The Chant of Savant

Thursday 22 December 2016

Makonda aeleze anavyopata pesa anayotoa

Hivi karibuni vyombo vya habari vilipoti kuwa mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda alitimiza ahadi yake ya kutoa fedha taslimu za mitaji na vifaa vyenye thamani ya shilingi 164 272, 000 kwa baadhi ya wakazi wa Dar Es Salaam aliowahaahidi kufanya hivyo. Sijui mshahara wa Makonda. Ila kwa nijuavyo uchumi na kiwango cha mshahara wa Tanzania, hii fedha si kichele hata kidogo.
Je Makonda anatoa mfukoni mwake? Na kama anatoa mfukoni mwake ametengenezaje utajiri huu kwa muda mfupi aliokuwa madarakani? Je anachangiwa; na kama anachangiwa, ni akina nani hao wanaofanya hivyo? Pamoja na nia njema, uzoefu umeonyesha kuwa hata wahalifu wengi hupenda kutakasa fedha zao na kuwa karibu na wakubwa kwa kutoa michango itokanayo na fedha chafu. Rejea namna baadhi ya wafanyabiashara waovu walivyokuwa wakichangamkia kununua leso au hata soksi za rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi lakini wakaacha kufanya hivyo alipoachia madaraka. Rejea hata namna ya wafanyabiashara wenye kutia kila aina ya shaka walivyokuwa wakichangia NGOs za marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete lakini sasa wasifanye hivyo. Hivyo, kama serikali imeamua kuchunguza namna watu walivyopata utajiri wao lazima na Makonda aeleze hata kuchunguzwa namna anavyotengeneza fedha yake bila kujali yuko karibu mbali au karibu na rais.
            Hapa tunaongelea milioni mia na ushei. Vunja rekodi ni pale Makonda alipoahidi kulijengea Baraza Kuu la Waislam  Tanzania (BAKWATA) makao makuu yenye thamani ya shilingi bilioni tano na ushei. Na tunapoandika, vyombo vya habari vimeisharipoti maendeleo makubwa ya mradi huu. Huyu si mtu wa kawaida. Lazima awe na namna anavyotengeneza fedha. Tungependa aiweke wazi ili iwasaidie viongozi wengine  waweze kuwakwamua watu wao. Muhimu ningependa kujua siri ya Makonda ili amsaidie rais John Pombe Magufuli naye afanye mambo makubwa kama anayoyafanya.
            Sitaki kuonekana kama natia chumvi. Huyu bwana kwa sasa anaonekana kuwa Bwana Mapesa aka moneybag ambaye akisema lazima liwe. Hapa lazima kuwa na namna iwayo yoyote ile iwe halali au haramu. Pia nichukue fursa hii kuwaomba wale mashabiki wa Makonda kutoniona kama namuonea wivu au kuvuruga ulaji wao. Hasha. Wakati huu wa uwajibikaji lazima kila kitu kiwe wazi hasa ikizingatiwa kuwa sote ni binadamu tunaoshughulika na masuala ya umma. Ninachojaribu kutetea hapa ni utaratibu na mfumo wazi wa kisheria usio na kujuana wala kupendeleana.
            Kwanza, siamini katika utegemezi wa misaada. Wachina wana msemo kuwa ukitaka kumsaida mtu mfundishe kuvua na si kumpa samaki.nasi kadhalika, badala ya kutegemea viongozi kutuchungishia vijifedha vyenye kutia shaka, wajenge mazingira ya kutengeneza utajiri wa kujitegemea.
                        Pili, kama nilivyosema hapo juu, Makonda ni binadamu tena maskini sawa na wengine. Je tutajuaje kuwa hapo alipopata hiyo fedha ni hizo tu zilizopatikana? Je kuna chombo gani cha umma kinachosimamia huo upatikanaji wa fedha kama anachangiwa? Nijuavyo, ukiachia fedha za michango ya harusi, sheria ya Tanzania hairuhusu mtu kuwachangisha wenzake kwa sababu yoyote bila kusimamiwa na serikali. Nasema. Makonda ni mtu binafsi anayetumia nafasi yake kujijenga kisiasa hata kama anayofanya yana wengi wanaoyashabikia. Tunasema hivi kwa vile yeye ni mkuu wa mkoa. Asingekuwa na mamlaka aliyo nayo, hiyo fedha wala asingepata hata moja ya kumi yake.
            Tatu, najua kuwa tokana na umaskini na utegemezi wa wengi wetu, wengi wanafurahia hii misaada isiyojulikana inakotoka. Kiuwazi, uwajibikaji na utawala bora, lazima mhusika aeleze anavyopata hiyo fedha.ni bahati mbaya hata vyombo vya habari vilivyoripoti neema hii, vilishindwa kumuuliza Makonda ilikotoka fedha hii na vigezo gani alitumia kuwateua hao aliowapa hiyo fedha na vifaa. Tusisitize kuwa hatuhoji misaada hii kwa nia mbaya. Uzoefu wetu unaonyesha kuwa kuna wakati mwingine misaada inaweza kuonekana mizuri lakini ikawa na matukio mabaya. Mfano wa karibuni ule wa rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi. Huyu bwana alipenda kumpa kila aliyemtembelea mabulungutu ya fedha. Baada ya kung’oka aligundulika kuwa alikuwa amefanya ufisadi mkubwa ili kujijengea sifa ya kuwa mkarimu kiasi cha kupendwa wakati nyuma ya pazia alikuwa mwizi na fisadi wa kawaida. Moi anasifika kwa kutumiwa na wafanyabiashara wa kihindi kufikikia karibu kuifilisi kenya chini ya kashfa maarufu ya Goldenberg.
            Mfano wa pili ni ile hali ya rais Magufuli kusema wazi kuwa hakuruhusu wafanyabiashara wamchangie wala kumdhamini wakati akitafuta urais. Hii imempa jeuri ya kutekeleza mipango yake kwa umma bila kusumbuliwa na wafadhili. Sijui kama Makonda analikumbuka hili.
            Tumalize kwa kusema yafuatayo:
            Mosi, wananchi wanataka mazingira ya kujijengea uwezo wa kujiletea maendeleo na taifa na si ufadhili ambao uzoefu wetu umeonyesha kuwa ni udhalilishaji na wenye nia ya kurejesha fedha zake kwa faida.
            Pili, Makonda aeleze kinagaubaga anavyopata hiyo fedha; na vigezo anavyotumia kuwateua wa kuwapa hiyo fedha. Je ana kibali cha kufanya hivyo? Je fedha husika inaratibiwa na taasisi gani ya umma kulingana na sheria? Je hiyo fedha inalipiwa kodi? Je yuko tayari kuwataja wanaomchangia?
            Mwisho, tunamshauri Makonda aige mfano wa rais Magufuli ambaye fedha yote aliyotumia kufanya mambo ambayo wengi hawakutegemea kama kuondoa posho bungeni na kuelekeza kwenye barabara na hospitali amezitolea maelezo hata kabla ya kuombwa kufanya hivyo.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano jana.

No comments: