The Chant of Savant

Friday 17 October 2014

Mlevi afaidi filamu ya RugeSingasinga

Pamoja na kupiga bangi na kanywaji, wiki jana nilifaidi filamu iitwayo IpTL yaani Interdependent pilfers in Tanzia Limited (IpTL). Katika filamu hii yenye wahusika wengi japo wanaojulikana ni wawili, inaonyesha ukatili, uroho, roho mbaya hata upofu wa aina yake na vitu vingine vya ajabu ambapo majuha na matapeli tena wenye elimu za kutia shaka wanawatumia wasomi wanaojiona kukubuhu kumbe mabunga.
Filamu hii ilinikumbusha filamu nyingine niliyomaliza kuitaza wiki chache zilizopita iitwayo UdA yaani United and dangerous Animals ambao nao kama IpTL wamewatumia watu unaoweza kudhani wamepiga vitabu kumbe hovyo kuibia walevi kwenye nchi ya kufikirika ya Mizengwe inayopatikana kwenye kitabu cha Saa Ya Ukombozi kilichotungwa na mlevi. Hata hivyo, napanga kuwashitaki watunzi wa filamu hizi mbili kwa kunukuu kitabu changu bila kuomba na kupewa ruhusa. Hayo tuyaache.
Turejee kwenye filamu ya IpTL. Ukiwachunguza wahusika wakuu tagundua kitu kimoja ambacho ni kuzidiana akili na kila mmoja kujifanya mwema na mjanja. Katika unyama na ujambazi huu, vyombo vya habari viliripoti kuwepo kwa barua za msanii mmoja aliyekuwa akijifanya kuionya serikali ya Mizengwe si kwa kuipenda nchi yake bali kutaka kutumia nguvu na kupata chumo la wizi pamoja na kumkomoa mwenzake ambaye aligundua kuwa kumbe alipiga dili la dola kama milioni mia tatu bila kumhusisha yeye wakati yeye ndiye aliyesuka mpango mzima akishirikana na watawala majambazi wa Mizengwe.
Matapeli ni watu wa ajabu. Katika filamu hii mmoja wa wahusika wakuu aitwaye Jimmy Rugeruge Malira toka kaya ya Nshomile anajionyesha kama mzalendo kwa nchi yake wakati ukweli nyuma ya pazia ni jambazi katili ambalo laweza kumuuza hata mama yake ilmradi lipate njuluku. Hivyo anachofanya Jimmy Ruge Malira si upendo wala uzalendo bali unafiki. Unadhani aliandika aliyoandika kwa kuipenda Mizengwe? La. Ni kwa sababu mwizi mmoja amemzidi akili mwenzake.
Ruge Malira anashirikiana na ponjoro Harbinger SeSinga toka kaya ya Gabacholi kuibia kaya ya Mizengwe wakishirikiana na wakubwa zake vipofu na waroho. Ni filamu nzuri yenye kufikirisha na kuonya wale wote wanaojikuta kwenye mazingira kama haya. Pia inafundisha kuwatahadhari matapeli wa nyumbani na wa kigeni.  Minyoo hawa nyemelezi kwenye migogo ya wakubwa ni hatari kuliko hata Ebola, ukoma na Ukimwi.
Mtunzi wa filamu hii amejitahidi kuonyesha wasifu wa wahusika kwenye filamu yake. Wote wanatia shaka kuanzia maisha yao elimu zao hata huo ukwasi wao utokanao na wizi na utapeli. Wawili hawa ni viumbe wa hatari sana katika jamii yoyote. Kwani wana sura nzuri na wako tayari kutumiwa na wakubwa wezi wa Mizengwe kuficha uchafu wao kwa kugawiwa kidogo.
Kitu kingine kinachowakutanisha licha ya hulka na tabia zao za utapeli, uroho na wizi ni ukweli kuwa wote ni wasanii au tuseme matapeli wa kimataifa wanaojirahisi kwa wakubwa wenye uchu kuwatumia kuwaibia walio wengi. Pia wana tabia nyingine ya kujifanya wana huruma na wale wanaowaibia. Hawakosi kuchangia upuuzi mbali mbali kwa kutoa vijifedha kiduchu hapa na pale ili waonekana wanaisadia jamii wakati ni mibaka makubwa yanayopaswa kuchomwa moto kama vibaka.
Sifa nyingine ni kwamba wote wana bahati Mizengwe bado haijaanza utaratibu wa kuchoma moto mijibaka. Huwa mara nyingi walevi wanapenda kuwachoma moto vibaka huku wakiwaabudia mijibaka wanaobaka kaya yao.
Ukichunguza mchezo ulivyoanza utalia kama siyo kutamani kujinyotoa roho. Je unaweza kuamini, hata kama ni katika kaya ya kufikirika, kuwa jizi linaweza kwenda kwenye banki kuu na kuchomoa mabilioni ya madafu bila kuwekwa lupango? Hata hivyo, nani aliweke lupango wakati wanaopaswa kufanya hivyo ndiyo waajili wa jizi na jambazi hili? Basi katika kaya ya Mizengwe ujambazi huu wa kwenye filamu ya RugeSingasinga ni kitu cha kawaida. Katika kaya ile inasemekana hata mkuu wao aliwahi kufanya kitendo kama hicho kwa kuiibia banki kuu ili kupata fedha ya kununulia kura ya kula. Na huwezi kuamini hata kama ni katika kaya ya kufikirika. Alifanikiwa na akawa anawaambia walevi wa Mizengwe kuwa angewapatia maisha poa wakati alishapiga njuluku zao. Jamaa huwa hana aibu hata kama ni rais wa kufikirika.
Filamu hiii japo inachusha na kuudhi, ina fundisho moja kuu, siyo kila king’aracho ni dhahabu. Kuna waja tena wakubwa tu kwa nyadhifa ambao ukiwaona unaweza kuwaamini na kuwathamini. Lakini nyuma ya pazia ni wachafu kuliko hata nguruwe. Ni waroho kama fisi. Ni vipofu kama watoto wa mbwa. Wana uchu kuliko hata fisi na wana mawazo mafupi kama nguruwe. Je utawajuaje? Utawajua kwa matendo yao fichi ambayo filamu nyingi huyafichua.
Kuna viumbe wanafanya mambo utadhani wataishi milele. Hata wahusika wakuu kwenye filamu hii ukiwatazama si wazima. Watakuwaje wazima wakati wanaua mamilioni ya walevi wa Mizengwe? Watakuwaje wazima wakati kila siku roho na nafsi zao zinawasuta zikitukuta na udhambi? Wanaweza kujionyesha kama viumbe wenye furaha mbele ya pazia. Nyuma ya pazia unaweza kukuta mijitu inayojutia inayoishi kwa vidonge vya usingizi ulevi na laana nyingine nyingi. Lako ni kuomba Mungu awaongezee mapigo wasifaidi kanywaji na bangi kama sisi walevi tunavyovifaidi.
Unaweza kuamini kuwa hata hili igizo la kuingiza walevi mkenge kupitia kwenye katiba ni bure? Walioko nyuma yake waweza kuonekana watu mbele ya hadhira. Nyuma ya pazia ni madudu ya kutisha mithili ya majini ya kwenye hekaya za mfalme Suleiman. Ni viumbe wachafu na wa hovyo kuliko hata kinyesi. Je utawajuaje? Tafakari kila filamu unayoletewa na wasanii wanaozitumia kutengeza ulaji wao. Onyo, usipende kutazama filamu za udaku wala kusoma magazeti yake.
Chanzo: Nipashe Oktoba 18, 2014.

No comments: