The Chant of Savant

Tuesday 28 October 2014

Kikwete urais si kazi ngumu


WAKATI mwingine baadhi ya wanasiasa huongea vitu visivyoingia akilini kana kwamba wanaowasikiliza hawana akili za kutosha au wenye kufikiri sawasawa. Hivi karibuni, akiwa nchini China, Rais Jakaya Kikwete alitoa mpya pale alipokaririwa akisema, “Pili, kazi hii ya urais ni ngumu sana. Kwa hakika nawaonea gere sana wenye nguvu na ubavu wa kutaka kubakia kwenye kazi hii kwa miaka mingi. Pengine wana nguvu zaidi kuliko mimi.”
Hii si kweli. Kwanza, tupinge, kurekebisha na kusahishia kauli ya Rais Kikwete. Urais si kazi bali cheo cha kisiasa ambacho kinaweza kukaliwa na yoyote awe na elimu, ujuzi au hata asiwe navyo.
Ndiyo maana wahuni na majambazi kama Joseph Mobutu, Idd Amin, Sani Abacha na wengine waliweza kuupata na kuutumia tena kwa muda mrefu na wengine kuung’ang’ania hadi wakaondolewa ama kwa mapinduzi au mitutu ya bunduki.
 Je, Kikwete aliongea kwa mafumbo akimaanisha kinyume cha ugumu? Marais kama Yoweri Museveni, Robert Mugabe, Theodoro Obiang, Denis Sassou-Ngwesso au Blaise Compaore wangemsikia wangemcheka na kuthibitisha kuwa anayosema hayana ukweli bali kutaka kujipa sifa tu.  
Tangu kupata uhuru, urais umekuwa ni ufalme uliojificha kwenye koti la demokrasia. Hata Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere, pamoja na usafi wake, alithibitisha hili pale alipoanzisha utawala wa chama kimoja huku akigombea na kivuli ili asiuachie huu ulaji wenye kila aina ya raha na ulinzi kisheria.
Hata hivyo, si mara ya kwanza kusikia uongo huu toka kwenye kinywa cha Rais wa Tanzania kwani hata Benjamin Mkapa alipoulizwa alipomaliza kipindi cha kwanza alisema hivyo. Ajabu aliwazuia wengine chamani kwake kumpinga ili aendelee na “kazi hii ngumu.”
Urais, hasa kwenye nchi zilizokataa na kuzika uwajibikaji na maadili ya utumishi wa umma, ni ufalme na fursa ya mwenye kuwa nao kujitajirisha yeye na watu wake wa karibu.
Ni nafasi ya kutengeneza utajiri, japo uwe haramu, wa haraka sana. Urais hasa wa Tanzania anaoongelea Kikwete ni rahisi hasa baada ya kubariki ufisadi na umangimeza. Tumpe mfano mdogo Kikwete. Urais ungekuwa mgumu na wenye changamoto za kiuwajibikaji angeweza kweli kuficha hata majina ya watu anaoandamana nao kwenye ziara zake za mara kwa mara ughaibuni?
Kweli Kikwete angeweza kuwa bingwa wa kuizunguka dunia kwa kuunguza fedha za umma ambao umepiga kelele kumtaka aache tabia hii ya ufujaji wa fedha za umma hadi ukachoka naye akaendelea kutumia mamlaka yake kusafiri nje?
Hapa nani anataka kumdanganya kiasi cha kumgeuza hamnazo akubali kuwa urais ni kazi ngumu wakati ni ulaji wa dezo hata bila kufanya kazi yoyote?
Hata kama tukikubali kuwa urais ni kazi ngumu kama Kikwete anavyotaka kutuaminsha, kuna maswali ambayo yakiulizwa ukweli unakuwa tofauti.  Kama kweli mbona kila mmoja anautaka? Ilikuwaje hata baadhi ya marais wakafikia hata kuiba fedha benki kuu kuupata.
Nani mara hii amesahau mchafuano ambapo vyombo vya habari vilitumika kuwachafua baadhi ya wagombea mwaka 2005? Nani amesahau baadhi ya waandishi wa habari nguli waliogeuzwa nepi za wagombea waliowachafua wenzao wakaupata urais na kuwalipa nyemelezi hawa fadhila hata kwa kuwateua kuwa wasemaji wao na wengine wakuu wa wilaya? Akina Salva Rweyemamu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ofisi ya Rais Ikulu na Mihingo Rweyemamu wanaweza kuthibitisha hili.
Kama tutakuwa wakweli, urais si kazi ngumu hasa kwenye nchi ambapo rais yuko juu ya sheria akijifanyia atakavyo kama mfalme wa tawala za kiarabu. Urais utakuwaje mgumu wakati rais hawajibishwi kiasi cha kutumia nafasi hii na watu wake kula watakavyo? Ungekuwa mgumu kama kubeba zege nchi ingejiendea bila rais.
Hebu tujaribu kuthibitisha kuwa urais ni kazi rahisi ambayo kila mwenye kutaka kuukata haraka anautaka kwa udi na uvumba hata kwa kuvunja sheria au kuhujumu nchi yake.
Mosi, ukiwa Rais, mkeo watoto, wako hata waramba viatu wao wanakuwa marais kwa namna yao. Wanatumia nafasi yao nao kutengeneza utajiri wa haraka kwa njia mbali mbali.
Pili, unasafiri nje na kuizunguka dunia utakavyo kila unapotaka na hakuna anayekuuliza wala hulipii matanuzi yako.
Tatu, unapewa shahada hata bila kuingia darasani wakati watu wanasotea miaka hadi wengine kughushi wasipate.
Nne, unalindwa utadhani utaibiwa wakati hakuna mtu mwenye hamu hata ya kukuiba.
 Tano, mkeo na mashoga zake wanaanzisha kampuni ziitwazo NGO na kukata kutajirika haraka na wanapata wafadhili kirahisi kutokana na cheo chako cha rais.
Sita, mwanao, marafiki zake hata watoto wa marafiki na marafiki zako, wanatumia nafasi yako kugombea vyeo mbalimbali vya kisaisa kama vile ubunge na vinginevyo na wanavipata kutokana na kuwa watu wako. Waulize akina Ridhiwan, Dk Hussein Mwinyi, January Makamba, Stephen Masele na wengine watakupa ukweli.
Tumalizie kwa kuongeza msisitizo kuwa urais wa Tanzania si kazi bali cheo wala si ngumu kama anavyotaka kutuaminisha Kikwete. Matendo yake na waliomtangulia yanaonyesha hili bila kupingwa.
Hivyo, tusihadaike na maneno ya wanasiasa kuamini kuwa urais ni kazi na ni kazi ngumu. Hakuna, Kikwete aliponiacha hoi kama kusema eti angetamani akachunge mbuzi na ng’ombe na kulima mananasi. Ngoja amalize. Utamuona jijini sawa na watangulizi wake. Wakati huo muulize ahadi yake imeishia wapi. Hutopata jibu!
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 28, 2014.

No comments: