The Chant of Savant

Thursday 12 February 2015

Utawala wa Kikwete utaingia kwenye Guiness book

Japo kila utawala katika nchi yoyote huweka historia iwe mbaya au nzuri, utawala wa sasa utakumbukwa kwa mengi. Utawala wa Awamu ya pili unaendelea kukumbukwa kwa kuanzisha ufisadi tunaoshuhudia kubwa likiwa ni kuuzwa kwa mbuga ya wanyama ya Loliondo na kuruhusu mambo ya hovyo kama vile kutajirika kupitia jinai bila vyombo vya dola kuwashughulikia wahusika. Muendelezo wa kadhia hii ni kutoroshwa wanyama zaidi ya mia hapo Oktoba 26, 2010. Tangu jinai hii kutokea, serikali haikujihangaisha wala kujali kutoa maelezo yanayoingia akilini. Nadhani Tanzania ni nchi pekee duniani inayoweza kuwa na serikali inayoweza kuwa shahidi wa utoroshaji wa wanyama hai mkubwa kama huu. Je tunamkomoa nani na kutoa picha gani kwa vizazi vijavyo?
Awamu ya tatu iliuza mashirika ya umma na kubariki ujambazi huku ikisema kuwa ili kuendelea lazima tukubali uwekezaji ingawa baadaye uligeuka uchukuaji wa mchana. Muendelezo wa hili ni kuzuka kwa makampuni tata na hatari kama IPTL,Richmond na RITES yakiingia nchini yakiwa maskini na kuondoka yakiwa mabilionea tokana na uzembe na mfumo wetu fisadi. Jingine ni familia ya rais mstaafu Benjamin Mkapa na marafiki zake kujitwali mgodi wa kuchimba Makaa ya Mawe wa Kiwira. Nani anaohoji iwapo tuliambiwa tumwache mzee Mkapa afaidi maisha ya ustaafu hata baada ya kutuingiza kwenye matatizo ya kiuchumi na kupora mali zetu hasa nyumba za umma?
Funga kazi katika historia ya taifa hili ni serikali ya awamu ya nne ambayo imevunja rekodi katika kufanya madudu au tuseme kubariki uhujumu. Hata kabla ya kuingia, iliasisi kilichokuja kujulikana kama EPA ambapo mabilioni ya shilingi yaliibwa Benki Kuu na kudaiwa kutumika kwenye uchaguzi wa 2005 bila wahusika kukanusha wala kutaka kuongelea kashfa hii hadi leo. Kama vile haikutosha, miaka mitatu baada ya kuwa madarakani, awamu hii iliasisi balaa jingine yaani kashfa ya wizi wa mabilioni ya umma kupitia kile kilichojulikana kama Richmond. Kama siyo Bunge kujitoa kimasomaso na kuhoji, huenda hakuna ambaye angegushwa wala kuwajibishwa. Hata hivyo, historia itaandika kuwa, kwa mara ya kwanza, Bunge liliweza kumfurusha waziri mkuu na mshirika mkuu wa rais.
 Mchovya asali hachovi mara moja. Baada ya kuacha mambo yapoe, miaka sita baadaye serikali hii ilikuja na kitu kingine kipya yaani kashfa ya Escrow ambayo, nayo kama EPA na Richmond, ilizamisha mabilioni ya fedha za umma maskini wa kitanzania. Wengi walikosea kudhani kuwa kashfa ya Richmond ingetoa somo kwa wahusika wakaacha ufisadi wa kuleta wageni kuanzisha makampuni hewa na kuyatumia kuliibia taifa. Kashfa ya escrow imethibitisha kuwa hawa watu ni wagumu kubadilika na kujifunza na kusoma alama za nyakati kuwa mambo yamebadilika.
Sifa nyingine ya kihistoria kwa utawala wa awamu ya nne ni ile hali ya rais na watu wake wa karibu kusafiri nje mara kwa mara akiandamana na utitiri wa walaji bila kujali kuwa taifa letu ni maskini. Watanzania wamepiga kelele hadi wamechoka. Rais naye kwa upande wake amewapuuzia na kuendelea na ziara zake zisizoisha za mara kwa mara. Je ni fedha kiasi gani tunapoteza hasa kwa taifa ombaomba na maskini?
Sifa nyingine ni kwa utawala wa sasa kuwafumbia macho wauza unga, majambazi na mafisadi hata baada ya rais kukiri hadharani kuwa anazo orodha za waharifu hawa. Je ni nini kilimzuia kuwachukulia hatua wakati anavyo vyombo vyote vya usalama? Je hii haiwezi kujenga dhana potofu kuwa kuna namna rais au watu wake wananufaika na kadhia hizi?
Utawala wa awamu ya nne utaingia kwenye vitabu vya historia kama utawala uliotumia jeshi la polisi vibaya hadi likaibuka na sifa kuu mbili yaani kuwa mabingwa wa kupokea rushw ana kuuua waandamanaji katika sehemu mbali mbali za nchi huku wahusika wasichukuliwe hatua ukiachia mbali kupata ‘sapoti’ ya waziri mkuu Mizengo Pinda kuwa wawapige tu. Hali hii imeendelea ambapo viongozi wa upinzani wananyanyaswa na kukamatwa bila makosa yoyote ukiachia mbali kujengeka chuki baina ya wananchi na jeshi la polisi hadi kufikia kujichukulia sheria mkononi kwa kuvamia na kupora vituo vya polisi.
Funga kazi ya utawala huu ni ile hali ya kuamuru yakusanywe maoni kwa ajili ya kuandika katiba mpya serikali ikaishia kuyachakachua na kuyakataa huku ikipandikiza katiba yake kidhabu. Wengi wa watanzania wanahoji: Kama serikali ilikuwa imeishaandaa katiba yake, kwanini iliwapotezea muda na fedha? Kinachoumiza zaidi ni ile hali ya kuua katiba kielelezo iliyolenga kurekebisha na kusafisha mfumo mbovu na wa kifisadi uliopo na kupandikiza ile inayoonyesha wazi kulea ufisadi. Je tunamkomoa nani? Ajabu ya maajabu ni pale waliotenda jinai hii kusimama kwenye mimbari na kutangaza bila aibu kuwa wameandika katiba rafiki wa watu wakati ukweli ni kwamba katiba ya watu yaani umma iliuawa na kupachikiwa katiba rafiki wa watu ambao si wote bali mafisadi na genge dogo la walaji. Ni matusi kiasi gani kwa watanzania walioibiwa fedha yao na kupotezewa muda?

Kwa vile bado utawala wa sasa haujamaliza ngwe yake, huenda mengi ya ajabu zaidi yakatokea hasa kwenye ngwe hii ya lala salama ambapo wahusika, bila shaka, watafanya kama Mkapa: kusaka mtaji wa kustaafia. Hakika utawala wa sasa utaingia kwenye kitabu cha maajabu duniani cha Guiness!
Chanzo: Dira.

2 comments:

Anonymous said...

Toba tumekwisha
CCM hiyo 2015
Watanzania mkiichagua CCM ntajiuwa nimechoka i sitaki

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umenena. Ni kweli tumekwisha. Tutakwisha zaidi kama CCM itaendelea kutuburuza kwa kisingizio cha kutawala. Ipigwe chini. So be it.