The Chant of Savant

Monday 18 May 2015

Hizi ni dalili kuwa serikali ya CCM ikiri imeshindwa


                Kwa wafuatiliaji wazuri wa mambo yanayoendelea nchini, kuna dalili tosha kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeshindwa vibaya sana. Ingekuwa ni dini tungesema kiama kimekaribia.  Hakika, kama watanzania hasa wapiga kura wangesoma alama za nyakati vizuri, wana kila sababu ya kuiadhibu na kuiwajibisha serikali ya namna hii bila shaka.
Zifuatazo ni dalili tosha kuwa serikali ya CCM imeshindwa:-
Mosi, ni ile hali ya kukosekana kwa usalama kwa wananchi na mali zao. Rejea mauaji ya kishenzi ya mara kwa mara ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Kutamalaki kwa ufisadi, wizi na uporaji wa mali na raslimali za umma. Rejea kusitasita kwa serikali ya CCM kuwashughulikia watuhumiwa wa wizi mfano kashfa ya escrow ambayo imezamisha mabilioni ya fedha ya umma.
    Pili Kuonyesha kushindwa, rais Jakaya Kikwete aliwatoa kafara mawaziri wake wachache bila kuwafikisha mahakamani huku akiendelea kuwafumbia macho watuhumiwa wakuu ambao ni James Rugemalira na Sethi Harbinder Singh ambao wanaendelea kutanua mitaani wakipanga na kupiga dili nyingine. Serikali ambayo ima hawawajibishi wahalifu au kulala nao kitanda kimoja bila shaka haifai na imeshindwa tu.
Tatu , kuhujumu rasimu ya Katiba Mpya kama ilivyokuwa imeandikwa na Tume ya Kukusanya Maoni almaarufu kama Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Nne, matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma. Rejea utoro wa mara kwa mara wa watendaji wa umma ukiachia mbali matumizi yasiyo na nidhamu kiasi cha deni la taifa kuumka bila maelezo ya kutosha wala yanayoingia kichwani. Hata kile kitendo cha wahusika kukaa kimya kinamaanisha wamefikia ukomo wa kufikiria ukiachia mbali kuwa wahusika wakuu wa hujuma hii.
Kukithiri kwa jinai nchini ambapo ujambazi wa kutumia silaha, kughushi nyaraka na vyeti, ufisadi, rushwa na matukio mengine ya namna hii vimetamalaki na hakuna anayejali kuchukua hatua au kutoa maelezo ni kwanini asiwajibishwe. Kwa sasa, watanzania hawana tofauti na wakimbizi, watumwa hata yatima kwenye nchi yao.
Tano, ukosefu wa uzalendo miongoni mwa wananchi na watawala wao. Nani hajui kuwa watanzania, kwa sasa hawana haja ya kuwa wazalendo hasa ikizingatiwa kuwa wanaojitahidi kuonyesha uzalendo ima wanaonekana washamba au maadui wa mafisadi kiasi cha kuwatumia wahuni wawatishe na kuwadhalilisha kama ilivyotokea kwa jaji Warioba?
Sita, serikali kutokuwa na msimamo mmoja katika utendaji wake. Rejea maneno ya mara kwa mara ya Katibu mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana akiitupia vijembe serikali yake kuonyesha kuwa hakuna mawasiliano wala mshikamano baina ya serikali na wanaoiunda. Hivi karibuni Kinana alitoa mpya alipokaririwa akisema, “Kila kona ni kodi na kila kukicha ni kodi, Sumatra anadai kodi, Fire wanadai kodi, taasisi zingine zinadai kodi, yaani ni kero tupu.” Sasa kama Kinana mwenye serikali yake analia hawa wananchi wafanye nini?
Hebu angalia uhovyo na usanii wa Kinana ulipo. Aliongeza kusema, “Sihamasishi wafanyabiashara mgome, lakini nasema hivi, hata Museveni aliwaambia URA kwamba ninaweza kubadiri idara za kodi lakini hawa wataendelea kulipa kodi, hivyo wafanyabiashara ni bora zaidi kuliko idara za kodi.” Ukimuuliza alichokuwa akimaanisha na nini jibu la tatizo unagundua usanii wa kitoto na uongo wa mchana. Unalalamika ili iweje kama siyo kuwahamasisha wananchi wazigomee hizo kodi unazoona hazistahili na si za haki?
            Japo Kinana anatumia majukwaa kumwaga chozi la mamba, anatusaidia kugundua uoza na kushindwa kwa serikali yake. Kimsingi, wananchi wanapaswa wasimchukulie kama kiongozi anayewaonea huruma au kuwatakia mema wakati anayewashindilia kodi ni serikali yake ambayo bila shaka naye anahusika kwa vile ni mmoja wa walaji wa kodi hizo hizo anazojifanya kulalamikia.
Kuonyesha kuwa serikali ya CCM imeishiwa, kumekuwapo mparaganyiko karibu katika kila jambo. Imekuwa ikifanya mambo kana kwamba si serikali kwa maana ya kushindwa kutumia asasi zake vizuri.
Saba, kuongezeka kwa matumizi ya mabavu na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na polisi kwa maagizo na amri za serikali kuu. Badala ya jeshi la polisi kuwalinda wananchi, limejipatia sifa ya kuwatesa, kuwanyanyasa, kuwahujumu hata kuwaua bila sababu.
Nane, serikali kutokuwa na sera ya kuendeshea nchi. Ukiuliza serikali kwa sasa inatumia sera gani kuendesha nchi, hutapata jibu. Kama kuna sera inayoonekana kwa wananchi si nyingine bali usanii na ubabaishaji ambapo kila mtu anajifanyia atakavyo na ajuavyo ilmradi aweza kubangaiza na bora liende hasa kwa watu wa kawaida.
Tisa, kukithiri kwa kujuana katika ajira na kuvumiliana kwa wale wanaotenda maovu kwenye ofisi za umma. Rejea rais kuwakingia kifua majambazi, wauza unga, walioghushi na mafisadi. Hii ni dalili kuwa ima serikali inawagwaya, inashirikiana nao au haina uwezo wa kufanya lolote katika kutekeleza sheria. Rejea uoza uliofichuliwa kwenye idara ya uhamiaji hivi karibuni ambapo waajiriwa karibu wote walikuwa ndugu au watoto wa vigogo au marafiki zao. Nani wamechukuliwa hatua zaidi ya kufunika kombe mwanaharamu akapita? Hata hivyo, nani angemwajibisha nani wakati wote mchezo wao ni mmoja?
Kumi, kuua uchumi. Ingawa takwimu zitolewazo na serikali, mara nyingi, huonyesha mafanikio. Je hali za wananchi wa kawaida zinasemaje? Ukiuliza uchumi unawezaje kukua sambamba na wizi, ufisadi, rushwa, misamaha ya kodi na matumizi mabaya ya fedha za umma? Hupata jibu.
Tuhitimishe kwa kuwataarifu watanzania kuwa serikali ya CCM imeshindwa. Hivyo wafikirie mbadala wake hasa kwenye uchaguzi ujao. Hata hivyo, watawala wa Tanzania wana bahati ya mtende. Maana ingekuwa nchi nyingine wasingepata hiyo nafasi ya kungojea uchaguzi kam ilivyotokea kule Burkina Faso miezi michache iliyopita. Hakika serikali ya CCM imeshindwa. Iadhibiwe na kuwajibishwa ili kuliokoa taifa.
Chanzo: Dira.

No comments: