The Chant of Savant

Saturday 3 January 2015

Kwa Walevi 2015 ni mwaka wa kupigika sana


          Baada ya kushuhudia ujambazi na kila aina ya jinai vikiteka kaya, Mlevi napanga kunywa na kuvuta kama sina akili nzuri. Japo si muumini wa utabiri uchwara ulengao kuwapa wasaka tonge ulaji, naamini mwaka huu unaoanza utakuwa mgumu kuliko uliopita tokana na sababu zifuatazo:
          Mosi, kaya inajiandaa kwa ajili ya uchakachuaji ambao wengine hupenda kuuita uchaguzi.  Bila shaka, utagharimu njuluku kibao kiasi cha wengi kusahaulika ili kuhudumia wanasiasa na ndoto zao za kutaka ulaji zaidi. Bei za bidhaa muhimu zitapaa huku kodi ya kanywaji sigara na bangi zipandishwa kufidia pengo kama ilivyozoeleka hasa kutokana na ukame wa mipango na ubunifu. Bajeti za bangi sigara na ulabu zitaongezeka kama kawa.
          Pili, ukiachia mbali uchakachuaji au tuseme usasi wa walaji, ufisadi utashamiri hasa kipindi hiki kuelekea uchakachuaji ambapo wasaka tonge watafanya kila mbinu kupata njuluku ya kuwahonga wapika kura ya kula. Ninaposema ukwapuaji msidhani ni wa njuluku ya tumbaku. Ni ukwapuaji wa mabilioni ya umma ambayo mkuu atasema ni ya wakwapuaji. Pia madafu ya Danganyika yataporomoka. Rejea kila tunapobadilisha kiranja akaja na sera na walaji wapya njuluku inavyoporomoka kichizi.
          Tatu, walevi watazidi kuzaliana huku huduma za jamii zikipungua tokana na mipango mibovu na walaji wengi kwenye lisirikali. Idadi ya walevi itafura kuliko wakati wowote katika historia tokana na wakimbizi wengi wa kiuchumi toka Asia na kaya jirani kuingia na kuishi kinyume cha sheria baada ya kutembeza mshiko kwa wakubwa wa uhamiaji. Mabohari mengi mnayodhani yamejaa bidhaa yataongeza idadi ya wakazi wake huku klabu za usiku za kichangu za wageni zitaongezeka na maafisa husika watazidi kuwa matajiri kwa kuwatoa upepo wasafirishaji binadamu wa kike.
          Nne, madawa feki yataongezeka mitaani huku walevi wakizidi kuibiwa kwa kuuziwa midawa hii ambayo mingi itawanyotoa roho au kuwaachia madhara ya kudumu. Nani anajali hata wakipungua iwapo wenye nazo na ulaji wao wanaangalia afya zao au kutibiwa ughaibuni? 
          Tano, walaji, kadhalika, wataongezeka sambamba na wachukuaji wapya na wa zamani wakiendelea kung’ang’ania ulaji. Hapa jamaa zangu wa kigabacholi watakuwa wanawinda walaji wa kudhamini ili nao walinde na kutetea ulaji wao. Maana, kwa siasa za kisasa na kisasi kijambazi za ulaji bila mfadhili, hakuna anayeweza kutoboa vinginevyo awe ameiba kweli kweli kama jamaa yetu wa Richmonduli alivyofanya hadi akawa na uchache wa kumwaga kila mahali ili apewe ulaji ajilipe mara mia. Mmesahau jamaa yetu aliyeingia kwa EPA alivyowawezesha wafadhili wake kwa kuwalipa fadhila? Kama mmesahau, mwaka huu msisahau tena mkaliwa zaidi na zaidi huku mkijiona. Mtume wenu kwa walevi ameishawaonya. Mkiendelea na uzezeta msimlaumu kuwa hakusema. Na hiyo ni zawadi yake ya mwaka mpya kwenu.        
