The Chant of Savant

Saturday 7 May 2016

Viongozi wa kiroho nao wataje mali zao


            Tangua aingie madarakani, rais John Pombe Magufuli amejizolea umaarufu kutokana na falsafa yake ya “kutumbua majibu” ikiandamana na kauli mbiu ya “Hapa kazi tu.” Wengi–hasa wanaotuhumiwa kufanya ufisadi, wizi, ubabaishaji hata uzembe–wameishaonja joto la Magufuli. Licha ya kutumbua majipu, Magufuli amejizolea sifa nyingine kama vile kutaja mali zake, kupunguza mshahara wake na kuuweka wazi tofauti na watangulizi wake ambao wengine hata hawakutaja mali zao wala mishahara yao ukiachia mbali kutoipunguza. Tungependa watumishi au viongozi wote wa umma wafanye hivyo ili kuongoza kwa mfano na kuondoa shaka juu ya vipato vyao.
             Leo tutaongelea umuhimu wa kingozi wa umma awe wa kisiasa au kiroho kutaja mali kama sehemu ya utekelezaji wa kanuni za maadili ya utumishi wa umma. Leo tutashauri viongozi wa kiroho wafuate mfano wa rais kwa kutangaza mali zao na namna walivyozipata ili kuwapima na kuwatathmini kama kweli ni viongozi wa kiroho au viongozi wa uroho. Tutatoa sababu zifuatazo:
            Mosi, viongozi wa kiroho, kwanza ni binadamu; pia ni viongozi wa umma sawa na wanasiasa. Hivyo, nao wanapaswa kutaja mali zao ili kuondoa shaka miongoni mwa umma wanaouongoza ukiachia mbali kuuonyesha umma sura na rangi zao halisi. Wasifanye hivyo kama sehemu ya utashi bali wajibu katika nchi inayoanza kujenga utamaduni wa kuwajibika na kutenda haki.
            Pili, ni muhimu kujua wanaingiza fedha kiasi gani ambapo wengine wameonyesha kuwa na ukwasi wa kutisha na kutia shaka kiasi cha kujenga imani kuwa wanaingiza fedha nyingi tu.  Tokana na ukwasi na aina za maisha ya baadhi ya viongozi wa kiroho, imefikia hata hatua ya kujengeka imani kuwa ima wapo wanaotumia majoho yao kuingiza biashara bila kulipa kodi au kutumiwa na wafanyabiashara kukwepa kodi tokana na kupewa misamaha tokana na huduma zao au hata kushiriki biashara ya mihadarati nyuma ya pazia. Je hiyo fedha inatokana na shughuli wanazofanya; au kuna shughuli nyingine nyuma ya pazia? Maana, inakuwa vigumu kuamini kuwa kiongozi wa kiroho anaweza kununua helkopta au kujenga hekalu wakati anaowaongoza ni maskini wa kawaida. Inashangaza zaidi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wanaotia shaka kwa kuwa wakwasi wanamhubiri kiongozi kama Yesu aliyejulikana kwa umaskini wake na kuchukia utajiri. Kwani haikuandikwa kuwa, “Ni heri ngamia kupita tundu la sindano kuliko tajiri kuuona ufalme wa Mungu?” Je viongozi wa kiroho matajiri kweli wanamhubiri au kumuuza Yesu? Wanapata wapi ithibati ya kutumikia mabwana wawili yaani Mungu na dunia (utajiri)? Wanadhani–kama Yesu angetaka kuwa tajiri angeshindwa–au aliacha kwa sababu za kuepuka dhambi? Hata hii hali ya kutia shaka iliyoanza kuzoeleka ya viongozi wa kiroho kutokea kuwa matajiri wa kutupwa ni jipya kwa Tanzania. Tulizoea kuona mapadri na maaskofu hasa wa kweli na si wa kujipachika wakiishi maisha ya kawaida isipokuwa bosi wao yaani Papa ndiye amekuwa na ukwasi siku zote lakini si viongozi wengine. Ghafla bin vu likaibuka tabaka la viongozi wafanyabiashara ya jina la Yesu kiasi cha kuwa matajiri. Lazima kutakuwa na namna si bure.
            Tatu, kwa vile uwajibikaji na ulipaji kodi ni wajibu wa kila mtanzania, tunaishauri serikali kuanza kuwachunguza viongozi wa kiroho sawa na inavyoshughulika na watanzania wengine kama vile wafanyabiashara na watumishi wengine wa umma. Najua hili litapokelewa kwa mikono miwili na viongozi wa kiroho wa kweli. Lakini linaweza kupingwa vikali na wale waroho. Hivyo, serikali itakapowamulika, tusisikie lugha za kuchanganya dini na siasa. Kama serikali  hii hii inapowasamehe kodi na kuingiza vitu bure au kwa kodi kidogo haiwi kuchanganya dini na siasa, basi na kuwachunguza kwa ajili ya maslahi ya taifa ni wajibu wa serikali na si kuchanganya dini na siasa wala kuingilia uhuru wa viongozi wa kiroho.
            Nne, ni lazima wanaowachangia viongozi wao wajue namna fedha zao zinavyotumika ili wajiridhishe kuwa fedha zao zinatumika kama zilivyodhamiriwa. Kama ningekuwa rais, ningeamuru hata taasisi za kiroho zifanyiwe ukaguzi wa mahesabu kila mwaka ili kuondoa shaka na ufisadi. Rejea tuhuma zilizosambaa huko Marekani ambapo baadhi ya maaskofu wa Kanisa Katoliki walifikia kutumia fedha ya sadaka kutunza vimada na kulipa fidia kwa wale waliowanajisi. Kwani Tanzania ni kisiwa? Hivyo, uwajibikaji lazima uwahusu watanzania wote bila ubaguzi wala visingizio vyovyote. Lazima mapato ya viongozi wa kiroho yafahamike ili wanaowahudumia wawajue na kuwapima.
            Japo si wote, wapo wengi waliotumia fursa ya misahama ya kodi kama fursa ya kujitajirisha wakati waumini wakiendelea kuwa maskini. Lazima tufikie mahali tuue utamaduni ambao umegeuza dini kuwa biashara ya kuwatajirisha wajanja wachache kwa kuwanyonya wengi tena maskini. Zama za kusamehe kodi taasisi za kidini zimepitwa na wakati. Kwani, kuna aliyewatuma waanzishe huduma hizo?
            Tumalize kwa kumtaka rais Magufuli aanzishe utaratibu wa kuwajibisha watanzania wote hasa viongozi wa umma bila kujali ni wa kidini au kiserikali.
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: