The Chant of Savant

Thursday 29 December 2016

Kakoko wataje wanasiasa wanaotaka kukukwamisha bandarini

            Hivi karibuni, vyombo vya habari vilipoti kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) Deusdedit Kakoko akisema “wapo wanasiasa wakubwa wakiwamo wabunge wananiambia kwamba vita ya flow mita kamwe sitaiweza, nawaambia sitaki kuingiliwa na mwanasiasa yoyote nitafanya kazi zangu kulingana na maagizo ya Rais John Magufuli, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mawasiliano (Profesa Makame Mbarawa).” Je haya ni ya kweli; na kama ni ya kweli, kulalamika kunatosha?
            Ukiangalia nafasi ya Kakoko, madai yake na aliwaowatuhumu utagundua kuwa haya ni madai mazito yanayohusu mambo mazito na watu wazito. Hivyo, hayawezi kuchukuliwa kirahisi na kuacha yapite bila kudurusiwa. Kwanza, tunadhani Kakoko hakukurupuka wala kutaka sifa hasa ikizingatiwa kuwa, kwa nafasi yake, hana sababu ya kufanya hivyo.
            Pili, tunadhani mtoa madai, kisheria, ana wajibu wa kuthibitisha madai yake kwa kutoa ushahidi. Je hao wanaomtishia Kakoko kuhusiana na kutaka kulinda ufisadi kwenye mita za kupimia mafuta ni akina nani? Kakoko anapawa kuwataja ili watanzania wawajue wanaotaka kuwakwamisha ukiachia mbali rais kuwajua na kuwatumbua haraka iwezekanavyo?
            Tatu, tunamtaka na kumshauri Kakoko awataje haraka ili kuondoa mazoea ya baadhi ya wakubwa wanaotumia dhamana ya umma kutoa madai mazito juu ya mambo nyeti bila kutoa ushahidi wa kile wanachodai. Haya yameanza kuwa mazoea ya ajabu. Bila kutoa maelezo na ushahidi Kakoko anarejea kile kilichotokea hivi karibuni kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda aliyedai kutaka kuhongwa milioni 50 kwa mwezi ili aruhusu shisha liuzwe ukiachia. Hadi tunaandika, Makonda ima kwa hiari au kulazimishwa na vyombo husika hajatoa ushahidi kuhusiana na madai yake makubwa hivyo tena yanayowahusu wakubwa. 
            Mbali na Makonda, Waziri wa Ardhi, William Lukuvi naye aliyewahi kutoa madai kama haya bila kutoa ushahidi kuwa kuna walanguzi wa ardhi walitaka kumhonga mabilioni ya shilingi bila ya wahusika kuwataja waliotaka kufanya hivyo. Kama Makonda, vyombo husika havijambana mhusika kutoa ushahidi ili kuwashughulikia wahusika.  Ni ajabu kuwa hata vyombo vinavyoshughulikia jinai kama hizi vimekaa kimya bila kutoa maelezo ni nini kimefuatia na ni nani walitaka kutenda makosa haya. Je hawa wakubwa wanaotoa madai bila kutoa ushahidi si washirika wa wale wanaowatuhumu hasa ikizingatiwa kuwa wameamua kuficha majina yao kwa faida wajuazo? Je umma utaendelea kugeuzwa mabwege wa kupokea kila uongo unaolenga kuwajenga wahusika na kuwaonyesha kama wachapakazi waaminifu wakati ukweli wa mambo unaweza kusema tofauti?
            Kakoko kama mtendaji mkuu wa TPA anapaswa ataje majina ya hawa wanasiasa ili washughulikiwe. Sijui wananchi waliomchangua na kumtuma mbunge awawakilishe akaishia kujiwakilisha na kuhujumu taifa lao watajisikiaje watakapogundua kuwa yule waliyedhani ni mbunge wao si wao bali mbunge wa tumbo lake? Hapa ndipo ulazima wa kuwataja watuhumiwa unakuwa muhimu zaidi. Kwani, utawasaidia wananchi wanaowakilishwa na wabunge kama hawa matapeli kujua la kufanya ili kupata mtu safi wa kuwawakilisha bungeni.
            Je baada ya hao wanasiasa wakubwa kutaka kumkatisha tamaa, Kakoko amechukua hatua gani? je aliwahi kuwambia bosi wake ili awatumbue? Je kimya chake kuhusiana na kutochukua hatua mujarabu zinaashiria nini na kujenga dhana gani? Je Kakoko aliogopa nini kuwataja wahusika au kuwaripoti kwa bosi wake kama hakuna namna? Je Kakoko alipotoa madai yake kwa vyombo vya habari alijua namna umma utakavyoyatafakari na kuyafanyia kazi? Ni ajabu.kama mtumishi na kiongozi wa umma wa nafasi na hadhi kama ya Kakoko sawa na Lukuvi na Makonda hajui taratibu za kisheria katika hali kama hii? Je hawa wanangoja nini kwenye ofisi za umma wakati wanaonyesha wazi wasivyofaa?
            Madai ya Kakoko, sawa na ya Lukuvi na Makonda yanaweza kuonekana kama poroja za kisiasa za kutafuta umaarufu kama wataendelea kukalia taarifa nyeti kama hizi zinazoweza kutusaidia katika kupana na ufisadi. Sijui kama rais au wasaidizi wake walisoma habari hii. Je kama waliisoma, wanangoja nini kuchukua hatua au ni yale yale ya kulindana? Sitaki niamini hivyo. Hata hivyo, tokana na unyeti wa safu hii, naamini wahusika wote watapata taarifa juu ya namna umma tunavyofanyia kazi madai yao. Haiingii akilini kwa watendaji wanaojua wazi kuwa wanachoambiwa kufanya ni jinai wakae kimya bila kuwa na maslahi binafsi au mapungufu kiutendaji. Hata kama wahusika ni vipenzi na jamaa za waliowateua, wanapaswa kufahamu kuwa wanashughulikia umma wenye watu wenye akili na wengine hata taaluma kuliko wao. Wanapaswa kujua umma wa wa-Tanzania si mazuzu wa kuweza kupokea machukizo kama habari za furaha kama ilivyo kwenye kadhia hii tunayoongelea leo.
            Tumalizie kwa kumtaka Kakoko achague moja. Ima awataje wahusika huku akiomba msamaha kwa kutochukua hatua mujarabu au aachie ngozi ili kuendelea kuwalinda hao wenzake. Pia tunamshauri rais awe mwepesi wa kuwatumbua watendaji wanaotoa habari za hovyo zinazoonyesha uzembe wao kama hawa watatu tajwa kwenye makala hii bila kujali ukaribu wake nao. Tunadhani Kakoko amepata ushauri wa kutosha. Hivyo, tunangoja utekelezaji. Tunaomba kutoa hoja.
Chanzo: Tanzania Daima jana Jumatano.

No comments: