The Chant of Savant

Thursday 4 December 2014

Escrow-IPTL: CCM wanamhadaa nani?

Si kupiga chuku. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimo kwenye hali mbaya tokana na kukumbwa na kashfa ya wizi wa mabilioni ya umma toka kwenye mfuko wa escrow. Kinachoshangaza ni ile hali ya CCM kutaka kujiweka mbali na kashfa hii wakati walioitenda licha ya kuwa makada wake wa vyeo vya juu, serikali yake ndiyo mtuhumiwa mkuu.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM Abdurahman Kinana na Mkurugenzi wa Itikadi na Uenezi Nape Nauye walisikika wakisema kuwa hakuna kulindana mwongo huu. Je ya kweli haya? Maswali mengi yanaulizwa. Ilikuwaje CCM hii hii inayotaka kujitenga na mchezo iliouasisi na kuuzoea iwapo iliingia madarakani kwa mchezo ule ule? Rejea wizi wa fedha za umma kwenye kashfa ya EPA ambayo CCM haijawahi kuongelea achilia mbali kushindwa kukanusha.
Kinana alikaririwa akisema, “Muda wa kulindana haupo tena ndani ya CCM. Uvumilivu umefika mwisho. Muda wa kubebana na kuvumuliana sasa umekwisha.” Kinana hapa anakiri na kuthibitisha kuwa kumekuwapo na mchezo wa kulindana.  Huu nao ni ushahidi tosha kuwa makada wa CCM wamehusika kuiba fedha ya umma. Kwa mantiki hayo, chama kilichafuka zamani. Hivyo, anachofanya Kinana na CCM ni kumwaga machozi ya mamba tu. Ni wale wale. Wameshikwa pabaya sasa wanaanza kukanana. Tusiwape nafasi wakati huu kuendelea kutuchezea mahepe. Wawajibishwe kuanzia mwenyekiti wao hadi serikali yake ambayo iliingiza kampuni ya IPTL na kuiruhusu iendelee kuliibia taifa kwa zaidi ya miaka kumi. Rejea taarifa kuwa Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Horace Kolimba ndiye alikuwa kinara wa mazungumzo ya kuiingiza IPTL.
Kuonyesha kuwa CCM ndiyo wahusika wakuu wa kashfa hii, hata mwenyekiti wao amejitahidi kukwepa kushughulikia wala kuongelea kashfa hii. Ametumia mbinu ile ile aliyotumia kwenye kashfa za EPA na Richmond ili apate fursa ya kutoa kafara baadhi ya makada na mchezo uendelee.
Nape alikaririwa akisema, “Chama chetu kiko imara na kinafuata kanuni na taratibu zake za kuwawajibisha wale wanaokosea ndani ya chama, skendo zote za rushwa mnazoziskia huko tunashughulika nazo, hata hili sakata linaloendelea huko bungeni la Escrow, msimamo wa chama ni kuwawaliohusika waondoke waache chama kikiwa salama.”
Nape aliongeza, “Katika hili naomba niseme kila ambaye atabainika kuhusika achukuliwe hatua, kila mtu abebe msalaba wake mwenyewe. Hatutakubali kuona watu waliohusika katika sakata hilo wanaachwa, lazima wachukuliwe hatua.” Kumbe wanajua CCM si salama? Ajabu bado wanaonyesha kutokubali kuwa wapo wanaohusika na kashfa hii!  Huu ni ushahidi tosha kuwa wanahusika moja kwa moja na kashfa hii. Kama hawahusiki kupitia serikali yao, walikuwa wapi muda wote huu kama siyo kutaka kuimaliza kashfa tajwa kinamna kama walivyozoea? Hapa wa kutaka ajiuzulu ni rais na serikali yake. Maana wameshindwa kulinda raslimali na fedha za umma. Uzuri kashfa hii si ya kwanza. Zipo nyingi kuanzia SUKITA, Richmond, EPA, Meremeta, pesa ya uagizaji mafuta, usafirishaji na uuzwaji wa wanyama hai, kutorosha na kuficha fedha nje, misamaha ya kodi, matumizi mabaya ya fedha za umma, wizi kwenye serikali za mitaa na mwingine mwingi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba alikaririwa akisema, “Tunamtaka Waziri Mkuu awajibike kwa kitendo cha kupotosha umma, alichokifanya, kama asipojiuzulu inabidi afukuzwe kazi mara moja, amekuwa akitafuta visingizio vya kuzuia mjadala wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ndani ya Bunge.”   Hatumtetei Waziri Mkuu. Je Waziri Mkuu awajibishwe kwa lipi iwapo anamwakilisha rais na serikali nzima? Inabidi wapinzani wajifunze tokana na makosa yaliyofanyika wakati wa kashfa ya Richmond ambapo Waziri Mkuu alibebeshwa zigo la kashfa kuepusha kuangusha serikali yote. Ajabu sasa inaonekana hawajifunzi. Wanataka kurudia makosa yale yale.
Huku ni kutapatapa na kutaka kuwatwisha watu binafsi wakati kashfa nzima inaihusu serikali ya CCM. Ni ajabu hata wapinzani wamehanikiza kusema eti Waziri Mkuu ajiuzulu wakati wanaopaswa kujiuzulu ni serikali yote!
Kada mwingine wa CCM anayepigiwa upata kutaka kugombea urais Profesa Mark Mwandosya alikaririwa akisema, “Kwa sasa hivi vikao vya chama na serikali vinaendelea, ni lazima ripoti iwasilishwe bungeni, mambo yawe hadharani ili mbivu na mbichi zijulikane.” Huu ni ushahidi mwingine unaoihusisha CCM na wizi huu. Kwanini vikao serikalini na chamani kama hawahusiki? Mbona vyama vingine havifanyi hivyo zaidi ya kuwaachia wabunge wake washughulikie kashfa husika kupitia bungeni kama hakuna namna?
Kwa vile wapinzani wanaonekana kushindwa kuliangalia tatizo kama lilivyo, na badala yake wanaangalia makada wachache, basi wananchi wafanye kama walivyofanya wenzao wa Burkina Faso kwa kuingia mitaani na kutaka serikali husika iwajibishwe kwa kushinda kutetea na kulinda maslahi yao. Na hili linawezekana hasa ikizingatiwa kuwa wafadhili nao wanaona kama CCM na serikali yake wameishiwa udhu na uwezo wa kutawala. Pia uwapo wa International Criminal Court (ICC) kunatoa fursa zaidi kwa watanzania kujiletea ukombozi wa kweli baada ya wanasiasa kuonekana kushindwa na kuwaangusha kwa kuangalia karibu.
Tumalizie kwa kuwataka wabunge wafumue serikali nzima. Na kama watagoma au kushindwa basi wananchi waiwajibishe serikali na chama ambavyo vimegeuka washirika wazuri wa wezi wa fedha za umma maskini wa nchi ombaomba na inayoishi kwa kukopakopa.
Chanzo: Dira ya Mtanzania.

2 comments:

Anonymous said...

Wapiga kura wao ambao ni watanzania

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umesikika.