          Sita, kwa vile njuluku nyingi itatumika katika kuwafadhili wagombeaji ulaji huku nao wakilipa fadhila baada ya kuukwaa hii itafanya maisha ya walevi kuwa magumu zaidi. Mara hii mmesahau alipoondoka Mr Denjaman Makapi na kuingia kwa filamu mpya ya ANGUKA? Mtaanguka kweli kweli. Sitanii. Msipobadili namna mlivyozoea kufanya mambo tena mambo yenyewe madudu matupu, mtaliwa zaidi na zaidi. Uhalifu utaongezeka na usalama kutoweka. Hata hiyo amani mnayoimba bila kuangalia hali halisi itakuwa msambweni kama siyo kutoweka hasa kutokana na wachache kuwateka walio wengi wakawatumia kama punda na kuishi kwenye pepo iliyozungukwa na bahari ya umaskini wa kunuka.
          Saba, thamani ya madafu itaporomoka kama mgonjwa wa kuharisha. Bei za vitu zitapanda na kufanya maisha kuwa magumu na dunia kuwa kama gunia kwa wasio na maulaji au njuluku au fursa za kuhomola kama walivyofanya jamaa zenu wa escrow ambao wataendelea na biashara ya kuwalangua nishati huku wakichafua mazingira kwa sana tu. Najua kuna kipindi mliwacheka wenzenu wa Zimbabwe kwa kubeba mabilioni ya dola yasiyoweza kununua hata mkate. Msipoamka, yatawafika nanyi mchekwe kama mlivyowacheka wazimbabwe.
          Nane, wake, watoto na jamaa za vigogo wataongezeka kwenye ulaji hasa mjengoni huku na wafanya biashara tena wenye kutia shaka nao kuongezeka ili walinde ima maslahi yao, jamii zao hata wazazi wao. Na hapa ndipo siasa zitakuwa chafu kweli kweli. Bila kuwa na hongo au jina kubwa sahau kuula. Msishangae watuhumiwa wote wa ukwapuaji kama escrow na mwingine uliopita wakapeta na kuendelea kufanya mambo nyuma ya pazia kama Mzee wa Vijisenti anavyoendelea kuvuta uchache na kupewa majukumu mazito ya kubaka katiba mpya bila aibu. Viongozi wengi wa dini wenye kutia shaka watafunga ndoa na mafisadi.
          Tisa, mtegemee maafa yatokanayo na majengo kuporomoka hasa kutokana na yale yalioonyesha wazi kuwa yataua kufumbiwa macho. Barabara mbovu mlizojengewa nazo zitaanza kumeguka na kuharibika hata kabla ya nyingine kuanza kutumika. Waliokuwa wakiwadanganya kwa kujigamba kuwa wamejenga barabara wataadhirika ingawa wengine watakuwa wameishakitoa na kuwaachia kile waingereza huita white elephant.
          Kumi, walevi watazidi kukata tamaa kuliko wakati wowote wa maisha yao. Kwani raslimali zao kama vile madini, wanyama hasa tembo na faru vitafanyiwa kitu mbaya sana huku magenge ya wahalifu yakitajirika wakati wao wakiendelea kuzama kwenye umaskini na hakuna mkubwa atakayejali wala kuwajibishwa kwa jinai hii. Hapa ndipo walevi watalia na kusaga meno wakijilaumu kwanini hawakuwa makini kwenye uchaguzi kwa kuchagua mabadiliko badala ya ukale uliokwisha wafikisha pabaya.

          Kumi na moja, msisahau kuwa biashara haramu ya bwimbwi itaongezeka huku biashara ya magendo nyingine zikiwahusisha wazito vikiongozeka. Rushwa kadhalika itapanda hasa kwenye sekta za ardhi, ajira, biashara, elimu, nishati na uhamiaji. Kwa ufupi, mwaka huu si wa kushangilia bali kutafakari na kutahadhari. Bonne Anne et Bonne Sante especialement mes amis qui boivent comment la poisson. Mtatafsiri wenyewe.
Chanzo: Nipashe Januari 3, 2015.

No comments: