The Chant of Savant

Saturday 11 July 2015

Zitto anamdanganya nani?

















          Wanasiasa hawa waliochoka huwa wana tabia moja kubwa –hujionyesha kama hawajachoka. Mwenyekiti wa ACT wazalendo, Zitto Kabwe ambaye nimekuwa nikimheshimu sana, ameingia kwenye kundi hili. Sijui kama anajua au ni kwa bahati mbaya. Hivi karibuni akiwa Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Zitto alisema: “Majina ninayo haya hapa niwataje nisiwatajee! Ni wengi sana wengine wanamiliki kampuni kubwa.” ajabu Zitto hakujataja eti kwa sababu za kisheria. Sababu zipi  kama mhusika ana ushahidi wa kutosha na si maigizo na sanaa? Mbona Dk Wilbrod Slaa pale Mwembe Yanga Temeke mnamo15 Septemba, 2007 alitaja bila kificho wala kujificha nyuma ya legal technicalities au sababu za kisheria?
Ushahidi wa kimazingira unamuonyesha Zitto kama mtu mwenye ushahidi usio na uhakika au wa kuokoteza kama si kutengeneza ili kutafuta umaarufu kisiasa. Nijuacho mimi ni kwamba , kama una uhakika na ushahidi wako huna haja ya kuuficha. Ukiona mtu anasitasita kwenye ushahidi anaodai kuwa nao mtilie shaka. Zitto amenikumbusha marehemu Oscar Kambona aliyedai kuwa marehemu baba wa taifa alikuwa na fedha nyingi nje. Nyerere alimjibu kuwa amwage data ili watanzania wapime. Kutokana na kutokuwa na ushahidi madhubuti, Kambona aliishia kunywea  hadi mauti yanamkumba. Zitto asitake tumuweke kwenye kundi hili. Kama ana ushahidi na ameupata kisayansi basi amwage na wenye kuguswa washitaki ili wakutane mahakamani akama alivyofanya Dk Slaa Mwembe Yanga.
Zitto asitake kutupotezea muda au kutugeuza watoto au hamnazo. Kama ana uhakika na ushahidi wake anaogopa sheria gani wakati wahusika wakienda mahakamani atautumia ushahidi wake kuwaziba vinywa?
Kuonyesha alivyo mbabaishaji, gazeti moja liliripoti tukio la Zitto kuanika majina ya wenye fedha Uswizi ifuatavyo: Wakati maofisa wa ACT wakigawa orodha ya majina hayo, wananchi walionekana kuwa na shauku ya kupata nakala ya karatasi hiyo yenye majina 99 ya wafanyabiashara hao maarufu ndani na nje ya nchi, lakini kiongozi huyo hakuwa tayari kuwapatia na badala yake akiwaambia wasome magazeti ya kesho. Hata kesho yake ilipofika hakukuwa na kitu kwenye magazeti zaidi ya habari kuwa Zitto aligwaya kuwataja hao watu wake. Ajabu ya maajabu, badala ya kuanika uoza wa watuhumiwa, Zitto alianika uoza wake kuwa anachofanya ni usanii. Kwani angekuwa na data asingesita kumwaga ili kila mtu ajionee na kuamua mwenyewe. Tumempa mfano hai hapo juu kuhusiana na tukio ambalo limeacha historia ya pekee la Mwembe Yanga ambapo Dk Slaa alitimiza ahadi yake ya kuwataja mafisadi ambao hawajawahi kwenda mahakamani kwa vile alichosema ni ukweli mtupu.
Kwa upande wake, Zitto anapaswa aambiwe aache utoto na ubabaishaji. Kama ana orodha ya watuhumiwa wa kuficha fedha Uswizi aaanike. Kwanini Zitto anashindwa kujitofautisha na rais Jakaya Kikwete aliyejivua nguo hadharani kudai ana orodha ya majambazi, mafisadi na wauza unga akaishia kuumbuka hadi anaondoka na pigo hili. Je Kikwete alikuwa na orodha hizo au ulikuwa ni mkwara sawa na wa Zitto? Nadhani wakati wa siasa za kibabaishaji na kitoto tena zikifanywa na watu wazima umepita. Kama Zitto kweli ana majina, hana sababu ya kuyaficha au kuyatoa kwa baadhi ya watu. Je Zitto alidhani waandishi wa habari ni mabwege na wajinga kiasi cha kuanika majina ambayo mwenye kuyatoa ameogopa kuyaanika? Zitto go tell it to the birds. Acha usanii na unachosema ni majina ni uzushi vinginevyo usingeogopa kuuweka wazi mwenyewe.
Japo alipotimliwa kutokana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wengi walikosea kuona kama anaonewa, sasa Zitto anaanza kuonyesha sura yake halisi. Kama Augustine Mrema, Zitto si mali chochote zaidi ya mtafuta ukuu na mkuu bila kufuata utaratibu. Kitendo cha Zitto kutamka kuwa ataweka wazi majina ya mafisadi walioficha fedha Uswizi akaishia kugwaya na kuufyata ni ushindi kwa haki kuwa waliomtimua CHADEMA hawakumuonea. Zitto anazidi kufichua sura yake ya kweli ambayo wengi hawakuijua.  Wapo wanaomuona kama mtu mwenye papara na siye na subira. Pia wapo wanaomuona kama mroho wa madaraka asiyeangalia hata njia anayochukua kuyafikia. Na yote kati ya yote hajakomaa kisiasa.
Na hii si mara ya kwanza kwa Zitto kuonyesha uhovyo na uoza wake. Alipokabiliwa na tishio la kutimliwa toka CHADEMA alisikika akitishia kumwaga mtama kuhusiana na uoza wa CHADEMA. Nini kilitokea zaidi ya kunywea na kuanza kuomba msamaha huku CHADEMA wakiamua kuondoa gugu kwenye shamba lao? Muone sasa akiwa nje tena kwenye chama alichokianzisha kabla ya kuhama CHADEMA anavyoendelea kuadhirika. Tumemlinganisha Zitto na Mrema kwa makusudi. Wote wawili wanafanana kwa tabia na haiba.

Tumalize kwa kumuuliza Zitto, je anataka kumhadaa na kumdanganya nani? je kwanini habadiliki wala kusoma alama za nyakati kuwa wakati wa siasa za kisanii, usaka tonge na uganganjaa ulikwisha zamani? Je Zitto anatoa tishio hili ili kupata nini kama siyo kutafuta umaarufu na saa nyingine chochote kitu? Je atafanikiwa wakati janja yake imeishajulikana? Nategemea Zitto atajibu hoja hizi. Kwani ana nafasi ya kufanya hivyo.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 12, 2015.

No comments: