The Chant of Savant

Thursday 4 August 2016

Kijiwe chalaani Mrema kudhalilisha wanawake

 
Baada ya Agust Lyatongolwa Mremavu kuwadhalilisha wanawake akiwamo washirika wa bedroom wa wazee wa Kijiwe, tumeamua kulaani uchumia tumbo na udhalilishaji huu kwa herufi kubwa. 
Sofia Lion aka Kanungaembe ndiye anayeangusha mada leo. Akiwa amechukia kweli kweli anakula mic, “Jamani mmemsikia huyu njaa kali Mremavu alivyotudhalilisha wanawake wote tena akianza na bi mkubwa wake? Sijui mnashauri tumfanye nini gendaeka huyu mwenye uchu wa fisi mwenye kuweza kujivua nguo hadharani bila hata chembe ya aibu?” 
Mbwamwitu anamchomekea Sofia, “Twende tukamfanyia kitu mbaya na kuhakikisha uteuzi wake unatenguliwa huku naye akitumbuliwa jipu lake la muda mrefu. Huu si wakati wa kuhongana ulaji kwa vile waramba makalio wanamwaga na kuimba sifa kwa munene.” 
Mipawa naye hataki kuachwa nyuma. Anakula mic, “Jamani njaa nyingine bwana, yaani baba zima linajivua nguo hadharani hata kwa kumtusi mama yake mzazi bila chembe ya aibu wala utu ili lipewe tonge na watu wazima wanalinyamazia ukiachia mbali kulishangilia! Huyu hawezi kuwa mpinzani wala kiongozi wa kweli bali msakatonge wa kawaida tu; anayepaswa kuogopwa kama ukoma.” 
Mpemba naye anaangusha hoja, “Yakhe mie hata sikuamini masikio yangu wallahi. Nilisikia ankata kiasi cha kutaka niende ninsake na kuntia adabu mjalaana huyu wallahi. Ajabu ya maajabu, hata hao wanawake waloshuhudia na kusikia mauzauza haya tena vigogo kama dada yangu Sulhu hawakuchukia wala kukemea. Hii, kwao, ni ajabu na aibu. Jamani twendaapi? Ukisikia kuliwa wajiona asemako siku zote Mbwamwitu ndo huku.” 
Mzee Maneno anakula mic, “We unaongelea kukemea wakati walikuwa wakikenua utadhani walikuwa wamemwagiwa sifa. Hata hivyo, tuwe wakweli. Kama wanaume wenyewe tena marahis walinywea na kushabikia jinai hii, ulitegemea wanawake wafanye nini zaidi ya kujiunga na mkumbo wa udhalilishaji? Hivi hamjagundua kuwa katika kaya yetu siku hizi msemaji ni mmoja tu yaani Dokta Kanywaji ambaye watani zake wanaanza kumwita imla? Kama hamjui, kudhalilishana ni sera ya jamaa hawa ambao ukipingana nao lazima wakudhalilishe kama walivyomtumia huyu Mremavu njaa kali ambaye hana tofauti na Don Trump wa kwa Joji Kichaka.” 
Msomi Mkatatamaa naye anakula mic mapema, “Mie sikushangaa na wala sishangai hasa nikizingatia kuwa Mremavu–kwa tunaomjua–hana sifa hata chembe hata ya kuwa mjumbe wa nyumba kumikumi achilia mbali nafasi aliyozawadiwa kwa kujivua nguo na kujikomba.” 
Anaweka simu yake mezani na kuendelea, “Hakuna kilichoniacha hoi kama jamaa huyu kuhoji urume wa wenzake wakati yeye kishawekwa rumenya na Chama Cha Magamba (CCM). Kusema ukweli, hakuna niliyemshangaa na ambaye nitaendelea kumshangaa si mwingine bali daktari mwenzangu Kanywaji aliyeingizwa mkenge na msakatonge huyu kama alivyomeuelezea vizuri Ami pale. Rahis alipaswa kusema wazi wazi kuwa maneno ya Mremavu si msimamo wake, serikali yake wala chama chake. Hata MC wa mkutano ule anaonekana kuwa kilaza ambaye anapaswa kutumbuliwa. Alishindwa nini kusema kuwa maoni ya Mremavu ni yake binafsi hata kwa kuchomekea au kuchombeza?” 
Kanji anamchomekea Msomi, “Somi vacha mimi chomekee veve leo dugu yangu. Mimi hapana shangaa. Kama Jaa Kaya napeleka yeye Bombei tibiwa zani iko veza sema baya chama ile? Swahili iko sema adui yako veve ombea jaa. Hii Rema ongea kwa tumboni badala ya bongo. Veve sikiliza yeye taona point mimi nasema.” 
Mipawa anakatua mic, “Jamani wala mshingae.  Kwani hamkujua kuwa sera ya jamaa wa nambari wani ni kudhalilisha wanawake na vijana ambao siku hizi Dokta Kanywaji ameanza kuwakumbuka? Angalia hizo jumuia zao zinavyotumiwa kuwafunga kamba kuwa nao wamo wakati wanatumiwa kupitisha warume wahomole kwenye ulaji wa juu. Hivyo, usitegemee wanawake wajitete wakati wameishaona kama udhalilishaji ni sehemu ya maisha kama ilivyo ufisadi.” 
“Pamoja na kwamba hakuwadhalilisha washirika zetu wa bedroom, msimsahau mzee Mapesa wa zamani aliyeishia kufilisika kulhali baada ya CCM kumpeleka Ugabacholini kutibiwa kiasi cha kujitoa mwili na roho kama alivyoonyesha kwa maneno yake mwenyewe. Naye alisarura kweli kweli japo kwa kituo. Tofauti ya wawili hawa ni kwamba mmoja alitetea njaa yake bila kuwatukana wala kuwadhalilisha wengine.” Anachomekea Kapende huku akibwia kahawa yake. 
Mgosi Machungi aliyekuwa kimya muda mrefu anakula mic, “Huyu meku ana laana ya mama yake. Hamkusikia aivyomvua mama yake nguo akisema eti aikuwa akizia hovyo hovyo? Hamkuona aivyojivua nguo kwa kuamba matapishi yake akiisifia magamba kwa vile aipewa ulaji wa dezo hivi karibuni ukiachia mbai kupeekwa ugabachoini kutibiwa? Ashindwe na aendee kunyong’onyea. Anadhani njaa yake itaisha kwa nafasi aiyopewa? Ikiisha sijui atafanya nini wakati ameamua kujiacha uchi bia kujua kuna kesho?” 
Anapiga chafya na kuendelea, “Kwa mia zetu wagosi, mwanaume huwa hawezi kumsifia mwanaume mwenzie isipokuwa mwanamke na mwanamke kadhaika tokana na sababu za kimaumbie. Ajabu huyu Muemavu alihoji uanaume wa wenzie wakati yeye aikua akitoa mipasho na sifa za kike. Ama kwei nyani haoni kundue!” 

Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita Lyatongolwa! Acha tummwagie kahawa!
Chanzo: Tanzania Jumatano.

No comments: