The Chant of Savant

Thursday 7 January 2016

Serikali imulike makampuni ya simu


            Serikali ya awamu ya tano imeanza kuweka nchi kwenye mguu sawa baada ya kuanza kushughulikia ufisadi wa kutish na wa kunuka wa muda mrefu nchini. Bandari, Mamlaka ya Mapato, Hospitali ya taifa ya Muhimbili, na Reli wameishaonja joto ya juhudi hizi za makusudi. Hata hivyo, hizi zote ni taasisi za umma.  Hatujui kama serikali imeanza na taasisi za umma ili baadaye zifuatie za binafsi au ndiyo utakuwa mwisho wa opereshini. Japo hatuwezi kusema kuwa serikali imezisahau taasisi na makampuni binafsi –kutokana na ukubwa wa tatizo –si vibaya tukaipa tipu nyingine ili iweze kutumbua majipu mengine ambayo haijayashughulikia. Kwani taasisi hizi zinashirikiana katika mambo yote yawe mabaya au mazuri kwa taifa. Hivyo, si vibaya tukiikumbusha serikali kuzimulika taasisi na makampuni binafsi ili kuweka nchi kwenye mstari unaotakiwa kwa ajili ya maendeleo ya taifa na watu wake.  Hakuna watu wanawawachezea watanzania kama makampuni ya binafsi yakiwamo makampuni ya simu. Kwanza, yanawalangua watu wetu ikilinganishwa na nchi jirani. Sijawahi kupata jibu ni kwanini nikipiga simu Kenya au Uganda natozwa pesa kidogo ikilinganishwa na Tanzania. Pili, sijawahi kupata jibu kwanini ninapopiga kwenye nchi tajwa hapo juu naongea bila simu kukatika hadi mwisho wa maongezi tofauti na Tanzania ambapo simu inakatika mara kwa mara ili kukatwa tozo la kuuganishia mitandao na simu.
            Tatu, huwa sijapata jibu kwanini simu za Tanzania –hasa kwa tulio Amerika ya Kaskazini –kutopatikana sawa na nchi tajwa.  Baada ya kukumbwa na hayo matatizo hapo juu, nilifikia hitimisho kuwa kuna kitu si cha kawaida nchini.  Ajabu nikiangalia shughuli zinazofanyika nchini sioni cha maana zaidi ya kuandaa mashindano ya kuwalewesha watanzania huku wakitapeliwa.
            Taarifa za hivi karibuni kuwa serikali iliyapiga faini makampuni ya simu kwa kufanya biashara kitapeli ilinizindua kiasi cha kunilazimisha kuandika makala hii. Vyombo vya habari vilimkariri mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Dk Ally Simba akisema kuwa makampuni ya simu yalikuwa yakitumia ujumbe wa kitapeli na kiulaghai kwenye mitandao. Laiti TCRA ingekujua kuwa utapeli wa makampuni ya simu hauiishii utapeli wa ujumbe bali hata viwango wanavyotoza. Tunadhani hata mitambo mingi iliyofungwa Tanzania ni ya kizamani na isiyofaa kwa matumizi tena ikilinganishwa na nchi jirani. Kuna haja ya kuchunguza hili kwa makini.
            Pia kuna upande hatarishi wa makampuni ya simu kwa afya za watu wetu. Ni Afrika tu ambako minara ya mawasiliano inatumika. Nchi zilizoendelea hutumia setalaiti kuepuka kuathiri afya za watu wake. Afrika, bado inatumia minara tena iliyotapakaa na kujengwa hata kwenye makazi ya binadamu kama ule wa Kunduchi Mbuyuni, Chalinze na maeneo mengine. Ni bahati mbaya kuwa watu wanaoishi karibu na mitambo ile wanaumizwa kwa kansa bila kujua. Je wataalamu wetu waliojazana serikalini hawajui au ni ile hali kuwa wao si waathirika? Kama hawajui utaalamu wao ni wa nini? Ingawa kuna migongano baina ya watafiti wa magonjwa ya binadamu kuhusiana na kama minara inasababisha kansa na mangonjwa mengine hasa kwa akina mama na watoto, huwa sipati jibu ninapoangalia huku jinsi minara inavyowekwa mbali –pale wanapolazimika kuitumia –milimani mbali na makazi ya watu wakati kwa Afrika minara husika inajengwa kwenye makazi ya watu bila kuhofia madhara yanayoweza kutokana na kuwa na minara hii kwenye maeneo ya watu. Kuna haja ya wataalamu wetu kuchunguza bila upendeleo na kuja na majibu juu ya huu utata wa kuruhusu minara ya simu kujengwa kwenye makazi ya watu. Hata ukiachia mbali madhara yanayoweza kutokana na mionzi ya sumu, kuna upande wa pili. Minara mingi ya simu ni mkusanyiko wa vyuma. Je ikititokea mnara husika ukaanguka tutegemee nini kwa wakati wanaoishi karibu nao hasa ikizingatiwa kuwa mingi iko karibu na makazi ya watu?
            Kama minara husika ingekuwa salama –basi hata huku inakochimbuka –ingejengwa sawa na inavyojengwa huko nyumbani. Kuna haja ya serikali kuondosha minara ya simu kwenye makazi ya binadamu bila kungoja madhara makubwa ambayo yataigharimu serikali na watu wake. Pia kuna haja ya kuchunguza viwango vya tozo katika nchi jirani ndipo serikali itagundua madudu na wizi mwingi mkubwa wa makampuni ya simu. Mfano, kampuni ya Primus Canada inatoza dola ya Kikanada 1.298 kwa dakika nikipiga simu kenya wakati kwa Tanzania ninatozwa dola za Kikanada 2.376 wakati Uganda natozwa 1.452. Ukiangalia haraka haraka, Tanzania ndiyo aghali ikilinganishwa na nchi nyingine kwenye ukanda mmoja. Kwanini kama hakuna namna wawekezaji kwenye simu wanavyotulangua?
            Wakati serikali ikiyamulika makampuni ya simu, inapaswa kujimulika pia kuona kama inawatoza kodi kubwa kiasi cha kuwasababishia walaji kutwishwa mzigo au inazidiwa akili kama ilivyokuwa kwenye kashfa za ukwepaji kulipa kodi na ushuru bandarini na kwingineko. Lazima watu watendewe haki ili waweze kuendeleza nchi yao na kujenga mazingira mazuri ya kiuzalishaji na kiuchumi. 
Chanzo: Tanzania Daima, Januari6, 2016. 

No comments: