The Chant of Savant

Thursday 27 August 2015

Je ni mwanzo wa mwisho wa CCM?


          Si uvumi tena. Waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye ametua kwenye upinzani akimfuatia waziri mwingine wa zamani Edward Lowassa. Haijawahi kutokea kwenye nchi yoyote duniani!  Sasa Sumaye yuko nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Bila shaka CCM hawakulitegemea hili sawa na la kuondoka Lowassa. Je kuondoka kwa Sumaye kutaleta mtikisiko au kubakia kuwa unyasi mmoja kwenye msonge? Je CCM itatikisika au kuendelea kujikaza kisabuni wakati mambo yakizidi kuwa mabaya? Ama kweli kwenye mchezo wa siasa hakuna anayeweza kutabiri lolote kwa ukamilifu tokana na wachezaji kusifika kwa uongo wao. Kwa waliomsikia Sumaye akisema kuwa kama CCM ingeteua fisadi angejitoa, hawakutegemea hili hasa ikizingatiwa amemfuata fisadi yule yule aliyempinga! Je kuondoka kwa Sumaye kutaiathiri CCM? Je amefanya hivyo kwa sababu na hoja au kulipiza kisasi kwa kutopitishwa kupeperusha bendera ya CCM? Je Sumaye amesoma vizuri alama za wakati? Ama kweli, ukishangaa ya Musa utaona ya Firauni!
          Alipojiengua Lowassa mengi yalisemwa kubwa likiwa ni tamaa yake ya urais. Je Sumaye ambaye amejiengua baada ya zoezi la kusaka urais kufungwa naye watasemaje? Majibu anayo Sumaye mwenyewe aliyekaririwa akisema, “Naamini Ukawa watashinda uchaguzi huu, CCM wamezubaa wakidhani watashinda wakati wananchi wamewachoka, wanahitaji mabadiliko.” Sasa tunajua kuwa kumbe Sumaye amefuata ushindi na siyo sera wala nini. Je Sumaye amesoma alama za wakati au kufuata ushindi?
          Japo waliotabiri kuwa CCM ingefia mikononi mwa rais Jakaya Kikwete waliposema hivyo walibezwa, lolote laweza kutokea kuanzia sasa. Maana haiwezekani chama ambacho kimehimili kufutika kashfa kama vile Escrow, EPA, utoroshaji wa pembe za ndovu tena ukiwahusisha wakuu wake kikakubalika na kupendwa na wananchi.  Je CCM itatumia miujiza gani kuzima upepo huu unaoielekeza kuzimu kisiasa ambapo vigogo wake wanazidi kuitupa mkono? Sitashangaa nikisikia wakongwe kama Kingunge Ngombale Mwale, Joseph Bukuku, Joseph Walioba na wengine wameipiga teke. Maana, imekuwa kichwa ngumu hasa pale ilipoua katiba mpya na kuendelea kuwalea, kuwaendekeza na kuwakumbatia mafisadi. Hata hivyo, kwa kushika dola muda mrefu, CCM bado ina nyenzo ukiachia mbali kuwa na roho ya paka. Je kama itatumia mabavu na kushinda na upinzani ukaamua kukomaa watu watashindwa kuishia The Hague kama jirani zetu wa Kenya?
          Hata hivyo, wapo wanaohoji kama Sumaye ana jipya ikizingatiwa kuwa haya yaliyowachosha watanzania kama anavyodai mengine ameyaasisi na rafiki yake Benjamin Mkapa? Hawa ni wale wanaosema: Lao moja. Kimsingi, hawa wanashindwa kumtofautisha Sumaye na Lowassa na mgombea wa CCM Dk John Magufuli kwa sababu wote walikuwa kwenye chama hicho hicho kinacholaumiwa. Je kuondoka CCM kutaleta nafuu na kubadilisha mambo?
          Tukiangalia upande wa pili, CCM imekuwa ikijiridhisha kwa kuwaita wanaoihama kuwa oil chafu. Je wataendelea na jeuri hii au kubadilika? Maana, oil chafu inazidi kuchafua hali ya hewa huku injini ilimotoka ikizidi ku-knock. Je kweli wanaotoka ni oil chafu au oil chafu ni  ile iliyobaki kwenye injini husika? Hili swali ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wanaamini kuwa mageuzi yanaweza kuja kupitia upinzani huku ukale ukiendelezwa na CCM. Je hapa oil chafu ni ipi kwenye macho ya wananchi ambao kimsingi ndiyo waamuzi kwenye uchaguzi ujao?
          Ingawa CCM wameendelea kujikaza na kuona kama hili ni wingu la kupita, ukweli mambo ni tofauti. Na kama CCM wataendelea na dharau hizi watastuka wakiwa nje ya ulaji waanze kulaumiana. Tumeyashuhudia kama haya kule Malawi, Kenya, Zambia na kwingineko. Je wakati wa kaundika waraka wa mwisho kwa CCM umefika? Je kinachoendelea kutokea ni mwanzo wa mwisho wa CCM au mwanzo wa mwanzo wa upinzani kuchukua nchi?  Kwa vile waamuzi ni wananchi na wapiga kura, yetu macho japokuwa–kwa hali ilivyo–unaweza kutabiri kitakachotokea. Hata hivyo wahenga walisema; Hakuna marefu yasiyo na ncha na kila chenye mwanzo sharti kiwe na mwisho. Je ni mwanzo wa mwisho au mwisho wa mwanzo? Oktoba itatuambia.
Chanzo: Dira Agosti 27, 2015.

No comments: