The Chant of Savant

Monday 3 October 2016

Barua ya wazi kwa Hamad na Lipumba

 
          Waheshimiwa,
Naamini hamjambo na mnaendelea na shughuli zenu kama kawaida. Naandika barua hii kwa uchungu mkubwa kama mpenda mageuzi. Kilichonisukuma kuandika barua hii ni mambo yafuatayo:
            Mosi, mtafaruko ndani ya chama chenu cha Wananachi (CUF) unaoendesha kukidhoofisha chama na upinzani kwa ujumla. Najua siasa ni mchezo unaoweza kuwa mchafu kama utachezwa vibaya na kwa kutofuata kanuni.  Hivyo, nashauri msijiruhusu au kuruhusu huu mtafaruko kukimega, kukidhoofisha hata kukiua chama ambacho mmekijenga kwa muda mrefu. Kubomoa ni rahisi sana kuliko kujenga.
            Pili, nandika kutokana na kuanza kuona kuwa kuna kila dalili za kukiua chama tokana na ima maslahi binafsi ya wawili nyinyi au kutunisha misuli kila mmoja akiamini atashinda. Katika mchezo huu mnaoshabikia na kucheza hakuna mshindi; na kama yupo, basi si mwingine, bali maadui zenu ambao sasa wanachekelea na kushangilia kwa visu mnavyojidunga.
            Tatu, nikiangalia historia ya CUF nagundua; haijawahi kuwa na viongozi waandamizi zaidi ya nyinyi. Mmeshikilia nafasi za juu kiasi cha kugeuka kile kwa kiingereza huita fixtures au kitu kisichoaminishika. Hii ni kinyuma na demokrasia na matarajio ya umma. Kwa mfano, profesa Ibrahim Lipumba amekuwa mkiti wa CUF tangu mwaka 1995 yaani miaka 21 jambo ambalo linamfanya awe mwenyekiti wa chama kwa miongo zaidi ya minne. Aliingia madarakani na Benjamin Mkapa akahudumu kama mkiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka kumi akaondoka na kuja Jakaya Kikwete ambaye alihudumu miaka kumi akaondoka. Sasa mkiti mpya John Pombe Magufuli ndiyo yuko kwenye usukani.  Kwa upande wa maalimu Seif Sharrif Hamad, kadhalika aliingia kwenye uongozi wa juu wa CUF tangu mwaka 1992 akiwa mgombea pekee wa CUF kwenye nafasi ya urais wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar (BMZ). Alianza kugombea urais akipambana na Salmin Amour, kisha Amani Karume na juzi alipambana na Dk Ali Mohamed Shein. Na inavyoonekana, bado ana hamu ya kugombea na mwingine atakayemfuatia Shein anayemaliza muda wake mwaka 2020. Hii maana yake ni kwamba Hamad atakuwa amegombea mara nne mfululizo jambo ambalo linatia shaka udemokrasia wake.
            Nne, kwa kuangalia trajectory hii, unagundua kuwa kuna haja ya CUF kuanza kufikiria kile ambacho kwa kimombo huitwa post-Lipumba-and-Hamad era yaani kipindi ambacho kitakuwa kwenye mikono ya wengine. Hili ni Dhahiri na laweza kukisaidia chama hasa ikizingatiwa kuwa mliyoshindwa kuyafanya kwa miaka zaidi ya 20 mliyokuwa kwenye uongozi wa juu wa chama hamuwezi kuyafanya na kuyafanikisha hata mkipewa miaka 200 zaidi. Hivyo, si vibaya wala uchochezi kuwataka mfikiri kuachia ngazi ili damu mpya iingie na kujaribu kufanya mambo kwa namna tofauti mlivyofanya. Japo CCM imekuwa madarakani kwa miaka mingi tangia uhuru, inawazidi kitu kimoja. Imeweza kuruhusu watu wengine–tena ambao ni wageni chamani–kushika hatamu za uongozi ili kufanya mambo tofauti na wengine waliotangulia. Huu ndiyo ukomavu kidemokrasia. Kwani hakuna aliyeumbiwa kuongoza wala kuongozwa. Yeyote anaweza kuongoza sawa na kuongozwa.
            Tano, kama wanachama wenu bado wanawahitaji, jambo ambalo hata hivyo nina shaka nalo, basi suluhisheni ugomvi wenu ili mkinusuru chama pia nanyi binafsi. Kwani si jambo jema kuingia kwenye vitabu vya historia kama wawili walioua chama tokana na maslahi au uadui binafsi. Sidhani kama mna haja ya kutojifunza toka kwa wanasiasa kama akina Augustine Mrema na John Cheyo walioamua kuvigeuza vyama vyao mali binafsi kiasi cha kutoona wengine wa kuweza kuviongoza zaidi yao.
            Sita, kitu kingine kilichonisukuma kuandika barua hii ni ile hali ya kuona kuwa wanachama wenu, kwanza, hawana mamlaka tosha ya kuwawajibisha kwa pamoja. Na pili wanaonekana kuangukia kwenye mtego wenu wa kuwashabikia kiasi cha kugawanyika badala ya kuangalia chama kama asasi huru isiyopaswa kukwazwa na watu binafsi kama ilivyo kwa CUF kwa sasa. Sisikii wanaowakumbusha kufanya jambo la maana yaani kuachia ngazi ili chama kiendelee kama kinavyopaswa. Wote wamegawanyika pande mbili jambo ambalo linakinyima chama fursa na siha ya kusonga mbele hasa usawa huu serikali ya CCM inapofanya mambo mengi yanayowavutia watanzania. Sijui kwanini hamuoni tishio hili na badala yake mnakuwa waanzishaji wa mauti ya chama chenu. Ili iweje na kwa faida ya nani?
            Nahitimisha barua hii kwa kuwaomba kwa unyenyekevu mchague kati ya mawili yaani kusuluhusisha ugomvi na kusonga mbele au kuachia ngazi ili akili, damu na nguvu mpya ichukue hatamu na kukwamua chama kinachochungulia kaburi. Wapiganapo mafahari wawili ziumiazo ni nyasi (wanachama).
            Pia niwasihi wanachama kuachana na ushabiki wa kisiasa; na badala yake wapiganie mstakabali wa chama.
Nawatakieni kila la heri katika kujipima, kujisuta na kuchukua maamuzi magumu kwa faida ya demokrasia nchini. CUF ni zaidi ya Hamad na Lipumba.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili jana.

No comments: