The Chant of Savant

Saturday 28 January 2017

Bongo kuna jaa si njaa


          Kuna mjadala ulioniacha hoi hivi majuzi. Mjadala wenyewe ni juu ya kuwa kama kuna baa la njaa Kayani au la? Upande wa utawala unasema hakuna kitu kama hii wakati upande wa upingaji ukizidi kukoleza moto kudai hali ni mbaya. Baada ya sintofahamu na mparaganyiko utokanao na madai kama haya, Mlevi nimeamua kuingilia kuamua ugomvi usio na tija kwa kaya na walevi wake. Wakati wawili tajwa wakigombea nani mwenye mamlaka ya kutangaza balaa, mie nitajitenga na mjadala huu. Badala yake nitajikita kwenye mambo ya kifalsafa na kilevi lau niwape shule ya bure. Hivyo, naelekea suala hili kwa kuangalia yafuatayo:
            Mosi, je Bongo pamoja na kuwa na ardhi yenye rutuba kiasi ilicho nacho inaweza kukumbwa na baa la njaa au balaa la akili za njaa? Haiingii akilini kwa kaya kama hii kukumbwa na baa la njaa kama itatumia akili za shibe na si za njaa na kuombaomba kama ilivyokuwa chini ya Njaa Kali na watangulizi wake akina Dugong Makapi.
            Pili, inakuwaje kaya yenye walevi milioni zipatazo 50 kukumbwa na baa la njaa wakati wa akili na mikono zana wanazohitaji kuwekeza kwenye ardhi na rutuba yake na kuweza kujilisha na kulisha wengine. Sitegemei walevi kulishwa makapi toka kaya zenye wenye njaa kali kama vile Uchina na Ugabacholi, Sirilanka na kwingineko. Mtalishwa sumu hasa ikizingatiwa jamaa hawa wanavyowabagua weusi.
            Tatu, tukiachana na akili za njaa zenye kuweza kuleta njaa, inakuwaje kaya yenye mito na maziwa kukubwa na njaa wakati ina uwezo wa kulima hata wakati wa ukame? Hapa tatizo si njaa bali jaa la ujinga na kutokutumia upstairs vizuri. Hapa lazima tukubaliane kuwa zama za kutegemea matone ya mvua wakati yamejaa kwenye mito na maziwa umeishapita siku nyingi. Badala ya kuwekeza kwenye siasa majukwaani mkirushiana vijembe na hata wengine kuzua, wekezeni kwenye mipango ya maana inayoweza kukomboa kaya yenu tokana na balaa la njaa kuanzia vichwani, mioyoni hadi matumboni. Naweza kusema wazi kuwa kama kuna njaa inayoweza kusababisha baa la njaa si nyingine bali njaa ya kichwani ambapo wenye kuwa nayo hupiga domo bila kuchapa kazi.
            Juzi kuna mwanasiasa wa upingaji aliniudhi nusu nipasuke. Huyu jamaa anaitwa Mzito Kabwela. Si alidai kuwa rahis anaogopa kutangaza kuwa kaya inakumbwa na balaa na njaa. Kwani rahis ndiye anayetengeneza mvua au njaa kiasi cha kuogopa kuitangaza? Kwani rahis ndiye aliyewapa baadhi ya walevi njaa vichwani hadi aogope kutangaza njaa ya tumboni? Kwanini rahis atangaze kitu ambacho hakipo au cha kujitakia?
            Kama tutakuwa wakweli kwa nafsi na mawazo yetu, lazima tukiri. Tuna tatizo tena kubwa tu. Mfano, tunafyatua vitegemezi vingi kiasi cha kuongeza mzigo bila kusahau tunavyoruhusu wakimbizi wengi wa kiuchumi kuja kula vyakula vyetu kiasi cha kuanza kuhofia njaa. Wakati mwingine huwa nawashangaa waswahili na mapenzi yao ya mshumaa kama si ujinga. Wakati wanafukuzwa majuu na kuonekana kama balaa kwa maendeleo na tamaduni za majuu, kaya zao zinaendelea kukaribisha wakimbizi wa kiuchumi hasa toka Uchinani na Ugabacholini? Ninapoongelea jaa na njaa ya mawazo ninamaanisha hii? Hivi ni mswahili gani anaweza kwenda Ugabacholini akaruhusiwa kukaa  au kutajirika kinyume cha sheria kama ilivyo hapa? Tieni akilini.
            Haiwezekani mkaishi kama wanyama mbugani bila vitambulisho mkawa salama wakati mmezungukwa na kaya zenya njaa na vita. Ni vyakula kiasi gani vinapenyezwa mipakani tokana na kutokuwa na usalama? Leo mnalalamika njaa. Ngoja itakapoanza njaa ya wanyama wetu ndipo mtashika adabu. Ni mara ngapi tunaambiwa kuwa kule akina Nshomile kuna wafugaji toka kaya jirani wamevamia kaya kusaka malisho wakati ndugu zetu akina Ng’wadera wakihaha kusaka malisho hadi kupotelea Selous. Hii ni akili au jaa?
            Kwa vile sijanyaka kanywaji, acha  leo nikomee hapa huku nikishauri wanasiasa waache ugomvi na urongo visivyo na sababu. Waseme ukweli kuwa kayani tuna jaa na njaa ya mawazo lakini si njaa. Waache kusambaza njaa na urongo. Na badala yake kila mmoja aje na mipango yake ya kuonyesha kuwa hana njaa upstairs na mingine ya kupambana na njaa na jaa vinavyonyemelea kaya kwa kujitakia.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: