The Chant of Savant

Saturday 7 May 2016

Mlevi kuhamia mlima Kilimanjaro

            Furiko la juzi lililolipiga jiji la Bongolala limenifanya niichukie Bongo niliyoipenda kuliko hata bi Mkubwa. Mwenzenu naamua rasmi kubwaga manyanga. Si kwa sababu yoyote bali mafuriko ya mara kwa mara yanayoanza kuzoeleka kiasi cha kuwageuza wabongolalalanders samaki–kama siyo vyura-watu. Tofauti na samaki na vyura ni kwamba mafuriko yenyewe ni ya vinyesi vitupu kwenye karne ya 21. Nimechoka kuogelea kwenye vinyesi kila masika. Juzi nusu nitapike maini bure. Maana, baada ya furiko kuvamia niliona kila dizaini ya madudu haya. Niliona kila dizaini ya mapishi kuanzia ya kimakonde, Kigabacholi aka Kiabusii bin Kalu na mengine mengi. Kinachoitwa mafuriko si chochote bali kutapika kwa jiji lililojengwa hovyo hovyo huku likisheheni wanadamu tena bila mpangilio wowote. Ama kweli, hata hili nalo jipu tena kubwa tu.
            Ajabu ya maajabu, pamoja na jiji kuelea kwenye bahari ya vinyesi, kuna watu wanachimba visima tena kwa ajili ya maji ya kunywa! Licha ya mafuriko ya vinyesi, hakuna kinachonitisha kama haya maji ya visima. Kimsingi, haya si maji ya visima bali mavi ya visima if we truly face it. Unachimba kisima karibu na vyoo vya kibongo vyenye kutapika hovyo hovyo hata kabla ya kutapishwa halafu unasema unakunywa maji! Haya ni maji au mavi? Ulimwengu huu karne hii ya 21 ni aibu kuishi kama vyura. Hata vyura wana nafuu kwa vile hayo ndiyo majaaliwa yao. Hivyo, wapendwani wangu, ndugu zanguni, maaduini zanguni na yeyote, rasmi nawaageni tena kwa moyo mkunjufu. Nimeshindwa mie.
             Hata kama Bongo kuna inshu, vyangu, dili na maraha vya kumwaga, mwenzenu na ulevi huu siwezi kuwa tayari kuishia kuokotwa kwenye mikoko beach baada ya kuuchapa mma na kuzolewa na mafuriko ya mavi. Unategemea nini kwa mheshimiwa kama mimi anayelewa ulabu na si madaraka kama wale, kurejea usiku kwenye jiji lililojaa mitaro na mashimo wakati wa furiko hili kama siyo kurejesha namba kabla ya wakati? Nashangaa hata akina Makonda; badala ya kushupalia miundo mbinu wanafukuzana na ombaomba wakati nao ni wale wale. Hayo si mwake humu leo. Ngoja tuyaachie hapo japo message sent.
            Naona hilo furiko la kufa mtu; je msomaji wangu umenusurika au ndiyo unangoja kwenye tuta uopolewe? Hata big mwenyewe ameamua kutimkia Dom na kuwaachia zahama yenu; unadhani nchenzo? Washirika na washikaji zangu acha niwape nyuzi. Mwenzenu naamia kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro ili kuepuka hii gharika ya zama hizi. Heri nikapambane na akina Kimaro na Kimario kuliko mafuriko ya vinyesi. Sijui tunazamishwa kwa sababu ya kukirithi ufisadi na madhambi mengine kama watu kupenda ngono na kula maraha wakamsahau subhanna au ni balaa liitwalo Global Warming? Naona yule anatikisa kichwa. Kwani nisemayo nazua au ni kweli tena tupu?
            Na kama hali yenyewe ni hii hamnioni Bongo! Du kwanini kuishi kama samaki!  Tokana na kuizimikia Bongo tokana na mishemishe zangu zote kuwa pale, nilifikiri hata kwenda kuishi kwenye  Daraja la mzee Mchonga pale Feri. Je nalo ni imara? Linaaminika usawa huu ambapo kila mwizi anapiga dili? Kama hawa waliolijenga nasikia miskendo ya ulaji kibao, lenyewe litakuwa limepona.
            Hivyo ndugu zangu akina shimbonyi mmkae mkao wa kupokea mgeni mheshimiwa rais wa walevi. Ila chonde chonde yale mambo ya “Kimaro umekataa kuiba utakula mafi yako” msinifanyie nisije nyotoa mtu roho mchana kabla ya kumpiga zongo au vipi? Wala akina Kekue, Manka na Mashoo msipoteze muda wala kutegemea kupeleka nyumbani chasaka wa kuchuna. Vyumba kwangu vilishajaa; na bi mkubwa wangu ana sifa moja kubwa ambayo ni wivu wa kuua mtu. Pia mfahamu, bi mkubwa mwenyewe ni kiboko yenu toka Tanga. Si mnayajua mambo ya Tangaline?
            Turejee kwenye furiko la mwaka. Mitaro imeziba tokana na kurundikana mijengo iliyojengwa kigabachori ikiporomoka na kuua huku wezi wachache wa jiji wakipiga dili wasijue wanatengeza maafa mchana kweupe! Nani aliwaroga nyie mnaotumia mitumbo kufikiri badala ya vichwa?  Sasa tazama mnampoteza mtu muhimu katika jamii kiasi cha kuwapa ujiko akina Meku bure.   Lazima nihame piga ua. Siko tayari kuishi kwenye bahari ya vinyesi vitokavyo kwa jamaa zangu akina Kalu na Absii waliozoea kunonihino kwenye mifuko na kurusha nje kama vile iko kule Bombei. Kwa jamaa zangu akina Muriuki na Kariuki–si Mwiruki na Kairuki–hii kitu huita flying toilets. Nadhani jamaa zangu wa Uthiru, Kibera, Kanungaga, Kwa Njega na hata Kawangware pale jiji Nairoberry wanajua nisemacho. Nakuja Kilimanjaro wanayosema iko kwao na si Bongo. Na huu nchezo nitaukomesha nikifika. Maana bila kuukomesha utasikia kuwa daraja la Mchonga nalo liko kwao na si Bongo.  Sasa Bongo kama Bombei kwa vinyesi.  Veve fanya chezo na Bombei dugu yangu?
            Kwa vile sijazoea mbege na Dengelua na madude mengine mazito mazito kama uji lazima nijiandae kuyakabili haya masanga lau niweze kupata stimu tayari kuzoza hapa ugani kama kawa. Leo sisemi mengi. Acha niaende kukusanya umaskini tayari kuanza safari.
Chanzo: Nipashe.

No comments: