The Chant of Savant

Saturday 17 December 2016

Hakikini mali za walevi wote na si wanene tu

            Hivi karibuni, vyombo vya habari viliripoti kuwa sirikali ina mpango wa kuhakiki mali za wanene na wazito ili kubaini wangapi walipiga wakaficha kwa majina bandia au ambao ni wa kweli kama Dk Kanywaji na mimi. Tokana na hili, japo kwa ulevi, nina maangalizo kiduchu.
             Kwanza, naipongeza sirikali kwani kwa kuchunguza mimali hii ya kukwapua itatenda haki kwa walevi hata wapigaji waliotajirika haraka kwa njia za mkato. Sirikali inafanya hivyo ili kubaini kama kuna wanaotumika kuficha mali za wanene waliozipata kinyume cha sheria. Hili ni wazo zuri na mwanzo mzuri wa uwajibikaji na urejeshaji maadili kitaifa.  Hili ni jambo zuri la kupigiwa mfano kuwa sasa kaya yetu inaanza kujiondoa kwenye makucha ya ufisadi, uroho, ubinafsi na ufisi vilivyokuwa vimetamalaki kwa muda mrefu.  Hivyo, nashauri zoezi hili liwe endelevu ili kuepuka kuondoa wezi wa sasa na kuruhusu wezi wa baadaye kuendelea kuliibia kaya yetu huku walevi wetu walio wengi wakiteseka kwa umaskini wakati kaya yao imejaliwa utajiri wa kila aina.
            Pili, ifahamike kuwa si wanene peke yao walioibia na kufilisi walevi na kaya yao. Hata baadhi ya walevi wa kawaida ima walishirikiana na wanene au walishiriki kutokana na fursa za kufanya hivyo zilizojitokeza tokana na ubovu wa mfumo. Kwa mfano, wale wote walioruhusu bandari zetu kuwa mashamba binafsi wasakwe na kushughulikiwa. Pia, wale waliofunga mita ya kupimia wese bandarini kwa miaka mitano na kuacha kaya iingize wese bila kulipiwa ushuru wala kuhakikiwa viwango vyake vya ubora lazima wasakwe na kukamatwa ili haki itendeke.
            Tatu, ikumbuke; mfumo mzima ulikuwa wa kiwiziwizi na hovyo sana kiasi cha kuruhusu kila tapeli ajihomolee kiasi cha kufanya wanaopaswa kuchunguzwa kuwa wengi kuliko wanene na watumishi wa lisirikali.
            Nne, kushughulikia wanene au watumikaji wa umma na wanaodhaniwa kuwa washirika wao ni ubaguzi na mwanya wa kuwaacha wengine waendelee kufaidi mali za wizi bila stahiki yao.
            Tano, uhakiki wa mali uwe ni wa kaya nzima kuanzia walevi wa kawaida hata wanene wa dini ,taasisi binafsi, na kila mmoja ili haki itendeke sawa kwa wana kaya wote. Mfano ulio wazi ni ile hali ya kuibuka wanene wa majoho wengi matajiri wakati kazi ya kuhuburi wanayofanya haina malipo wala utajiri. Je hawa wanaramba sadaka au kutumia misamaha ya kodi kujitajirisha? Kama siyo hivyo, waeleze wanavyoweza kupata ukwasi wa ghafla bin vu hivi kwenye kaya maskini wakati hawafanyi kazi zaidi ya kupiga kelele. Tena ngoja niweke msisitizo kuwa mahubiri ima yafanyike siku zisizo za kazi au baada ya kazi. Nani anaweza kula au kunywa mahubiri? Akikutwa mlevi anahubiri saa za kazi akamatwe kama mzuraraji wa kawaida. Maana “Hapa ni Kupiga Mzito Tu.” Kimsingi, jamaa zangu wa majoho hasa wale wa kujipachika wanapaswa kuchunguzwa sana hasa ikizingatiwa kuwa Yesu au Mtume Mohamad walikuwa maskini wa kawaida waliotumia kila walichopata kula na si kuwala waumini wao. Jamaa zangu wa majoho wanapaswa kuiga mfano wa hawa viongozi waasisi wanaowahubiri. Tujikumbushe wosia wa Yesu kuwa ni heri ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kwenda mbinguni.
            Sita, hata wafanyabiashara ambao shughuli yao ni ya kuleta utajiri tuwachunguze ili kuona kama biashara na utajiri wao ni halali. Kama wanalipa kodi na kufanya biashara halali. Maana, tunao wafanyabiashara matajiri hadi wengine kuwekwa kwenye kundi la mabilionea wakati utajiri wao umetokana na kuuibia umma. Rejea mfano tajiri mmoja ambaye kampuni yake ya Kagoda ilishiriki wizi wa fedha za umma kwenye kashfa iliyotikisa nchi ya EPA.
            Saba, wale watakaopatikan na mali haramu wataifishwe na kufikishwa mahakamani ili watakaopatikana na hatia waadhibiwe ndiyo haki itendeke kwao na kwa taifa.
            Kumbe sijapata kanywaji! Ngoja nikitoe kwenda kuongeza mafuta. Message sent and received. Kama niliyosema yamekuudhi au kukukwaza ujue unapaswa kuchunguzwa. Kama umeyafurahia basi ujue wewe ni mlevi hata kama hunywi.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: