The Chant of Savant

Friday 12 August 2016

Ujaji tusitangaze ajira bali kutumbua hata waliopo


 
            Hivi karibuni mahakama imetangaza kuwa sasa kazi za ujaji zitakuwa zikiombwa kama kazi nyingine ili kuepuka kuendelea na mfumo na utamaduni wa kizamani ambao ulijaza majaji vihiyo na wenye mafungamano kisiasa kiasi cha kuinyima mahakama hadhi inayopaswa kuwa nayo kama taasisi ya umma na mhilimi mmojawapo wa dola.
Kwanza, tunapongeza hatua hii ambayo bila shaka italeta mapinduzi na maendeleo makubwa katika utoaji haki nchini.
Pili, tungeshauri hata upatikanaji wa jaji mkuu utumie utaratibu huu kama ilivyo nchini Kenya na Afrika Kusini. Kwanini rais apatikane kwa uchaguzi lakini jaji mkuu apatikane kwa uteuzi?
Tatu, tunashauri mahakama isianzie hapa; bali irudi nyuma na kuhakikisha majaji vihiyo na wenye kutumiwa kisiasa au kwa namna yoyote wanaondolewa ofisini ili kutenda haki na haki ikaonekana inatendeka. Kwani, wa vihiyo ambao sifa zao hazilingani na kazi na mamlaka waliyopewa.
Nne, wa majaji wanaojulikana kuwa uteuzi wao licha ya kutia shaka na kudhalilisha mahakama na mamlaka zilizofanya uteuzi huu na taifa kwa ujumla, unajulikana ulivyosukumwa na kujuana kwao na mamlaka zilizowateua.
Tano, wapo majaji ambao kuna ushahidi kuwa walishiriki vitendo vya kukiuka maadili, hivyo, kutofaa kuteuliwa kuwa majaji ingawa waliteuliwa kutokana na utawala mbovu uliopita kuangalia maslahi binafsi badala ya taifa.
Kwa wale wanaotaka kubaini majaji vihiyo na mabomu wanaopaswa kutumbuliwa kwa kuachishwa ujaji, warejee malalamiko yaliyowahi kutolewa na mwanasheria maarufu Tundu Lissu tena bungeni akidai kuwa baadhi ya majaji hawakuwa na sifa wala hawakupaswa kuteuliwa kwenye nafasi hizo hasa baada ya kubainika kutenda vitendo vinavyokiuka maadili kama vile rushwa na madhambi mengine. Kwa mujibu wa gazeti la Tanzania Daima la Novemba 29, 2012, ulimkariri Lissu akisema, “Nilieleza jinsi rais alivyofanya uteuzi wa baadhi ya majaji pasipo kupata ushauri wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Wamekuwa wakijibu kiujumla, mimi niliwataja kwa majina yao na hata hili nilieleza katika Kamati ya Ngwilizi ambayo taarifa yake haikuwekwa hadharani pasipo sababu za kueleweka.”
 Lissu aliwataja majaji Mbaruku Salumu Mbaruku na Fatuma Masengi kama majaji waliteuliwa bila kuwa na sifa za kitaaluma kufanya kazi ya ujaji.
Wengine aliowataja Lissu ni majaji Latifa Mansoor anayedai alifukuzwa na manispaa ya Ilala kwa ubadhirifu na udanganyifu, Kassim Nyangarika aliyewahi kushinda kesi kutokana na urafiki wake na jaji na Zainab Muruke, Pelagia Khaday, Aloysius Mujulizi ambaye licha ya kutuhumiwa kupokea fedha ya Escrow inadaiwa alishiriki kuanzisha kampuni ya Deep Green Finance Co. Ltd iliyotuhumiwa kwa wizi mkubwa wa fedha za umma.
Je wapo majaji wengine ambao waliteuliwa na mamlaka za hovyo ambazo zilidharau au kutofuata vigezo zaidi ya kujuana au kusaidiana kama anavyodai Lissu kuwa kuna majaji waliteuliwa wakiwa wagonjwa mahututi ili waweze kusafirishwa nje kwa matibabu. Lissu anawataja hawa kuwa ni marehemu Jaji Kulwa Masaba na Jaji Madina Muro na majaji Stephen Ihema, Juxton Mlay, Augustine Shayo na Vincent Lyimo. Wengine ni Mwendwa Malecela ambaye hadi Lissu anatoa madai yake alikuwa hajawahi kutoa hukumu yoyote tokana na ugonjwa.
Madai ya Lissu yanazua maswali mengi kuliko majibu. Je inakuwaje mamlaka zinazopaswa kuheshimu na kutimiza sheria kama zilivyochaguliwa na kuapa kufanya vitu visivyoingia akilini mfano kuteua watu wasio na sifa kitaaluma au kusheria kuwa majaji? Je ni wangapi ambao hawajapigwa kurunzi? Je watu hawa wamelisababisha taifa na mahakama madhara makubwa kiasi gani? Je tuhuma za Lissu ni za uongo? Kama ni za uongo, kwanini hajawahi kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma? Kama tuhuma za Lissu ni za kweli–na kama zinavyoonyesha ni za kweli kutokana na kutokuwapo shauri mahakamani–watuhumiwa ambao hawajastaafu au kufariki wanangoja nini kwenye ofisi za umma wakati hawana sifa na wamepatikana kinyume cha sheria? Je hili nalo linangoja rais Dk John Pombe Magufuli au jaji mkuu–kama anasoma habari kama hizi–anaweza kuomba ushauri kwa rais na mamlaka nyingine husika na kuwawajibisha wahusika? Je watanzania wataendelea kuumizwa na watu wasio na sifa kwa kuwanyima haki hadi lini?
Leo hatutaandika mengi. Badala yake tunaomba tuishie hapa kwa kutaka watuhumiwa wote  wajiwajibishe au wawajibishwe mara moja ili kulinda na kurejesha imani na heshima ya mahakama; na wasipewe nafasi na kurejeshwa kazini kwa vile kazi ya ujaji inahitaji mtu asiyekabiliwa na tuhuma yeyote. Kama watahitaji kuheshimika kama raia na wana taaluma wengine ima waende mahakamani kujisafisha au wajiuzulu kabla ya kuwajbishwa. Kwani madai yanayowakabili–hata kama yalifutikwa chini ya busati kwa muda mrefu–ni mazito sana kwa ofisi ya jaji. Kwa habari zaidi wanaweza kutembelea kiunganishi hiki: http://sheriayako.blogspot.ca/2012/08/tundu-lissu-afichua-mengi-juu-ya-majaji.html
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano.

No comments: