The Chant of Savant

Friday 21 August 2015

Je kampeni umeuona mtego uliomo?


          Japo tunaambiwa kuwa muda maalumu kisheria wa kuanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao hazijaanza, sidhani kama hili ni kwa wote. Hivi karibuni, mgombea wa upinzani, Edward Lowassa ameonekana kwenye miji mikubwa mbali mbali akivuta umati wa watu huku akijisifu kuwa anakubalika.
          Kwa vile muda maalumu wa kuanza kampeni haujafika, wengi wanajiuliza, anachofanya Lowassa ni nini kama si kampeni tena kabla ya muda muafaka kufika? Je anachofanya Lowassa kingefanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wapinzani wangenyamaza kama ilivyofanya CCM? Je ni kwanini CCM imenyamazia uvunjaji huu wa kanuni? Wapo wanaoamini kuwa CCM imeamua kunyamaza ili wapinzani waseme wamalize yote halafu ije kwa kustukiza na kuwazima kama kibatari. Sijui kama wapinzani wameishaling’amua hili.
          Hata hivyo, wengi hawashangai wapinzani kuendelea kuingia mtego huu wa kufanya kampeni kabla ya wakati hasa ikizingatiwa kuwa maamuzi ya kumpokea na kumpitisha Lowassa hivi karibuni yamewaonyesha kama watu wasio makini na serious.
          Sijui kama wapinzani wanaliona hili. Ukiangalia walivyompwakia Lowassa kwa imani kuwa watachukua nchi, huenda ni dhana hiyo hiyo wanayotumia kuwa wakianza kampeni kabla ya wakati watazoa wapenzi, wafuasi na wapiga kura wasijue siyo. Si kawaida kwa chama kikongwe kama CCM kunyamazia rafu hii kama hakuna faida kwake.
          Kunyamaza kwa CCM kunaweza kutafsiriwa kama janja ya kutathmini ufuasi wa upinzani na madhara ya kisiasa unayoweza kuisababishia CCM. Pili kunyamaza kwa CCM ni njia ya kisayansi ya kubaini maeneo ambapo upinzani una nguvu.
          Tatu, ni fursa ya kujua mbinu na mikakati waliyopanga kutumia wapinzani ukiachia mbali kuorodhesha hoja za wapinzani na kuzijibu. Siasa hasa za uchaguzi ni kama mchezo wa ngumi. Mhusika hapaswi kutumia nguvu zote mwanzoni. Kwani kufanya hivyo humfanya achoke mapema na hivyo kutwangwa kwa knockout kirahisi. Au tuiweke hivi. Harakati za uchaguzi ni sawa na mbio za marathon ambapo mkimbiaji mahiri huanza taratibu ili kutunza nguvu ambayo huionyesha anapokaribia mstari wa ushindi.
          Ukiangalia Bara na Visiwani, CCM inacheza mchezo ule wa wait and see yaani ngojea na uone. Inashangaza kuona upinzani –pamoja na kuwa na viongozi wengi wasomi –unaingia kwenye kile ambacho wataalamu wa vita huita booby trap yaani mtego shutukizi. Japo ni mapema kusema, mikiki mikiki ya uchaguzi itakapoanza kwa upande wa CCM itawastua wengi kwa namna watakavyowamaliza wapinzani.
          Wengi walitegemea wapinzani wangekaa kimya huku wakisoma na kujifunza udhaifu ambao CCM itatumia kuwakabili. Lakini si hivyo. Wapinzani wameishaanza hata kujitangazia ushindi wasijue ngoma bado mbichi!
          Ukiachia mbali kukurupuka, upinzani una kibarua kingine kikubwa ambacho ni kuonyesha kuwa ukweli wao wa awali ni uongo na uongo wao wa sasa ndiyo ukweli. Kwa kumpokea na kumsimamisha Lowassa ambaye wapinzani walimuonyesha kama mtu fisadi watakuwa na kibarua kigumu kumsafisha. Je wataweza na kufanikiwa? Je hili ndilo linalowahangaisha wapinzani kuanza kampeni mapema ili kumsafisha mtu wao waliyemchafua wenyewe pamoja na kuwa naye pia alijichafua hata kabla ya wapinzani kumuanika?
          Ukiachia mbali Lowassa kama mtu binafsi,je ana sera gani zinazoweza kuwavutia wapiga kura na wananchi waliokwisha choshwa na ufisadi?
          Wengi wangetamani kusikia mipango ya Lowassa hasa namna ya kupambana na ufisadi. Pia hata matamko machache aliyotoa kuwa anataka kuifanya Tanzania iwe tajiri bado hayaeleweki hasa ikizingatiwa kuwa haelezi ni sera gani atatumia kulifanikisha hili. Wengi watataka awaeleze ni kwanini alishindwa kulifanya hili alipokuwa madarakani na badala yake akafanya kinyume. Sijui kama kuingiza Richmond na kutumia fedha za EPA kutafuta urais ilikuwa ni sera nzuri ya kutajirisha zaidi ya kufilisi nchi. Lowassa ana mengi ya kujibu ukilinganisha na mgombea wa CCM Dk John Magufuli ambaye rekodi yake ya utendaji kazi haina shaka yoyote. Je Magufuli na CCM wanajivunia hili kiasi cha kuwaacha wapinzani wahangaike ili waje wawamalize mwishoni ambapo hawatakuwa na muda wala fursa ya kujibu mapigo? Je CCM wanawaacha wapinzani watumie raslimali zao kabla ya wakati muafaka ili wakati ukifika wawe wameishafilisika kimkakati na kulhali? Yote yanawezekana hasa ikizingatiwa kuwa si mara ya kwanza kwa CCM kushiriki uchaguzi mkuu ikilinganishwa na wapinzani wanaposhiriki kwa mara ya kwanza wakiwa na mgombea wa CCM tena mwenye kutia shaka.
          Kitu kingine kinachofanya wachambuzi waone ni kwanini CCM imeamua kukaa kimya kwanza, ni ile hali ya uzoefu walioupata mwaka 1995 wakati waziri wake wa mambo ya ndani Augustine Lyatonga Mrema alipojitoa chamani na kujiunga na upinzani akaishia kushindwa na kuzama nao. Kwa wanaojua hasara iliyotokea kwa upinzani mwaka huo, wanasikitika kuwa kishindo cha anguko mwaka huu kitakuwa kikubwa hasa ikizingatiwa kuwa Lowassa anaweza kushindwa na kuzama na vyama vikubwa vinne vilivyokuwa vinaonekana kuwa tegemeo kitaifa. Hata hivyo, wengi wanahoji ukubwa na ushawishi wa vyama husika iwapo vinazidiwa na mtu mmoja kiasi cha kumpokea, kumnyenyekea na kumwachia aamue atakacho hata kama hakiingii akilini kama kupeperusha bendera ya upinzani. Ingawa ni mapema kutabiri matokeo ya uchaguzi ujao, mshindi anajulikana hasa kutokana na sifa na mikakati ya wagombea.
Chanzo: Dira

No comments: