The Chant of Savant

Thursday 29 December 2016

Akina Lusekelo wachunguzwe na “zawadi” zao

Image result for photos of anthony lusekelo
         Image result for photos of anthony lusekelo
Baada ya kukumbwa na kashfa ya kile kilichoripotiwa na vyombo vya habari kama ulevi na kuonyesha tabia mbaya, mchungaji Anthony Lusekelo ametoa mpya mbili za kufungia mwaka. Moja ni kuwaombea waandishi wa habari walioandika habari za kashfa yake wafe. Amesema kama hawatakufa ataacha kuhubiri akauze gongo. Sijui kwanini amechagua gongo na si nyanya au hata kuuza vitabu vya neno. Lusekelo ametoa hadi mwezi wa tatu mwakani jambo ambalo limeshangaza wengi. Kwani mtu wa kweli wa Mungu tena anayehubiri neno la Mungu asingekuwa mtu vitisho, kushabikia kifo wala kulipiza visasi kwa makosa aliyotenda kutokana na kutokuwa makini. Hivi Yesu anayehubiriwa na wachungaji aina ya Lusekelo angekuwa kama wao kweli kungekuwa na kanisa hata moja? Je Lusekelo tutamtofautishaje na wale manabii wa uongo aliotahadharisha Yesu kama mambo yake ni hivi? Je Lusekelo alitoa tishio hili ili kuwafanya waandishi wa habari wagwaye kuripoti uoza wake kama kiongozi wa kiroho anayepaswa kuwa kioo cha jamii? Kwa wale waliotishiwa maisha, wanapaswa kuripoti polisi ili lolote likiwatokea Lusekelo awajibishwe kisheria. Maana, hakuna anayejua atakavyowaua hasa katika dunia hii yenye watu rangi mbili. Isije mkatumiwa wauaji au kupewa hata sumu au kugongwa akaishia kujisifu kuwa alitabiri wakati kuna mkono wa mtu.  Nani alijua kuwa baadhi ya wachungaji wangesafirisha mihadarati au taasisi zao kukwepa kulipa kodi, kulipia umeme hata kutoa utabiri wa uongo na kufanya mambo ya kishirikina na kitapeli? Wangapi wako kwa pilato wakishitakiwa na waumini wao waliowatapeli au kuwanyonya na kuwaibia?
             Sasa kama anadhani wote wanaogopa kifo kana kwamba yeye ataishi milele, basi mie naandika tena kwa uchambuzi wa kina na afanye atakavyo. Sidhani kama Mungu ni wa hovyo kiasi hiki kiasi cha kila anayetaka kumtumia anamtumia utadhani ni bunduki yake. Mungu, tena wa kikristo, ni mwenye rehema na si Mungu wa visasi vinginevyo Lusekelo angetafuta mahali pengine pa kufanyia biashara zake. Mungu si mjinga kiasi cha kumlipizia kisasi mkosefu aliyejichafua akasingizia wenzake wanamchafua.
            Pili vyombo vya habari viliripoti kuwa Lusekelo, baada ya kukumbwa na kashfa ya ulevi, eti alipewa zawadi ya magari mawili mojawapo likiwa Toyota Land Cruiser yenye thamani ya shilingi za kitanzania milioni 200. Sijui kama kweli hawa wanaokuja na sanaa kama hizi wanajua ukubwa wa fedha wanayotaja. Je ni nani hao ambao Lusekelo hawataji waliompa zawadi kubwa hivyo? Je wana utajiri kiasi gani na wameupataje? Mbona maaskofu tena wa kweli kama mhashamu Polycarp Pengo au Shehe Mkuu hatusikii wakipewa zawadi kama hizo? Je serikali itaacha watu watengeneze fedha kiharamu na kuzitakatisha kwa njia rahisi kama hii? Je hawa watoaji wanafanya biashara gani na wanalipa kodi kiasi gani?
            Kuondoa utata, Lusekelo anapaswa kutaja majina ya waliompa magari husika vinginevyo yakamatwe hadi afanye hivyo ili kuchunguza kama ni halali au ni hila mojawapo ya kuhalalisha utajiri haramu na wa kificho. Haiwezekani usawa huu ambapo watu wengi wanalalamikia ukosefu wa fedha tokana na serikali kuziba mianya ya rushwa na wizi watokee watu tena wasiotajwa majina watoe zawadi kubwa kiasi hiki. Kwa lipi kama siyo sanaa? Je ni wangapi wa aina hii wanaogeuza nchi yetu hamnazo kiasi cha kufanya michezo ya ajabu kama hii? Nimeandika wiki chache zilizopita kuwa hata viongozi wa dini wachunguzwe kwa vile ni watanzania na viongozi wa umma. Napendekeza itungwe sheria ya kushughulikia zawadi kama hizi za akina Lusekelo sawa na inavyowabana viongozi wa serikali. Hii ni kwa sababu zawadi zile zinatokana na madaraka ya umma aliyo nayo mhusika. Hivyo, zawadi zozote anazopewa hazipaswa kuwa mali binafsi kama kweli tutataka kujenga taifa la wawajibikaji na lisiloruhusu wachache kutumia nafasi zao za uma kujineemesha. Kama sheria kama hii itatungwa, inaweza kuzuia au kuondoa motisha wa baadhi ya matapeli kuunda madhehebu ya kidini kwa nia ya kuyatumia kujitajirisha.
            Tumalizie kwa kumtaka Lusekelo aache vitisho na awataje hao wafadhili wake wenye fedha za kumwaga kiasi hicho. Pia namshauri asome Biblia, Mathayo 18:22 pale Yesu anapoulizwa kama alisema kuwa tunapaswa kusamehe mara saba na akajibu tusamehe mara sabini na saba. Pia asome Mathayo 6: 15-15 isemayo, usiposamehe hutasamehewa. Zipo aya nyingi tu ambazo zinaweza kumpa mwanga  Lusekelo akaondoka na aibu na dhambi hizi anazotenda za kujifanya Mungu. Haiwezekani kiumbe dhaifu na mchafu kama mwanadamu akamuamuru Mungu kufanya uovu wala kuruhusu mhusika afanye uovu. Wakati huu si wa kutishana bali kujadiliana.  Ama kweli Yesu alisema, watakuja manabii wengi wa uongo na watadanganya wengi; na pia miti mizuri hutoa matundo mazuri na miti mibaya kadhalika na utaijua kwa matunda yake, Mathayo 7: 16-20. Hapa busara ya Yesu inasema mengi kuhusiana na Lusekelo, vitisho, na vitendo vyake bila kusahau na hizo tabia na “zawadi” zake.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili juzi.

No comments: