The Chant of Savant

Tuesday 10 November 2015

Kijiwe chahoji baadhi ya mambo kwenye uapishaji


            Baada ya wazee wa Kijiwe kujialika kwenye sherehe za kuapishwa kwa rahis mpya Dk Kanywaji Makufuli na makamu wake Samie Sululu, kimekaa kama kamati kuhoji baadhi ya mambo ili kujua maisha ya viongozi wake wapya
            Tukiwa tunapata kahawa na kashata anaingia Mgosi Machungi akiwa na gazeti la leo. Anaamkua na kusema, “Vipi wazee na uchovu wa jana kushuhudia kuapishwa kwa waaji wenu wapya?”
            Mpemba anamjibu, “Hata nawe hawa walaji wako sawa nasi.”
            Mgosi anajibu huku akijiweka vizuri kwenye fomu, “Mpemba tiheshimiane. Unaona mimi ni mtu wa kuiwa kama wadanganyika?”
            Mpemba anajibu, “Yakhe kwani we Nzanzibari au Ntanganyika?”
            Mgosi anajibu, “Mimi mtanzania sawa nawe. Anyway, haya tiyaache.”
            Baada ya Kapende maongezi yanakwenda tenge, anaamua kuwanyang’anya mic na kusema, “Mwenzenu yote tisa, sikuona mantiki ya kumualika mchunaji wa Kinigeria Temitope Jushwa ambaye najua mhoteli wake uliua makumi ya watu kutokana utapeli na tamaa zake. Je huyu naye alialikwa kama nani au ni yale yale ya babu wa Loliondo?”
            “Usikumbushe huyu habithi wa Liloyondo aliyewatapeli na kuwaua wengi kwa miwaya?  Huoni walikuwa wakimsifia wanavyoanza kunyonyoka kama kuku aliyenyeshewa mvua?” anajibu Mipawa.
            Anakohoa na kuendelea, “Nadhani kuna kitu nyie hamkukipata. Hamjui wanasiasa, wachunaji na waganga wa kienyeji lao moja? Sikushangaa kumuona huyu mchunaji wa kinigeria akishiriki sherehe zetu. Nikikumbuka alivyondangaya Joisi Banda kuwa angechaguliwa rahis wa Malawi sina hamu na tapeli huyu.”
            Mzee Maneno anauliza, “Je huyu mnigeria alikuja kama nani wakati si mwanasiasa?  Au tunataka kuungana na Nigeria? Maana Njaa Kaya na Nkapa walikuwa mfukoni mwa Dongote na Kanywaji sasa na Jushwa!  Sijui huyu naye kama uwekezaji wake una tija au ni uchukuaji ule ule. Dongote amewekeza kwenye saruji. Huyu nadhani atawekeza kwenye kondoo wa Bwana.”
 Mijjinga anakula mic, “Usishangae kesho ukaambiwa huyu msanii mchunaji wa kinigeria kesho anawekeza kwa kufungua bonge ya kanisa au uwanja wa kutendea miujiza. Umesahau kuwa Danganyika ni shamba la bibi? Kwanini hwajiamini au kumwamimi Mungu? Kwanini kama ni kuomba wasijiombee wakati wana akili sauti na mawazo? Aibu tena yam waka!”
            Kapende anachomekea, “Wenzangu sijui macho yangu, maana kwenye kuapishwa Makufuli akina Luwassa na wenzake wa UKAUA sikuwaona au waligwaya baada ya kujidanganya kuwa tungewaamini pamoja na usanii na ufisadi wao?
Mbwamwitu anajibu, “Wawepo kufanya nini wakati walitulazimisha kuchagua chata la mafisadi wale wale tokana na upogo uroho na ujinga wao? Wangeweka wapi nyuso zao wakati ni wasaliti watupu? Mie naona lao na CcM ni moja tu wanatufanyia usanii huku wakipeana mishiko nyuma ya pazia.”
            Kabla ya kuendelea Mgosi anapoka mic, “Hebu Mpemba tisaidiene. Hivi hawa CcM kualika madikteta wengi kiasi hiki walimaanisha nini au nao wanapaga kutifanyie hivyo?”
             Mpemba anajibu “Yakhe mie wallahi sioni tofauti baina ya uimla wa chama na watu binafsi.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic, “Hao mnaowaita madikteta si kazi yenu bali wanakaya wao. Kwanini mnapenda kuingilia mambo ya wengine wakati yenu yanawashinda?”Awe na mume au asiwe naye yakuhusu nini wewe au umbea tu? Mbona nyinyi hamji na wake zenu hapa?”
            Mbwa mwitu anakula mic, “Da Sofi acha nikuchomekee. Hujui kuwa mambo mengine kuyafikiria achia mbali kuyasema yanahitaji kichaa cha aina yake?”
            Mheshimiwa Bwege anakula mic, “Kwani nani anaweza kuwa rahis Afrika bila kuwa dikteta hata kwa mlango wa nyuma? Unapokuwa juu ya katiba unategeme uwe nani kama si dikteta? Unapotawala miaka karne hata kama ni chama unategemea uwe nini kama si dikteta? Warabu wa Pemba ati.”
            Mijjinga anarejea “Mwenzenu naona kama tumetua mzigo huu uliokuwepo ingawa hata huyu anayekuja hatujui kama atakuwa nyenzo au mzigo ule kama huu ulioondoka na walaji wenzake. Nangoja kusikia atakavyofumia mikataba ya uchukuaji aliyoinga Tunituni na huyu msanii aliyekitoa. Nenda mwana kwenda na utokomee na ahadi zako za uongo. Mambo kwa Makufuli, halo halo!” anapiga ung’ende Mheshimiwa Bwege huku akinyoosha kidole juu kama wacheza mdundiko.
            Mwenzenu mie huenda mshamba. Huu uchafuaji wa mazingira wa kulipua mizinga mliuonaje?”
            Msomi anajibu, “Unashangaa kulipua mizinga? Huu ni urithi na muigizo toka kwa wakoloni waliotutawala na kutuachia makando kando ya ukoloni. Huoni hata hawa wetu hukaa kwenye nyumba ile ile yaliyokuwa makao makuu ya mkoloni mwenyewe? Unategemea nini kuwa na viongozi wanaotoa ahadi wazitekeleze au kushiriki ufisadi wazi wazi tukaendelea kuwagwaya na kuwapa kiburi badala ya kuwafikisha mahakamani? Mie namngojea bwana Kanywaji kuona hawa waliomtangulia atawatia adabu namna gani. hapa lazima wote kuanzia awamu pili hadi hii iliyokwisha lazima wawe na appointment na pilato tu kama kweli jamaa anataka kung’oa mzizi wa fitina na ufisadi.”
            Kanji aliyekuwa akiongea na mkewe kule Bombei anaamua kutia guu, “Veve Somi ongea kama toto dogo siyo. Veve nazani vatu ya chama moja naweza fungana? Hii Kufuli na ile nasema veve yote koo moja. Kama nafunga hii natangulia naye tafungwa na ile nafuata. Yote hii siasa dugu yangu. Najua vengi goja timiza promise natoa. Ohoo! Nenda lia sana sana dugu yangu. Hapana jua samaki yote iko na surubu?”
Chanzo: Tanzania Daima Nov., 11, 2015.

No comments: