The Chant of Savant

Wednesday 8 June 2016

Kijiwe chamshangaa Tuliya

            Baada ya kushuhudia ubabe wa kizamani uliotokea Mjengoni ambako wawakilishi wa wachovu walitolewa mkuku–kisa kudai haki za watoto wao walioingizwa mjini na watu wenye tamaa–Kijiwe leo kinakaa kulaani ubabe na ubazazi huu uliotembezwa na muishiwa mmoja tena asiyemwakilisha yeyote zaidi ya yule aliyempa ulaji. Tunawaunga mkono kwa dhati wahishimiwa wa upingaji walioamua kumsusa. Kwani matendo yake yananuka kiasi cha kumfanya awe jipu linalonuka hakuna mfano.
            Mijjinga anaingia akiwa na gazeti la Danganyika Daima. Analibwaga mezani huku akijifuta kijasho tokana na kusulubiwa na kijua cha asubuhi na moshi wa ngwalangwala zilizojazana kwenye barabara za Dar si Salama. Mchunguliaji analinyaka na kuanza kulidurusu.
            Anakohoa kidogo na kuronga, “Wazee mmemsikia huyu baby dogo wa Mjengoni aliyewatimua wawakilishi wa upingaji kwa sababu ya kutimiza wajibu wao? Je tumeondoa Makidamakida na kuleta asiyeTulia kuendeleza mchezo ule ule wa kubeba chama cha Mafwisadi?  Nataka leo tupitishe azimio la kumtokea na kumtia adabu ili aache utukutu kwenye mjengo mtukufu.”
            “We ulidhani kulikuwa na mabadiliko mjengoni usawa huu chini ya Jobless Nduguy aliyekuwa naibu wa Makidamakida akishiriki kikikombe kimoja? Naona afya ya Nduguy imekuwa ugogoro kiasi cha kuachia kila kitu kwa huyu dogo asiyeTulia. Ubaya ni kwamba hawatutangazie kuwa jamaa anauma utadhani kuumwa siyo sifa ya ngurumbili!” anajibu Kapende kwa kuulizwa swali.
            Mpemba anakula mic, “Yakhe hata mie wala sioni hayo mabadiliko wallahi. Kama yapo ni ya kuwa na rahis Kanywaji lakini si zaidi ya hapo. Naya anaanza kunshangaza kuvumilia majipu kama haya. Huyu bibie asipotulia atajatumbuliwa aambue kujilaumu kama yule Kitwangaji alotwanga mma akaishia kutwanga karata na mapema hata kabla hajafaidi. Anshangaza sana kukataa kutambua kuwa vihiyo waloingizwa vyuoni walitapeliwa; hivo kuwafukuza bila kuwashughulikia walowatapeli na kuongeza adha wallahi.”
            Mipawa anakamua mic, “Kweli kaya yetu imekula hasara hasa Mjengoni. Watu wanakuja na hoja za haja halafu gendaeka mmoja anawanyima fursa kana kwamba mjengo ni mali yake. Nani alidhani baby huyu anayedaiwa mbukuzi angefanya mambo kama kihiyo Anae Makidamakida? Ama kweli kambale wote wana sharubu; na ukishangaa na Makidamakida utaona ya Tulie! Alipoteuliwa na kuchaguliwa tukaambiwa ni daktari mwenzetu, tulikosea kudhani ataleta mapinduzi tusijue naye kidampa tu kama waliomtangulia anayetumika kinepi.”
            Mgosi Machungi anakula mic, “Sisi tiisema mkadhani ni unazi. Kusema ue ukwei, mimi sitegemei chochote toka nambai wani. Hawa jamaa ni majipu mbee na nyuma. Mimi sishangai kuona msomi huyu akifanya madudu; kwani hii ni jadi yao. Hata tofauti na vihiyo waiokuwa wameingizwa vyuoni wakati ni divisheni fei. Hukuona wasomi kama akina J4 Majembe na Shukuuni Kawa-dog waivyoua eimu wakati tiiambiwa wameeimika? Huyu wa Tuia anaweza kuwa na jipya gani wakati ni wae wae waiopata eimu kwa mazabe?”
            Mbwamwitu anakwanyua mic, “Huenda naye baby hasa ikizingatiwa kuwa hakuingia kwenye debe kupata huo uishiwa wake anaoutumia vibaya asijue una mwisho. Ni suala la kawaida kwa waliopata ulaji bila kura ya kula kujiona wao ndiyo wao wakati si chochote si lolote. Najua naye anaogelea kwenye mwamba. Siku atakapopiga mbizi kwishnei kazi yake. Yuko wapi Makidamakida aliyecheza makida akatembeza undava akaishia kukitoa kama Ben Makapi mzee wa nyodo? Nimependa ya wapingaji kuamua kumsusia upuuzi wake. Laiti magamba yasingekuwa na tabia ya kulindana, huyu bibie angetolewa mkuku tena haraka sana.”
            Msomi Mkatatamaa anatia guu, “Hata mimi nashangaa daktari mwenzetu kufanya mambo kama kihiyo; au naye kihiyo aliyefika hapo kwa kubebwabebwa? Haiwezekani mtu aliyesomea sharia akaivunja na kushindwa kuielewa. Sijui kwanini hakutaka kujua kuwa wahishimiwa wapingaji si watoto wake wala washikaji zake akaepuka kujivua nguo. Nadhani huyu naye anapaswa kuchunguzwa alivyopata nondo yake. Huyu ni jipu tena linalonuka. Anatutia aibu sisi wenye PhD za ukweli kusema ule ukweli. I don’t get it how an educated person of this caliber would commit such buffoonery. If she doesn’t change, I’ll lunge her one day.”
            Mzee Maneno anakula mic, “Msomi umechukia hadi kuongea kikameruni kigumu na kuniacha nje ya mjadala. Wakati mwingine tafadhali usichukie na kuangusha kimombo kigumu hivi. Sasa hiyo bafuni inaingiaje mjengoni au bi mkubwa alitoka bafuni ndiyo akawatimua wapingaji?
            Kijiwe hakina mbavu kwa namna mzee Maneno alivyopotea maboya tokana na kutokimanya kimombo.
            Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic, “Huyu mwananke mwenzetu ametuaibisha kuliko hata aliyemtangulia aliyesahau kuwa u-microphone ilikuwa ni wadhifa wa muda tu. Juzi nimeona dokta Kanywaji kamtoa kwenye mawe kwa kumpa ulaji. Hapa ndipo nakubaliana aliyesema kuwa kambale wote wana sharubu. Kwa alivyovurunda, nani alitegemea angepewa wadhifa wowote kwenye ofisi ya umma? Hapa ndipo nashindwa kumuelewa dokta Kanywaji. Kwani huyu mdada naye ni jipu sawa na huyu anayepaswa kutulizwa akaTulia na usomi wake uchwara.”
            Kapende anarejea, “Juzi mmemsikia Dokta Kanywaji akimuita mwenzie jipu akisema kuwa alimuachia kila kitu hewa? Sijui kwanini hamtumbui hasa ikizingatiwa kuwa yeye ndiye alikuwa mwanzilishi na muhimili wa uchafu huu unaotuhangaisha wachovu? Ukimuona jamaa anavyokenua utadhani kavaa nguo wakati yuko uchi.”
            Kanji anakula mic, “Hii toto naona naleta toto kwa Jengoni. Kama wakilishi ya chovu nasema yeye napaswa sikiliza na ongoza jadala. Sasa kama nataka kila hesimiwa sema yeye nataka basi andika kwa karatasini iwape bunge iseme hiyo nataka sikia ifurahise yeye.”
            Kijiwe kilipokuwa ndiyo chanoga si likapita shumbwengu la Tulie. Acha tulitoe mkuku ili kumtuliza kabla hajatumbuliwa.
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: