The Chant of Savant

Thursday 5 January 2017

Magufuli nawe timua wamachinga wa kisiasa

        Image result for photos of wakuu wa mikoa    Hivi karibuni kulitokea malalamiko kuwa baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wasiojua mipaka ya madaraka yao wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi tena kwenye mikoa na wilaya zao. Hili si jambo zuri kwa maendeleo na uongozi bora kitaifa.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya, alipokuwa akisoma risala katika mkutano mkuu wa sita wa shirikisho hilo mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa alikaririwa na vyombo vya habari akisema“Sisi kama viongozi wa vyama vya wafanyakazi, hatukubali jinsi viongozi hao pamoja na wanasiasa wengine, wanavyowafukuza kazi watumishi kwa kutaka mambo yao yaende vizuri.” Je kama wafanyakazi wenye kujua mambo wananyanyaswa, hao wananchi kawaida wa vijijini wanavumilia maonevu kiasi gani? huu ni mfano tu. Rejea juzi baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya walivyokuwa wakiwatimua wamachinga tena bila kuwaandalia mazingira ya kufanyia biashara stahiki kabla ya rais kuwapiga stop.
            Unyanyasaji uonatendwa na baadhi ya wateule wa rais ni tatizo kitaifa. Hata hivyo, nani wa kulaumiwa. Nadhani kama tutarejea historia ya utawala wa kikale wa chama kimoja, tunaweza kujua ni kwanini Tanzania imekuwa na wakuu wa mikoa na wilaya tena wasiochaguliwa na wale wanaopelekewa kuwaongoza. Wanateuliwa na mtu mmoja yaani rais. Hii nadhani ilifanyika wakati wa utawala wa chama kimoja tokana na ile hali ya chama kuwa na nguvu kuliko serikali. Hivyo, chama kilitafuta namna ya kuibana na kuisimamia serikali kwa njia ya kuhakikisha mwenyekiti wake anakuwa rais. Hivyo, aliamua kutumia nafasi hii kuwateua wanachama wenzake kwenye nafasi za kiserikali ili kuweza kumsaidia kutumia kofia cha chama kufanya kazi za kiserikali na kukifaidi chama.
            Sasa ni miaka mingi tangu tuachane na utawala wa chama kimoja. Hata hivyo, pamoja na kuanzisha mfumo wa vyama vingi kinadharia, kivitendo, Tanzania bado ina mabaki na makovu mengi ya utawala wa chama kimoja. Hapa ndipo mgongano unaoanza kujitokeza baina ya wakuu wa mikoa na wilaya na wanachi unapoibua chimbuko lake.
            Kwa vile mambo yanaendelea kubadilika, ili kuwa na viongozi wenye kuweza kuleta ufanisi bila migongano na wananchi, tunapaswa kubadili mfumo wetu. Kwanini kwa mfano rais wa nchi ambaye ndiye mwenye mamlaka makubwa achaguliwe na wananchi lakini si wakuu wa mikoa au wilaya? Tokana na kwamba Tanzania si nchi ya majimbo, wengi watasema kuwa kuruhusu kuchaguliwa kwa wakuu hawa kutakuwa kinyume na mfumo wetu.  Kwanini tusiwe ha hybrid system yaani mfumo kizalia au mchanganyiko ambapo tutakuwa na viongozi wote waliochaguliwa na wale wanaowaongoza ili kuleta uwajibikaji wa kweli badala ya wahusika tulio nao sasa kuwajibika kwa mtu mmoja aliyewateua kiasi cha kuwadharau na kuwanyanyasa wananchi? Kama rais ni mwenyekiti wa chama tawala na anaongoza nchi, kwanini wenyeviti wa mkoa wasichukue nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya ambao wanaonekana kama wakoloni kwenye maeneo yao? Hii itasaidia kuondoa unafiki wa sasa ambapo makada wa chama tawala wanapewa nafasi za kiserikali na kujifanya hawapendelei wakati wanapendelea wazi wazi? Pia kuruhusu wakuu wa mikoa na wilaya utasaidia kufanya mambo yafuatayo:
            Utaondoa ukale wa rais kuwateua marafiki au watu wake wa karibu kama sehemu ya kupeana ulaji hata kama wahusika wanaweza wasifae kwenye nafasi husika.
            Pili, kutaondoa kiburi na dharau kwa watawaliwa tokana na ukweli kuwa wahusika watakuwa wamepitia kwenye mikikimiki ya kufikia walipo. Nakumbuka juzi rais John Magufuli alipositisha zoezi la kufukuza wamanchinga mijini alisema kuwa wakuu wa mikoa na wilaya wanafanya hivyo kutokana na kutojua ugumu wa kusaka kura. Kwa vile ni wateule wa rais, wengi wanajiona miungu watu wasiokosea na wasioguswa. Rejea hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam kumuita afisa wa wilaya kichaa wakati si kichaa ukiachia mbali kuwahi kumweka ndani mbunge wa Ubungo Saidi Kubenea na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Kinondoni alipokuwa mkuu wa wilaya.
                        Tatu, kutaondoa dhana kuwa wakuu husika ni wakoloni waliopelekwa na rais kwenye mikoa na wilaya kutawala na si kuongoza. Na hili lina ukweli usiopingika kuwa wengi wa wakuu wa mikoa na wilaya hawajui shida, tamaduni na mahitaji ya mikoa wanakopachikwa na kuishia kufanya kazi kumridhisha aliyewateua au kuwadharau hata kuwadhalilisha wananchi.
            Naweza kutumia mfano wa Magufuli wa kuwakaripia baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya waliokuwa wakiwabughudhi na kuwafukuza wamachinga nao kuwa wamachinga wa kisiasa. Hivyo, naweza kumshauri Magufuli kuanza kuwafukuza wamachinga hawa wa kisiasa ambao wameanza kuonyesha udhaifu wa mfumo wetu.
            Tumalizie kwa kumhimiza rais na serikali yake waangalie namna ya kubadili sheria ili kuondoa manyanyaso na migongano isiyo na ulazima. Kwani inachelewesha taifa letu licha ya kuwaumiza watu wetu. Wakati wa kufadhiliana kisiasa umepitwa na wakati hasa wakati huu wa “Hapa Kazi Tu”.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo. 

No comments: