The Chant of Savant

Tuesday 1 December 2015

Kijiwe chajivunia uanachama wa Majaaliwa

Kijiwe kimierauka leo. Leo wanakijiwe tuna furaha ya kufa mtu. Baada ya kukaa na waziri mkubwa bwana Katelephone na kumpa majina ya majambazi wa Bandarini naye –bila kulaza dam akawawashia moto, kwanini tusishangilia hasa ikizingatiwa kuwa wanaohomola wanaiba mali yetu wenyewe?
Mgosi Machungi analianzisha, “Kwei nimekubai bwana mdogo Kateephone kwa aivoshughuikia taifa tiizompa.” Anachomoa gazeti la Sasa Ngoma na kuonyesha picha ya mshirika wetu Katelephone akitema cheche kwa uchungu baada ya kufanyia kazi taarifa zetu.
Mijjinga anakula mic, “Walisahau kuwa mzee mzima natia mzigo Bandari bila kuiba wala kudokoa. Ngoja sasa nipange kumpa inshu ya jamaa wa TrA wanaoshirikiana na jamaa hawa wa bandarini pamoja na wafanyabiashara wanaochezea uchumi wetu wasijue Makufuli ameamua kutia kufuli kwenye ujambazi mbuzi dhidi ya kaya.”
Kanji anadakia mic, “Veve uza gahawa mwagia Jinga gahawa hadi kufa yeye.”
Kabla ya kuendelea, Mijjinga anamtahadhalisha, “Kanji tuheshimiane. Kama jinga basi mama yako. Mimi naitwa Mijjinga na jina langu halina uhusiano na Kiswahili wala lugha nyingine zaidi ya kisukusi. Tumeelewana au unataka nikupe zaidi?”
Huku akichekacheka Kanji anajitetea, “Hapana sema ile jinga jinga. Mimi sema jinga ya moto ile Kufuli na Jaliwa natumia choma fisadi yote nini bwana.”
Kapende aliyekuwa akisikiliza anaamua kula mic, “Kaka Mijjinga wewe umemaliza. Kwa vile nami niko TRA lazima niwataje vigogog wote wanaokula na wafanyabiashara majambazi. Nadhani hiki kilichofichuliwa ni cha mtoto. Bado kuna mazabe kibao tena mengi yakiwahusisha wezi wanaojidai kuwa mabilionea wakati ni wezi na matapeli wa kawaida. Nyie ngojeni Katelephone arejee au nitakapokwenda kumsalimia mtajionea mambo.”
Msomi Mkatatamaa anakula mic, “Msemayo ni kweli. Hiki ni cha mtoto. Nani angeamini kuwa kaya inayozalisha tanzanite inazidiwa na Kenya na India kwenye uuzaji wa mali hii aghali duniani wakati kaya yetu ikiendelea kubomubomu. Nina mpango wa kukuatana dokta mwenzangu Kanywaji na kumwambia kuwa sasa kaya yetu kuombaomba mwisho. Hapa lazima wezi wengine walioko uwanja wa ndege wa mzee Mchonga, Horohoro, Namanga, Kabanga, Tunduma, Kasumbalesa, Mutukula, Tanga kwenye matanki ya mafuta, TPDC, BoT, Mambo ya ndani, Jiji la Dar, Mizani yote, mahakama na kwingineko tuwachome. Kwanini watu binafsi wawe na njuluku kuliko lisirikali wakati wanazipata kwa kuliibia lisirikali. Nadhani zama za usanii na ubangaizaji za Njaa Kaya zimeishapita. Lazima tutendeane haki kwa kutajana na kuumbuana.”
Mzee Maneno anakamua mic, “Msomi usemayo kweli. Na kwa vile Ka-telephone ni mtoto wa mjini na mshikaji wetu walaji wajianadae kuliwa. Bado jamaa zangu wa EPA, Richmonduli, Dowans, Escrow, SUKITA, UDA, Mwananchi Gold na wengine wakae mkao wa kuliwa na kupigwa kipara soon. Lazima anyolewe mtu hapa haki ya nani.
Mipawa aliyekuwa akisoma gazeti anampasia Mchunguliaji na kula mic, “Tunadhani hata wale walioua na kuuza NBC wanapaswa kushughulikiwa bila kusahau NGOs za bi wakubwa walioachia ulaji maana nao ni vibaka wa kawaida waliotumia ikulu kujineemesha.”
Mgosi anakamua mic tena, “Tinapendekeza hata wae waiostaafu kwenye mamuaka haya ya ulaji azima wachunguzwe ili kujua wana utajii kiasi gani. Pia maswahiba zao waiowateua watenguiwe uteuzi wao na kuchunguzwa. Maana timechoka kuwa shamba la chizi ati. Haiwezekani tiendee kuwa maskini wakati vibaka wachache wakitanua.”
Mzee Ndevu anakula mic, “Hapo mmlenga. Maana nasikia jamaa wana ukwasi wa kufa mtu. Hata hawa waliosimamishwa nasikia nao si bure wameiba vya kutosha.”
Mijjinga anaamua kutoa jibu, “Usemayo ni kweli mzee mwenzangu. Nashangaa kuona makalani tena waliomaliza darasa la saba na kumi na mbili wana mihekalu na miradi lukuki huku sisi na PhD zetu tunasota. Haiwezekani. Maana nawajua wengi ambao elimu zao ni za kughushi na wengine ni vihiyo kabisa wa darasa la kumi na mbili lakini wanatanua kama hawana akili nzuri. Nenda pale uwanja wa mzee Mchonga uone vijana wadogo wenye elimu kiduchu wanavyoruhusu bwibwi kupita na kufumua mizigo na kuzichanga kama hawana akili nzuri.”
“Yakhe wankumbusha vijana wa ntaani kwetu waniofanya kazi uhamiaji walivyo na njuluku. Wameuza pasipoti zetu na kupata utajiri wa haraka. Yumo mmoja afanya kazi koritini ana fedha kama hana akili nzuri japo yu karani mdogo tu,” analalamika Mpemba huku akitikisa kichwa.
Baada ya kupongeza hatua za Katelephone, Kijiwe kimepanga kushehekea siku ya uhuru kwa kufanya usafi kijiweni. Kinafanya hivyo kwa kuunga mkono juhudi za mheshimiwa Dk Kanywaji za kubana matumizi na kuweka vipaumbele vya maana badala ya wizi na upuuzi ulimbukeni na ushenzi wa kutumia hovyo njuluku za wachovu. Kijiwe kinauliza maswali muhimu: Ina maana kwa miaka yote hamsini tumekuwa tukipoteza mabilioni katika ushenzi tu? Je ni fedha kiasi gani zimeangamia kwenye upuuzi kama huu?
Eti mijitu ilikuwa ikichapisha kadi kwa fedha za serikali. Haina adabu wala aibu hii. Kimsingi, kinachokwamisha kaya yetu si umaskini wa kujaliwa na Mwenyezi Mungu bali vipaumbele vibovu, ubangaizaji, roho mbaya, ulimbukeni, ujuha na upumbavu.
kijiwe kikiwa kinanoga si nikapokea simu toka kwa Dk Kanywaji!
Chanzo: Tanzania Daima,  Dec.,1, 2015.

No comments: