The Chant of Savant

Sunday 27 December 2015

Wachungaji wachunaji wamulikwe


Bishop Sylivesiter GamanywaVIJIMAMBO: MCHUNGAJI MWAKASEGE ALIVYOTEMBELEA TANZANIA HOUSE ...             Wapo viongozi wa kiroho wenye uroho wanaowachuna kondoo wa Bwana badala ya kuwachunga. Baada ya serikali ya awamu ya tano kuanza kushughulikia ufisadi nchini, wapo wanaoona kuwa imejikita sana kwenye watumishi wa umma huku ikiwasahau au kuwafumbia jicho wengine ambao ni watumishi wa umma kutokana na nyadhifa zao hata kama hawapokei mshahara toka serikalini. Hawa si wengine bali viongozi wa umma hasa wa kiroho ambao wengi wao wanatia shaka hasa kutokana na aina ya maisha wanayoishi. Wapo tulioshuhudia wakijiingiza kwenye siasa wakati wa kampeni wakati ni kinyume cha sheria kwa kiongozi wa umma kushabikia baadhi ya chama au wanasiasa hasa ikizingatiwa kuwa anaowaongoza ni wa vyama tofauti.
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekana kumtolea ...            Kinachovutia sana ni kwamba viongozi wengi wa kiroho, kwanza, ni wa kujipachika vyeo vyao. Pili, viongozi hawa wengi wa kujipachika wametokea kuwa matajiri wa kutisha tena kwa muda mfupi tofauti na wale tuliowazoea waliotawazwa kwa kufuata taratibu zinazokubalika kidini na kisiasa.
             Wakati wa serikali ya awamu ya tano kuwamulika hawa watu kujua jinsi walivyopata utajiri wao hata ikizingatiwa kuwa ni binadamu wenye udhaifu sawa na wengine. Wanaweza kuwa wanashirikiana na mafisadi hata wezi katika ofisi za umma ukiachia mbali hata kuweza kuwa wanajihusisha na biashara haramu kama unga na kukwepa kodi.  Kwenye biashara ya umma hakuna cha kuaminiana. Lazima kila mtanzania amulikwe. Uzoefu umeonyesha kuwa kabla ya kutokea ugaidi wa Septemba 11 kuna mashirika mengi ya kidini yalikuwa yakishirikiana na magaidi jambo ambalo wengi hawakuwa wakilitegemea au kulijua. Hivyo, kutoaminiana hakumaanisha kudharauliana au vinginevyo bali kutenda haki kwa wote bila kujali hadhi wala kazi ya mtu. Sisi sote ni binadamu wadhaifu. Ndiyo maana viongozi wengi wa kiroho wamekuwa wakwasi wa kutisha jambo ambalo kidini ni uroho tu wa kawaida.
PAMOJA BLOG: Kesi ya Kakobe Aprili mwakani            Siyo kulilenga kundi moja la watu. Ukweli ni kwamba siku hizi hakuna biashara inayolipa kama uganga wa kienyeji na uchungaji. Baada ya biashara hii kulipa sana, wamezuka waganga wengi wa kienyeji wakitoa madai ya ajabu kama vile kutibu ukimwi na magonjwa mengine yasiyotibika huku wachungaji nao wakishindana na waganga wa kienyeji ambao wengi wanajiita madaktari wakati wengi wao hata hilo darasa la saba hawakumaliza. Hii nayo inapaswa kukomeshwa haraka sana. Wachungaji wengi wamekuwa wakitangaza kufanya miujiza jambo ambalo haliingii hata akilini. Wapo wanaohoji: Kama wanafanya miujiza si waende kwenye hospitali za umma zilizojazana wagonjwa na kuifanyia huko badala ya kuwatapeli na kuwaibia wananchi maskini na wajinga? Hawa nao ni wa kumulikwa kweli kweli kujua wanapataje utajiri wa haraka bila kushiriki jinai hata kama ni kwa kificho? Wangepaswa kutangaza mali zao sawa na viongozi wengine wa umma.       
Mwl Christopher Mwakasege mnamo tarehe 17-19 August 2012 anatarajia ...   Bahati nzuri sana rais John Pombe Magufuli si mgeni katika dini. Historia yake inaonyesha kuwa alianzia kule kabla ya kujing’atua na kwenda kwenye shule za kawaida. Hivyo, angalau ana welewa wa viongozi wa kidini wa kweli na wa uongo.  Haiwezekani tuwabane watumishi wa umma huku tukiwaacha viongozi wa umma ambao uhusisha wa kisiasa na kiroho. Hatuwezi kuwashughulikia wakwepa kodi wakati kuna kila dalili kuwa wanaweza kuwa na washirika wengine nje ya biashara kama ilivyo kwenye mamlaka za serikali. Japo hatusemi kuwa viongozi wote wa kiroho ima wanakwepa kodi au kutumia misamaha ya kodi kupitisha biashara yao binafsi, uzoefu unaonyesha kuwa kuna viongozi wengi wa kiroho waroho na wasio waaminifu wanaotumia upenyo wa misamaha ya kodi kujineemesha binafsi. Wanapaswa kutwambia huu ukwasi wa haraka wameupataje wakati wanahudumia watu maskini na wenye shida nyingi? Wapo wanaotumia uongozi wao wa kiroho kiroho kwa kuwarubuni na kuwaibia watumini maskini na wajinga chini ya kile tulichokitaja hapo juu cha kutenda miujiza wakati miujiza yenyewe si nyingine bali kuwatapeli waumini hawa waliokwisha kukata tamaa.
MCHUNGAJI ANTONY LUSEKELO (MZEE WA UPAKO) AKIRI KUKAMATWA NA MADAWA YA ...
            Matapeli wengine wa kiroho wameamua kwa makusudi kujiweka karibu na serikali kwa kisingizio cha kuiombea ima serikali au nchi. Taifa letu limeishaombewa sana. Kinachotakiwa kufanyika si kuombewa bali kutendewa haki kwa kuacha kuwanyonya watu wetu au kukwepa kodi. Biashara hii ya kujikomba kwa serikali imevuka mipaka kiasi cha matapeli wa kimataifa nao kutaka kutumia nafasi hii. Ni juzi juzi nilisoma sehemu kuwa kuna wachungaji wanataka kumoumbea rais Magufuli na Tanzania. Kichekesho ni kwamba wahusika hawa wanatoka Ghana na Nigeria wakishirikiana na wa kitanzania. Kama kuombea kungekuwa dili nadhani nchi ya kuombewa ni Nigeria zaidi ya Tanzania kutokana na kuhangaishwa na Boko Haramu.
            Hivyo tumshauri rais Magufuli kuwa makini asije kumbwa na kashfa kama ile iliyomkumba rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda aliyetapeliwa na mchunaji aitwaye TB Joshua kuwa angeshinda urais akaishia kubwagwa na kujilaumu kwa kusikiliza utapeli huu.
            Tumalizie kwa kusisitiza kuwa wigo wa kupambana na rushwa na wizi upanuliwe na kuwahusisha wale wote wanojiita kuwa viongozi wa umma ima kupitia siasa au dini. Utajiri wao uwekwe wazi ili waumini wao wajue aina ya watu wanaoshughulika nao. Hii inaweza kusaidia kuwakatisha tamaa wanaopanga kula kupitia mgongo wa dini kama ambavyo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu. 
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 27, 2015.

No comments: