Image result for kikwete and magufuli
  1. Wiki iliyopita vyombo vya habari viliripoti habari ya kuzuiliwa kwa mzigo bandari wa shirika lisilo la kiserikali la Wanawake na Maendeleo (WAMA) linalomilkiwa na mke wa rais mstaafu.  Habari hii ilichapishwa kwenye magazeti mengi tena makubwa tu yakimkariri Mkurugenzi wa Elimu kwa Huduma za Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo akithibitisha ukweli wa habari husika.  Baada ya habari hii kurushwa, WAMA walitumia baadhi ya mitandao rafiki kukanusha kuwa walikuwa na mzigo uliozuiliwa bandarini.
                Baada ya WAMA kukanusha, kama haitoshi, na ikulu nayo ikatupa uzito wake nyuma yake. Japo ni haki ya ikulu kuwasaidia inawapenda kwa sababu na faida izijuazo, ilipaswa kukanusha ukweli wa habari badala ya kuziita uongo bila kutoa maelezo. Maana, taarifa ya ikulu ilisomeka “nimesikitishwa sana na uzushi unaofanywa dhidi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mke wake Mama Salma Kikwete. Tafadhali wale mnaotengeneza uzushi huu acheni mara moja na muacheni Rais Mstaafu Kikwete apumzike.” Hivi kweli kuzuiliwa mzigo bandarini ili kulipiwa kodi ni aibu au uzushi? Ina maana familia ya Kikwete ina uhuru wa kupitisha mizigo yake bila kulipia kodi na ushuru? Nadhani kama uhuru huu ulikuwapo wakati wa utawala wake, anapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani na kulipia mizigo yake hasa ikizingatiwa kuwa rais aliyeko madarakani, kikatiba, haruhusiwi kufanya biashara.
                Je kwanini ikulu iliamua kusema uongo wa makusudi bila kutoa ushahidi kuwa rais John Pombe Magufuli anahusishwa ili kumchonganisha na Kikwete? Nadhani wanachochanganya hapa ni ile hali ya kusema kuwa serikali ya Magufuli, tokana na uwajibikaji wake, imezuia mizigo ya WAMA. Ndiyo, mamlaka ya Mapato ni sehemu ya serikali; na kuzuia mizigo ni jambo la kujivunia badala ya kuogopana na kutupiana mpira. Japo Magufuli alisema hana mpango wa kufukua makaburi kwa vile hana uwezo wa kuyafukia akimaanisha ufisadi wa kunuka uliozoeleka. Inapotokea mamlaka husika zikafukua makaburi, aziache ziyapekue na kuyafukia bila kuziingilia.
                Kwa taarifa iliyotolewa na ikulu, kama ukiangalia ilicholenga kufanikisha si kingine bali kuwatisha TRA wasiwe wanagusa mizigo ya makampuni ya wakubwa au wake zao wazipe misamaha na upendeleo jambo ambalo ni kujipinga kwa mamlaka na serikali husika. Nani anahitaji WAMA usawa huu? Mbona Mke wa Magufuli hana hiyo NGO na wanawake na watoto wanahudumiwa vizuri na wizara yao? Je ni uzushi? Gazeti moja la Kiswahili litolewalo kila wiki lilikariririwa likikiripoti “Salma amepambana kwelikweli kujaribu kusaidia mizigo ya WAMA itoke bandarini. Tatizo ni kwamba hivi sasa mambo ya misamaha ya kodi yanapigwa vita na kila mtu anatakiwa kuchangia,” gazeti lilikaririri vyanzo vyake kutoka WAMA.
                Je mtu akisema kuwa serikali ya Magufuli imezuia mizigo ya WAMA ni dhambi au uongo wakati ukweli uko wazi? Kama siyo kukosa kujiamini, ikulu haikupaswa wala kupoteza muda wake kukanusha kitu ambacho ni kweli na wazi kuwa mizigo husika ilikamatwa.  Mbona juzi mke wa rais alipolazwa Muhimbili ikulu haikunusha au ni kwa vile ni habari inayomjenga mkubwa wan chi? Kwa watu wawajibikaji na watenda haki, wawajibikaji na wasio waroho, kitendo cha kuzuiwa mizigo ya WAMA ni cha kujivunia kwa serikali kuwa haina ubaguzi wala upendeleo.  Hata hivyo, kwa waliozoea vya dezo na kujionyesha kuwa hawana kasoro, kuzuiliwa mzigo ni aibu ya kufanya watu wahangaike kukana kitu kilicho wazi. Ni aibu kiasi gani na tunajenga jamii ya namna gani? Wakati mwingine kutojua sheria ni tatizo. Kama sheria inasema kila anayepitisha mzigo bandarini sharti alipie ushuru au kodi, basi, hata mwenye kupitisha mzigo angekuwa Mungu atapaswa adaiwe kodi na ushuru. Mbona Magufuli aliwaamuru Air Tanzania kumtoza hata yeye nauli huku akisema kuwa kuna tabia ya kujipendekeza kwenye baadhi ya mashirika ikiwa ni sababu mojawapo ya kufilisika na kushindwa kujiendesha kwa faida?
                Hata ukiangalia majibu na nafasi ya Kayombo, unashindwa kuelewa hawa waliotoa tangazo la kukanusha kama ni wa kweli kwa nafsi zao. Hivi mkurugenzi mzima wa elimu ya walipa kodi ana shida gani hadi kujiingiza kwenye kutoa habari za uongo; ili apate nini?
                Ukweli unaweza kuupata kwenye kauli ya Katibu Mtendaji wa WAMA, Daudi Nassib iliyokaririwa na gazeti akisema “unajua haya mambo ya kuchelewa kulipa yapo. Lakini hivi sasa tuna uzoefu kwa sababu tumeanza kulipia kodi muda kidogo. Tunalipia kodi hata kwa vitu kama kompyuta na vitabu ambavyo wanatumia watoto hawa kujielimisha. Lakini ndiyo taratibu na lazima zifuatwe.” Hakuna kitu kinachokera kama hii biashara ya kizamani ya wake za wakubwa. Salma si first lady tena. Anaendelea kung’ang’ania NGO kama kweli si mali binafsi kama ya Anna Mkapa kama nani? kama kuna kitakachowachonganisha Kikwete na Magufuli si kingine zaidi ya kutumikia mabwana wawili yaani wananchi na watawala wastaafu. Hapa lazima Magufuli achague moja; au aache kila mtu abebe msalaba wake au awabebe wakubwa wenzake umma umjue yeye ni nani ikilinganishwa na yule waliyemchagua kuwakomboa na kadhia walizoanzisha hao hao anaotaka kuwatetea na kuishi na kwa amani huku akiwaudhi wananchi.