The Chant of Savant

Saturday 19 November 2016

Je Tanzania inao wageni wanaohodhi ardhi wangapi?


 
            Hakuna ubishi. Chini ya utawala rais mstaafu Benjamin Mkapa, Tanzania ilipwakia uwekezaji bila maandalizi wala ujuzi wa kile ulichokuwa ukiingia. Mkapa atabaki kwenye vitabu vya historia ya Tanzania kama rais aliyeuza nchi kwa wawekezaji. Hili unaweza kuliona kwenye kashfa zilizohusisha uwekezaji zilizofumka wakati wa utawala wake. Jikumbushe iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) iliyouzwa kwa ABSA Group ya Afrika Kusini kwa bei ya kutupwa na kifisadi. Rejea mdororo wa Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) lililowekwa chini ya uendeshaji wa kampuni ya Afrika Kusini. Rejea kuuzwa kwa viwanda vingi vilivyoishia kuwa mabohari na vingine kunyofolowa vifaa hadi juzi tu rais John Magufuli alipoamuru wenye kuvifuja kuviendeleza kabla hajavitwaa.
            Kwa ufupi, uwekezaji chini ya Mkapa ulikuwa ni wa kijambazi na kifisadi uliotokana na rushwa ambao uliliingiza taifa kwenye mdororo wa kiuchumi jambo ambalo baadaye Mkapa alijutia. Alilwahi kukaririwa akisema “kwenye uongozi wangu kitu ambacho mpaka sasa ninajuitia ni kuanzisha sera ya ubinafsishaji na kushindwa kuweka mfumo au chombo cha kuudhibiti.”  Kwa kushindwa kuudhibiti uwekezaji, Mkapa alijenga tabia chafu ya kuabudia wageni ambao kwao wanasifika kuwabagua watu weusi.
            Mbali na Mkapa, utawala wa Jakaya Kikwete ndiyo ulivuruga kila kitu. Kwani, Kikwete alipokuwa akifanya kampeni, aliahidi kurekebisha mikataba ya uwekezaji. Hata hivyo, baada ya kuingia madarakani wala hakufanya hivyo. Badala yake alianzisha utawala wa hovyo ambao wengi waliuona kama uholela ambao uliiweka nchi kwenye autopilot kwa miaka yote kumi aliyokuwa madarakani akisifika kwa kuizunguka dunia akiandamana na marafiki na wapambe wasio na umuhimu kiasi cha kutunisha deni la taifa.
            Tukiacha na tawala zilizopita ambazo hazina lolote la maana kwa sasa, tuangalia hali ilivyo kwa sasa.
            Mosi, chini ya kivuli cha uwekezaji, kumekuwapo na tabia ya kuendekeza njaa kiasi cha maafisa wa serikali kugeuka makuwadi na vijakazi wa wawekezaji. Wamekuwa wakiwasaidia kukwepa kodi na kuingia mikataba ya kipumbavu kama mkataba wa TICTS ambao rais Magufuli alitaka ubadilishwe hivi karibuni badala ya kuubatilisha na kuwachukulia sheria walioingia mkataba huu wa hovyo.
            Pili, tumeendelea kuwa na mfumo mbovu wa udhibiti wa mali za umma. Mfano wa hivi karibuni ni kufutwa hati za umilki ardhi kwa Hamant Patel ambaye alighushi vyeti vya kuzaliwa na kujitwalia ardhi kinyume cha sheria. Je huyu Patel, hata kama angekuwa mtanzania wa kuzaliwa, aliruhusiwaje kuhodhi ardhi kila mahali? Je tunao patel wangapi walioodhi ardhi yetu na kuifanyia biashara huku wakiishi nje wakati hakuna mswahili anaweza kupata hata inchi moja huko watokako?
            Kumekuwapo na ukurupukaji katika kushughulia kadhia zinazotokana na uwekezaji na wizi mwingine wa mali na raslimali za umma. Mfano, tunaambiwa Patel amefutia hati. Je alikamatwa na kujibu tuhuma? Je waliomwezesha wamebainiwa, kukamatwa na kushughulikiwa?
            Nne, je nini kifanyike? Fanyeni ukaguzi mpya wa ardhi na raslimali zote ambazo majambazi wa kigeni wamezoea kuzitumia kukopea na kuishi ughaibuni kwa starehe. Ni bahati mbaya kuwa taifa letu lina tatizo la kusahau na kutojifunza kutokana na historia na makosa yake. Uozefu unaonyesha; hatukujifunza tokana na kashfa na hujuma ya Chavda aliyemilkishwa mashamba ya mkonge akaishia kuyatumia kujipatia mikopo na kutoroka nchi.
            Tano, tujibu maswali makuuu yafuatayo:
            Mosi, ilikuwaje huyu Patel hakuitwa na kukamatwa kwa makosa ya kujipatia ardhi na nyaraka kinyume cha sheria ili lau aonje joto ya jiwe na liwe somo kwa wahalifu wengine?  Bila kuwa na kuwaadhibu wahalifu waliokwishathibitika, tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu.
            Pili, je tunao majambazi kama hawa kiasi gani nchini wakichezea mali zetu wakati watu wetu wanaendelea kuangamia kwa ujinga na umaskini?
            Tatu, je ni nani hao waliompatia nyaraka na kumpa umilki wa ardhi? Haya ni maswali ambayo yalipaswa kujibiwa kabla ya kumstua mhalifu huyu. Je waliochukua hatua hii ya pupa na hasara kwa taifa hawakujua vitu rahisi kama hivi; au kuna namna kama siyo watu wasio na sifa na ujuzi kupewa nyadhifa nyeti kama hizi?
            Nne, je tutaendelea kuwa shamba la bibi hadi lini? Inashangaza kuona taifa lililojaliwa raslimali lukuki kuzidiwa hata na viinchi vidogo na visivyo na raslimali hata nusu yetu.
            Tano, je nini kifanyike? Kagueni hati zote za kuzaliwa za watanzania. Mchezo wa wageni hasa wahindi kuja kununua vyeti vya kuzaliwa nchini ukiachia mbali paspoti ni biashara inayojulikana kuwapo muda mrefu tena wakisaidiwa na watanzania wenzetu waroho umezidi kuzoeleka kiasi cha kuwa janga la kitaifa. Nadhani tunapaswa kupambana na genge hili na kulitokomeza kwa kuwafunga walioko nyuma yake vifungo vya maisha ili liwe somo kwa wengine.
            Sita, tungeni sheria kali ya kuhakikisha wanaokamatwa na mawakala wao wanafia gerezani. Bila kuwa na sheria kali za kupambana na jinai hii, hata hii amani tunayojivunia itatokea. Wananchi watakapojua kinachoendelea, watajichukulia sheria mkononi. Tumeishasikia wengi wakivamia mashamba na kujitwalia baada ya kugundua yalichukuliwa kifisadi.
Je namna hii twaweza kusonga mbele kiuchumi wakati ardhi na mali zetu zinatwaliwa na mahalifu wa kigeni na kuacha watu wetu wakiendelea kuteketea kwa umaskini? Je tunao akina Patel wangapi?
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: