambo kama kitakavyo kana kwamba taifa limeishiwa watu wanaofikiri sawa sawa.
          Tano, tumejifunza kuwa wengi wa wanasiasa wetu wamo madarakani kutumikia matumbo yao na si wananchi kama wanavyodai. Hivi, kwa mfano mbunge aliyeonyesha wazi kupinga rasimu iliyochakachuliwa akapiga kura kuiunga mkono kama hakuna namna ya hongo au kutetea maslahi binafsi. Kwa wanaomkumbuka mbunge huyu kidhabi, alinusurika kupigwa na wajumbe toka Visiwani baada ya kudai kuwa wanalalamikalalamika hovyo. Ajabu, ili kumaliza hasira zake binafsi na hao waliotaka kumtia adabu, ameramba matapishi yake kwa kuwa wa kwanza kuiunga mkono rasimu aliyoipinga. Imam mbunge huyu aliunga mkono baada ya kuahidiwa kitu au kulipiza kisasi kama siyo kwa kipindi kile alichopinga kutafuta gea ya kulipwa posho ya kila siku ya laki tatu.  Pia yupo mbunge wa Chama Cha Wananchi (CUF) aliyeenguliwa chamani na kusimikwa na mahakama aliyejitapa kuwa ndiye aliwezesha kupata kura mbili zilizopitisha jinai hii ikiwa ni njia ya kuikomoa CUF asijue suala la katiba si la chama wala mtu binafsi bali taifa na vizazi vijavyo. Huyu hakupaswa kuwa mbunge. Heri angeuza nyanya kuwa mganga wa kienyeji kama si mchezesha kamari.
          Sita, tumejifunza kuwa baadhi ya watu wetu bado wana tamaa na ubinafsi wa kutisha hasa ikizingatiwa kuwa wengi waliendelea ana Bunge Maalumu la Katiba (BMK) hata baada ya kuishiwa uhalali kisheria ili walipwe posho ya kila siku. Walitanguliza matumbo yao na kuuweka nyuma umma uliowaamini kufanya kazi hii adhimu iliyodhulumiwa.
          Saba, tumejifunza kuwa ufisadi Tanzania hautaisha hasa kama hujuma hii itapita. Na bila shaka, kama imevuka kizingiti cha kwanza, itapita kwa njia zile zile chafu na haramu, uchakachuaji hata wa kura ya kuipitisha.
          Hivi karibuni mwenyekiti wa Kamati bandia ya uandishi wa katiba bandia, Andrew Chenge alikaririwa akisema, “Bunge hili limeboresha Rasimu ya Katiba vizuri sana. Rasimu hii imebeba asilimia 75 ya maudhui ya Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba (Joseph) na nyie wajumbe mmeboresha kwa asilimia 25 tu.” Limboresha au limeboesha (bore)? Ajabu Chenge hakutaja ubovu wa hiyo aslimia 25 ukiachia mbali walipopata mamlaka ya kufanya hivyo na kwa misingi na sababu gani zaidi ya kulinda mafisadi wanaoogopa kuburuzwa mahakamani kama ingepita kama ilivyopendekezwa na wananchi.  Huwezi kuondoa vipengele, mfano, vinavyotaka viongozi kupeleka serikalini zawadi wanazopewa ukasema umeboresha. Huwezi kuondoa kipengele cha kuwawajibisha viongozi wanapofanya madudu hasa wabunge ukasema umeboresha. Kama kuboresha ni huku basi hakuna maana zaidi ya kukingia kifua ukale na ufisadi vilivyotamalaki ambapo uongozi umegeuka biashara ya kutengeneza fedha chafu na haramu kwa haraka kwa kuwaibia umma. Nadhani kwa sasa wezi wa EPA na Escrow wanachekelea. Wameshindaa. Wale waharifu wote waliofanya ufisadi madarakani waliostaafu sasa wanaashangilia. Mafisadi wanaopanga kuendelea na business as usual ya kuuibia umma lazima waangushe party.
Je katiba imepita au imepitishwa tena kwa mbinu, njia na nia chafu za kuendelea kuwashika mateka watanzania? Je huu ni mwisho au mwanzo wa mwisho wa kuiangusha katiba hii isiyojali wananchi?
Chanzo : Dira ya Mtanzania 

No comments: