The Chant of Savant

Friday 17 July 2015

Zitto, mabilioni ya Uswisi na Yeremia 5:21: Makala hii imenichanganya

 KUNA wakati, Mwenyezi Mungu ametumia lugha inayoweza kuonekana kali kupitia maandiko yake matakatifu. Kwa mfano, kitabu cha Yeremia 5:21 alisema; “Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu, mlio na macho ila hamuoni, mlio na masikio ila hamsikii”. Binadamu hawana ugeni kwa Mungu, anawajua! Unaweza kuwawashia taa na wakalalamika wapo gizani. Ukiwapa chakula, watakula na kusaza lakini baadaye watalalamika wamepunjwa au hawajala kabisa. Wape maji, kiu zikiwaisha watayatoa kasoro maji yako, ama kwa baridi, moto au vyovyote vile! Ndiyo sababu amesema nao kwa ukali. Mwenye macho anaweza kujifanya kipofu asiyeona kuliko mlemavu mwenyewe. Aliye na masikio yake timamu, atajidai hasikii. Akiamua asione wala kusikia, hata utumie picha na sauti gani, atakwambia hasikii wala haoni. Haina tofauti na ule msemo wa Kiswahili “Akutukanaye hakuchagulii tusi”, kwamba lolote linalokuja mbele yake atalitoa ilimradi litamkera au kumvunja moyo anayemkusudia. Kwa kawaida asiyekupenda hana jema na wewe. Utafanya kubwa litakataliwa au kushushwa thamani. Upepo unapokuwa mzuri, kwa wanaokupenda, hata waambiwe lipi baya hawataamini. Watakataa kila ovu utakalotupiwa na litatukuzwa kila zuri ambalo litaelekezwa kwako. Katika Uchaguzi Mkuu wa Liberia mwaka 1997, Waliberia, hususan vijana, walionywa kuhusu Charles Taylor, aliyekuwa anawania Urais wa nchi hiyo, baada ya vita vya kiraia. Wachambuzi wa mambo walionya kuwa Taylor ni mtu hatari, aliyesababisha nchi kuingia vitani na hata vifo. Vijana walikumbushwa kwamba wengi wao walipoteza wazazi wao kwa sababu ya vita iliyochochewa na uroho wa madaraka wa Taylor. Vijana hawakuambiwa kitu, ndiyo kwanza waliimba mitaani kauli mbiu ya “alimuua mama, alimuua baba, lakini nitamchagua…” (he killed my ma, he killed my pa, but I will vote for him). Ni ile ile dhana ya kuwa na macho lakini unajifanya huoni. Umepewa masikio hai lakini kwa makusudi eti husikii. Taylor alishinda urais kwa zaidi ya asilimia 75, ikiwa ni ushindi wenye upinzani dhaifu. Hata hivyo, yaliyotokea baadaye kila Mliberia alijuta. Walipopigana vita ya pili ya wenyewe kwa wenyewe, walijutia uamuzi wa kutoona na kutosikia kila baya lililosemwa kuhusu Taylor. Julai 4, mwaka huu, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, alifanya mkutano mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, kwa ajili ya kukitambulisha chama chake kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam. Katika mkutano huo, alitoa majina 99 ya Watanzania wenye akaunti kwenye Benki ya HSBC, Uswisi. Kwa mujibu wa Zitto, orodha hiyo imepatikana kwenye tawi moja tu katika benki hiyo. Maana yake ni kwamba pengine matawi mengine ya benki hiyo kuna majina mengine ya Watanzania ambao wameficha fedha zao. Kwanza; alichokisema Zitto hakikuwa hukumu kwamba majina yale 99 ndiyo hasa walioficha fedha haramu Uswisi. Alichosema ni kuwa kuyaweka kwake wazi majina hayo ni njia mojawapo ya kuichokoza serikali ili iweke mkazo wa uchunguzi. Pili; hotuba ya Zitto ilikuwa wazi kuwa Watanzania walioficha fedha nje ya nchi ni wengi na mataifa yanayohusika na ufichwaji wa fedha za Watanzania ni mengi. Kama uchunguzi utafanyika yapo mengi yenye faida yanaweza kujulikana. Kwa vyovyote vile, uhifadhi wa fedha nje ya nchi, hata kama ni halali, una madhara kiuchumi kwa nchi. Mfanyabiashara anayeweka fedha zake nje, maana yake zinaingia kwenye mzunguko wa kibiashara kwa benki ya nchi husika ambayo inanufaika kwa kukata kodi na makato mengine. Hivyo, kama fedha hizo zingehifadhiwa Tanzania, taifa lingefaidika kibiashara na kikodi. Kwa msingi ulio wazi ni kwamba yeyote ambaye anaishi Tanzania na kufanya shughuli zake ndani ya nchi kisha kutunza fedha zake nje, huyo ni msaliti kwa nchi. Hili lingeweza kuonwa haraka kisha Zitto angepewa pongezi zake. Kilichotokea badala yake ni Zitto kushambuliwa. Hoja kubwa ikihusu asili ya majina yaliyomo kwenye orodha iliyotolewa na Zitto. Kwamba mbona wote ni kama wana asili ya Bara la Asia? Wanasahau kuwa upo uhuni wa kutumia majina ya watu, kwamba mtu fulani kwa kutambua kuwa ikigundulika amehifadhi fedha kwenye akaunti ya nje ya nchi lazima atiliwe shaka, ataamua kutumia akaunti ya mtu mwingine ili kupata kivuli cha uchafu wake. Hapahapa nchini, inajulikana kuna watu wanaoitwa vigogo serikalini, wanamiliki makampuni ambayo majina ya wamiliki ni ya wengine kabisa. Mkurugenzi wa shirika la umma anaidhinisha zabuni kwa kampuni ambayo yeye ndiye mmiliki lakini ukienda kukagua majina yanayotambulika kama wamiliki huwezi kumkuta. Kama hayo yangetazamwa, Zitto asingezodolewa. Ingeshtua mjadala mkubwa sana wa kitaifa. Jina moja baada ya lingine lingepitiwa kujua anafanyaje biashara zake nchini, analipaje kodi na washirika wake wa kibiashara ni akina nani. Hatuwezi kufika huko kwa sababu kuna tabaka la watu ambao walishaamua kuwa ‘anti-Zitto’, yaani wapinga Zitto kwa jema kwa baya. Hao ndiyo wale ambao inyeshe mvua, liwake jua hawakubaliani na Zitto, imekuwa rahisi zaidi kwao kupaza sauti na kutamka, “alitafuta kiki.” Huyo anayesemwa anatafuta umaarufu, alishakuwa nao kitaifa, tena kwa kiwango kizuri, yapata miaka 10 sasa. Akutukanaye hakuchagulii tusi! Ilivyo ni kuwa Zitto angetaja majina ya wabantu, waliozoeleka kwa kashfa za ufisadi, bado angezodolewa. Yangetajwa majina ya wawania Urais 2015, angeambiwa amenunuliwa na ametumwa na makundi ya wagombea Urais. Ni yaleyale ya Yeremia 5:21, kuwa wana macho yao lakini hawaoni, na masikio wanayo ila wanagoma tu kusikia. Wataalam wa kupinga wanapokuwa kazini, thawabu wataita dhambi na dhambi itapambwa na kutukuzwa kwamba ni thawabu. Kama hatukukubali, baya lako tutalishangilia na uzuri wako tutaukataa. Hii ndiyo vita ambayo Zitto anakabiliana nayo. Bahati mbaya ni kuwa Zitto pengine hajui kwamba hawezi kuwa na jema la kuwafurahisha wanaompinga. Na ndiyo maana wakati mwingine anajaribu kuwalazimisha wamuelewe kwamba yeye ni mzuri kuliko wale waliotengeneza mpango wa kumpachika jina la msaliti au Yuda. Anawaambia “kwenye ilani ya kilichokuwa chama chetu, tulikubaliana tusichukue posho za vikao maana ni kuwanyonya wananchi, mimi peke yangu sikuchukua, wenzangu wote walisaliti na kuchukua posho, nani msaliti hapo?” Kwa sababu hawaoni wala kusikia kwa makusudi, jibu lao linabaki lilelile, msaliti ni Zitto. Anawaambia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni anatumia gari la kifahari kinyume na matakwa ya ilani ya chama chake katika Uchaguzi 2010. Mwanzoni alilikataa kisha akazunguka nyuma ya pazia na kulichukua. Hapo ni nani msaliti? Wanamjibu msaliti ni Zitto! Unadhani ni kweli hawasikii na hawaoni? La hasha! Isipokuwa ni ule msemo wa “kipendacho roho hula nyama mbichi.” Yeye anayewaambia hayo hayo maneno hawampendi, wanaamini katika njia walizopitishwa kwamba ni msaliti, kwa hiyo hata aseme maneno yenye rangi gani za kupendeza hawatamkubali. Zaidi, huyo anayewashawishi wamuone ndiye msaliti, wao wanampenda sana. Ni mvurugano tu hapo, ni ile lugha gongana. Sikitiko langu siku hizi hata waandishi tunakuwa wacheza karata kama mawakili mahakamani. Mteja wake ameua na hilo analijua lakini anaamua kutengeneza njia za kumfanya mteja wake aponyoke na aonekane hana hatia ya kuua. Ni michezo tu, waandishi nasi tunaamua kuangalia habari, kuichekecha na kuiwasilisha katika sura inayompendeza na kambi yake. Kama mhusika ni kipenzi chake na habari ni mbaya, anaigeuza ionekane nzuri na kuiwasilisha. Na ikiwa ni nzuri kwa asiyempenda, anaichezea ili iwe na ladha mbaya kwa mhusika. Ni uleule mtindo wa wakili na mteja! Ni suala la muda tu, muhimu ni kwa Zitto kuendelea kufanya kazi nzuri, wakati ukifika watu watageuka. Kwa kawaida huhitaji muda na uvumilivu wa kutosha kumbadilisha aliye amini. Upo msemo wa Kiingereza; Who love too much, hate in the like extreme, kwamba anayependa sana ndiye huchukia kupita kiasi. Tuvute subira, muda utafika! Mwandishi wa makala haya, Luqman Maloto ni mwandishi wa habari na vitabu. Anapatikana kwa simu namba 0683 35 57 17 
Chanzo: Raia Mwema  Julai 15, 2015

No comments: